Na AHMED MAKONGO-BUNDA
VIONGOZI mbalimbali wakiwamo wakuu wa wilaya, wabunge na madiwani wa Halmashauri za wilaya ya Bunda na Serengeti mkoani Mara, wamelaani kitendo cha udhalilishaji alichofanyiwa mwanamke mmoja katika Wilaya ya Rorya, kwa kuchapwa viboko 30 hadharani.
Inadaiwa kuwa mwanamke huyo alipewa adhabu hiyo baada ya kumtuhumu mama yake mzazi kuwa ni mchawi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti juu ya kitendo hicho, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola pamoja na madiwani kutoka Serengeti, walikiita kitendo hicho kuwa ni cha kinyama.
Viongozi hao walikutana juzi katika mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika mjini Bunda, kupitia mradi wa PS3, unaotekelezwa kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani.
Walisema wanaume wote waliohusika katika kitendo hicho cha kikatili ni vema wakafikishwa mahakamani kwani wanastahili kupewa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia ya kufanya vitendo vya udhalilishaji pamoja na ukatili ndani ya jamii.
“Sisi wabunge tumekuwa tukitunga sheria mbalimbali zikiwemo za kupinga vitendo vya ukatili kama huo aliofanyiwa huyo mwanamke. Kwa ujumla kitendo hicho mimi binafsi ninakilaani sana, maana si cha kiungwana hata kidogo ni cha udhalilishaji wa hali ya juu,” alisema Lugola.
“Mimi kama mwanamke nimeumia sana mwenzetu kufanyiwa unyama huo wa kuchapwa viboko vyote hivyo tena hadharani. Jamii iliyostaarabika kamwe haiwezi kukifumbia macho, lazima tukilaani kwa nguvu zote. Tena wale wote waliohusika wakamatwe na kufikishwa mahakamani ili sheria ifuate mkondo wake,”
alisema Dinnah Ngereja ambaye ni Diwani kutoka Wilaya ya Serengeti.
Hivi karibuni katika mitandao ya kijamii ilionyesha video ya mwanamke mmoja mkazi wa Kitongoji cha Migutu, Kijiji cha Kinesi Tarafa ya Suba wilayani Rorya, akifanyiwa ukatili kwa kuchapwa viboko 30 na wanaume waliokuwa wanapokezana baada ya amri kutolewa na viongozi wa mila kwenye mkutano wa ritongo uliofanyika maeneo ya Mastooni.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Andrew Satta, tukio hilo lilitokea Desemba 23, mwaka jana na tayari watu 10 wakiwemo viongozi watano wa baraza la mila wanashikiliwa na polisi na watafikishwa mahakamani wakati wowote.
Nalaani, nalaani, nalaani mno mno unyama aliofanyiwa mwanamke wa kitongoji cha Migutu,kijiji cha Kinesi Tarafa ya Suba wilani Rorya.Wale wazee waliomhukum na kutoa adhabu ile ya viboko kwa mwanamke yule, wahukumiwe kifungo jela na viboko mara mbili ya alivyopigwa yule mwanamke na wakaozee jela kabisa. Na wale vijana waliohusika kumpiga viboko mama yule, wafungwe jela na wapigwe viboko mara tatu ya walivyompiga yule mwanamke. Nasema hawafai, hawafai tena hawafai kabisa kuishi na jamii yoyote.