33.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

WAAJIRI ZAIDI YA 700 HAWAPELEKI MAKATO MIFUKO HIFADHI YA JAMII

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

ZAIDI ya waajiri 700 wamebainika kutokuchangia makato ya wafanyakazi wao katika mifuko ya hifadhi ya jamii nchini.

Waajiri hao wamebainika kupitia kanzidata ya taifa ya sekta ya hifadhi ya jamii ambayo hukusanya taarifa kutoka taasisi mbalimbali kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Hayo yalielezwa jana wakati wa utoaji wa tuzo ya ubunifu kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zilizotolewa na Umoja wa Afrika (AU).

SSRA ilipata tuzo hiyo baada ya kubuni mradi wa kanzidata ya taifa ya sekta ya hifadhi ya jamii (NSSCDB) wenye lengo la kupanua wigo wa hifadhi ya jamii kwa kutumia Tehama wakati TRA ilipata tuzo hiyo baada ya kubuni mfumo wa kurahisisha upakuaji wa mizigo bandarini ambao pia umeunganishwa na mifumo mingine (TanCIS).

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkuu wa Mawasiliano SSRA, Sarah Kibonde, alisema kupitia kanzidata hiyo waliweza kupata taarifa kutoka TRA zinazohusu walipaji kodi ya mapato (PAYE) zilizofanikisha uchambuzi wa waajiri wasiochangia mifuko ya hifadhi ya jamii.

“Mamlaka tayari imewasiliana na wizara mama (Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu) ambapo kupitia maafisa kazi watafanya kaguzi na kuwatembelea waajiri hao,” alisema.

Alisema pia kupitia mradi huo taarifa za wanachama milioni moja zimerekebishwa na hivyo kuwezesha upatikanaji mafao kwa wakati.

Alisema hadi kufikia Juni mwaka jana mamlaka hiyo ina wanachama milioni 2.4, wastaafu 106,781 huku mafao yaliyolipwa yakiwa ni Sh trilioni 2.9.

Naye Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi (TRA), Richard Kayombo, alisema mfumo wa TanCIS umerahisisha upakuaji mizigo bandarini na kuondoa mianya ya rushwa.

“Kupitia mfumo huu unaweza kujua upakuaji mizigo umefikia hatua gani au umekwama wapi, wakala wa forodha anaweza kukabidhi nyaraka popote alipo bila kuonana na mtu uso kwa uso na mteja sasa anaweza kufuatilia mzigo wake kwa kutumia simu ya mkononi,” alisema.

Alisema tangu kuwapo kwa mfumo huo mapato yameongezeka na mizigo imekuwa ikitolewa kwa haraka zaidi tofauti na hapo awali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles