Na PATRICIA KIMELEMETA – DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde, amesema kuwa idadi kubwa ya watendaji wa sekta ya manunuzi na ugavi si waaminifu, jambo ambalo limechangia Serikali kupata hasara.
Akizungumza jana katika mahafali ya nane ya Chuo cha Ununuzi na Ugavi (IPS), Chanika, Dar es Salaam, Mavunde alisema kuwa hali hiyo inatokana na kuwapo kwa watendaji wasio waaminifu na weledi.
Alisema kutokana na hali hiyo, vyuo vinavyotoa mafunzo ya ununuzi na ugavi vinapaswa kuwajengea uzalendo wanafunzi wao ili waweze kutanguliza masilahi ya taifa kwanza, jambo ambalo linaweza kupunguza ukubwa wa tatizo.
“Tuna tatizo kubwa la baadhi ya watendaji wa sekta ya ununuzi na ugavi kutokuwa waaminifu katika majukumu yao, jambo ambalo limechangia Serikali kupata hasara,” alisema Mavunde.
Alisema kutokana na hali hiyo, Serikali itaendelea kuwachulia hatua watendaji wasio waaminifu ili waweze kurudisha nidhamu ya kazi yao na kufanya kazi kwa weledi na uaminifu, jambo ambalo linaweza kulijengea heshima taifa.
Mavunde alisema kuwa licha ya kuwapo kwa tatizo hilo, lakini pia zaidi ya asilimia 61 ya vijana wanaomaliza vyuo vikuu vya Afrika Mashariki hawana uwezo wa kuingia katika ushindani wa soko la ajira kutokana na kutoiva ipasavyo.
Alisema tatizo hilo limetokana na baadhi ya vijana kutopenda kusoma, huku wengine kutoiva ipasavyo, hali inayowawia vigumu kuingia katika majaribio ya ajira kwa vijana kutoka nje ya Afrika Mashariki.
“Idadi kubwa ya vijana hawapendi kusoma, hata kama wamefaulu, wanapenda njia za mkato au hata kukaa vijiweni na kusubiri maisha ya mteremko, jambo ambalo linawafanya washindwe kufanya vizuri mitihani ya majaribio ya ajira,” alisema.
Alisema hali hiyo imesababisha hata vijana wanaochukua mikopo taasisi za kifedha kuitumia kununua magari ya kifahari badala ya kufanya biashara au kujikita katika shughuli za ujasiriamali ili faida wanayopata iweze kuwasaidia katika maendeleo ya nchi na taifa kwa ujumla.
“Serikali itaendelea kuelimisha vijana ili waweze kubadilika na kujikita katika uzalendo ambao utawajengea heshima na kutimiza majukumu yao ambayo yatawasaidia katika maisha ya baadaye,” alisema.
Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Deo Masaburi alisema kuwa watashirikiana na Serikali kuhakikisha vijana wanaomaliza wanafanya kazi kwa weledi na uadilifu, jambo ambalo linaweza kusaidia kupunguza ukubwa wa tatizo.