Na BENJAMIN MASESE – MWANZA
SERIKALI imepiga marufuku taasisi za umma kutuma mizigo au vifurushi kwa kutumia kampuni binafsi za usafirishaji, badala yake zitumie Shirika la Posta Tanzania (TPC), ikidai ni kuziba mianya ya upotevu wa fedha.
Agizo hilo lilitolewa hivi karibuni na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, wakati akizungumza na watumishi walio chini ya wizara hiyo katika kikao maalumu kilichofanyika jijini Mwanza.
Katika kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa ipasavyo pamoja na mambo mengine ya maadili ya kiutumishi, Profesa Mbarawa aliamua kutoa namba zake za simu za mkononi; 0622000001 na 0686955116 ili kuwasiliana naye pale itakapobainika mtumishi anafanya vitendo kinyume na taratibu za kazi.
“Shirika letu lazima lifufuliwe ili lipate mafanikio, hili tutalisimamia kweli kweli na naomba watu tuzingatie maagizo, kama Serikali tunaendelea kufanya maboresho kuanzia kwa watumishi wa kawaida hadi kwa postamkuu, kikubwa ni kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia sheria,” alisema.
Profesa Mbarawa pia aligusia juu ya mali za TTCL na kuahidi kuanza kuzifuatilia kwani alidai wapo baadhi ya waliopanga kwenye majengo la shirika hilo lakini nao wanapangisha wengine.
Alisema hadi sasa majengo ya TTCL hayana tija kwa shirika kutokana na udalali unaofanyika na kuwataka viongozi kuanza kupitia mikataba upya kabla ya wizara kuanza uchunguzi.