33.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

GHARAMA ZA UMEME ZISICHELEWESHE TANZANIA YA VIWANDA

felix-ngamlamgosiWATANZANIA leo wanauanza mwaka na kupanda kwa gharama za umeme, huku wengi wakiwa wameumaliza mwaka uliopita wakiwa wanalia kuhusu kukosa fedha mfukoni.

Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imeridhia ongezeko la bei ya umeme kwa wastani wa asilimia 8.5.

Shirika la Taifa la Ugavi wa Umeme (Tanesco), lilipendekeza gharama za umeme ziongezeke kwa asilimia 18.19. Hili lilikataliwa na Bodi ya Ewura.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Ewura, Felix Ngamlamgosi, sababu zilizotolewa na Tanesco ni kuboresha miondombinu yake, kupunguza malalamiko na kuboresha umeme unaotolewa.

MTANZANIA Jumapili tunaona kupanda kwa gharama ya umeme ni taarifa mbaya kwa wananchi, hasa wa kipato cha chini.

Ngamlamgosi alisema makundi yatakayoathirika na ongezeko hilo la bei ni pamoja na wateja wa nyumbani, biashara ndogondogo za nyumbani na taa za barabarani.

Katika kundi hili Tanesco ilipendekeza ongezeko la kutoka Sh 292 hadi Sh 338 sawa na asilimia 15.8. Hata hivyo Ewura imepitisha ongezeko la Sh 312 pekee katika kila uniti ya umeme watakayotumia.

Habari za umeme kupanda au kutopanda zimekuwa zikibadilika kila mara, hasa midomoni mwa wanasiasa.

Kutokana na hadithi za kuwapo kwa nishati nyingi ya gesi na mafuta, Watanzania wamekuwa wakipewa matumani lukuki, kwamba kupanda bei ya umeme itakuwa historia.

MTANZANIA Jumapili tunashangazwa kuona wananchi wataendelea kuumia na bei kubwa ya umeme mwaka huu.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amewahi kunukuliwa mara kadhaa akisisitiza kwamba bei ya umeme haitapanda bali itaendelea kuwa nafuu.

Profesa Muhongo alipoombwa na gazeti hili juzi atoe ufafanuzi kuhusu taarifa za kupanda gharama za umeme alidai kuwa hana taarifa.

Tukitafakari kwa makini, tunajiuliza Serikali itatimiza lini ahadi yake ya kushusha bei ya umeme badala ya sasa kuendelea kupanda?

Wakati Serikali ikihubiri mapinduzi ya viwanda hasa vidogo vidogo, bei ya umeme isiyotabirika huenda ikachelewesha Tanzania ya viwanda.

Tumeambiwa kwamba kupanda kwa bei ya umeme kutavigusa viwanda vidogo vidogo, minara ya simu na mabango ya matangazo, sekta ambazo zinaajiri vijana wengi na hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira.

Ngamlamgosi alisema kuwa Tanesco ilikuwa inaomba kukusanya Sh trilioni 1.9 kwa kiwango kile cha asilimia 18.19, lakini walibaini gharama halali za kwenda kwa mtumiaji ni Sh trilioni 1.6.

Pamoja na nia ya Tanesco kuimarisha miundombinu yake, bado tunadhani ni bora shirika hilo likafikiria vyanzo vingine ambavyo havitamuumiza mtumiaji wa chini.

Ni kweli Ewura imekataa kupandisha umeme kwa watumiaji wa vijijini, lakini Serikali ijue kwamba vijana wengi bado wanakimbilia mijini kutafuta ajira.

Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha ajira zinapatikana mijini kwa kuweka mazingira bora, ambayo pamoja na mambo mengine ni kufanikisha uwapo wa umeme wa uhakika na wa gharama nafuu ili sehemu zinazotoa ajira kama saluni, hoteli, mamantilie na viwanda vya kusindika matunda ziendelee kufanya kazi kwa ufanisi.

MTANZANIA Jumapili tunaishauri Serikali ihakikishe kauli zake kuhusu nafuu ya umeme ziendane na hali halisi.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles