33.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

PADRE: SERIKALI IWAKOPESHE WATOTO WA MATAJIRI

padre-mkamwa

NA SHEILA KATIKULA – MWANZA

SERIKALI imeaswa kufanya mabadiliko ya kisera katika sekta ya elimu, kwa kuwakopesha watoto wa matajiri ili kurejesha mikopo hiyo haraka na kutoa misaada kwa watoto wa maskini bila marejesho.

Wito huo umetolewa juzi na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine Mwanza (SAUT), Padre Thadeus Mkamwa wakati wa mahafali ya 18 ya chuo hicho.

Alisema ni muhimu Serikali ikatafuta njia mbadala ya mikopo kunusuru vijana wanaotoka familia maskini na tajiri, kufanya hivyo kutasaidia kupunguza kero ya kuwadai marejesho.

“Mikopo wapewe wanafunzi wanaotoka familia zinazoweza kulipa kwa sababu wanakopesheka, wale maskini wapewe kama msaada ili mradi wawe wanatimiza vigezo.

“Huwezi kuwapa mkopo watu maskini ambao hawawezi hata kulipa ada kidogo, maskini hawezi kukopesheka, iwe mtu au nchi, unamkopesha maskini halafu unafukuzana naye ili akulipe, huo si uchumi… tunajua wazi watoto wa matajiri wamekuwa wakipewa mikopo na ndio hawataki kulipa,” alisema.

Alisema SAUT inaunga mkono uhakiki wa wanafunzi hewa vyeti vya wafanyakazi na walimu kwa kuwa unasaidia kuboresha sekta ya elimu.

Alisisitiza kuwa kazi hiyo ifanywe kwa kufuata vigezo na si kwa kujiamulia mtu kwa sababu ni kiongozi.

“SAUT na vyuo vyake tunaunga mkono uhakiki unaoendelea, tunatoa ushauri uhakiki ufanywe kwa usawa na vigezo, hatutaki chuki ya kubagua vyuo na kuviacha vingine,” alisema.

Kwa upande wake, Askofu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Jude Thadeus Ruwa’ichi, aliyemwakilisha mkuu wa chuo hicho, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, alisema taifa linahitaji wasomi walio na nidhamu, uzalendo na maadili kwani ndio watakaochangia kuijenga nchi katika misingi endelevu ya utu, upendo na kutunza masilahi ya wengi, hususani wanyonge  na maskini.

“Silaha pekee itakayowawezesha kufanikiwa katika maisha yenu ni kufanya kazi kwa maadili na kujitambua kutokana na changamoto ya ajira kwa kujishughulisha na kuacha kusubiri  kuajiriwa na badala yake kujiajiri wenyewe na kutii sheria za kazi, kwani kufanya hivyo kutasaidia kufanya vizuri katika  kituo chako cha kazi,” alisema.

Katika mahafali hayo, wanafunzi 2,421 walitunukiwa vyeti kutoka idara na ngazi mbalimbali za masomo, huku 746 wakishindwa kuhitimu masomo yao kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo kufeli masomo na kushindwa kulipa ada.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles