JUMANNE ya wiki hii Rais Dk. John Magufuli aliagiza kuwa wafanyabiashara ndogondogo, maarufu machinga, wasibughudhiwe na wasiondolewe katika maeneo ya katikati ya miji wanayofanyia biashara kwani hakuna sheria inayowazuia.
Rais Dk. Magufuli alimwagiza Waziri na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusitisha mara moja utekelezaji wa kuwaondoa wafanyabiashara hao.
Rais akiwa na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan, alitoa agizo hilo Ikulu na kuonya kuwa kiongozi yeyote ambaye hayupo tayari kulitekeleza aachie ngazi.
Kwamba Rais hapendi machinga wafanye biashara kwenye hifadhi ya barabara, lakini hakuna sheria katika nchi hii inayosema mtu wa biashara ndogondogo au machinga hatakiwi kufanya biashara katikati ya miji.
Kwamba Kigamboni hapa Dar es Salaam kulikuwa na machinga ambao wamehama vizuri kweli, wakatengenezewa miundombinu yao katika soko lao na sasa hivi wanafanya kazi vizuri, na viongozi wa machinga walishirikishwa.
 Kwamba machinga wajengewe mazingira ya kufanya biashara na wasizagae. Kwamba wakitaka kuwahamisha wazungumze nao kwa utaratibu mzuri na watakapopelekwa liwe ni eneo rafiki kwao na wafaidike kufanya biashara.
Hata hivyo Rais Dk. Magufuli alitoa onyo kuwa amri yake isiwe chanzo cha wamachinga kufanya biashara na kujenga mabanda kila mahali kwa sababu yanachafua mandhari ya miji.
Lakini sasa hali imekuwa hivyo baada ya baadhi ya mitaa katika miji ya makao makuu ya mikoa mbalimbali nchini kufurika machinga.
Hiyo imetokea siku moja baada ya Rais kutoa agizo kwa wakuu wa mikoa na wilaya kutowafukuza maeneo ya katikati ya miji wafanyabiashara hao.
Katika miji mikuu ya mikoa sasa tangu Jumatano wiki hii machinga walionekana wakiendelea kujenga vibanda na wengine wakipanga bidhaa zao chini.
Mitaa kadhaa, kwa mfano, ya Kariakoo, Dar es Salaam wafanyabiashara hao wameweka shehena kubwa za bidhaa, huku wakiendelea kuzitandaza pembezoni na hata katikati ya barabara bila kujali wapitanjia wengine, hususan wanaotumia vyombo vya moto.
Mitaa iliyosheheni wafanyabiashara hao ni Kongo, Nyamwezi, Swahili, Sikukuu, Narung’ombe na Mchikichi.
Baadhi ya wafanyabiashara wa maduka walionekana nao wakihaha kutafuta nafasi za kutandaza bidhaa zao nje ili nao wasilipe kodi.
Wamachinga wengine walipanga bidhaa zao katikati ya barabara na kufanya magari yashindwe kupita.
Hali ni ya namna hii sasa katika miji yote mikoani nchini.
 Tunakumbusha onyo la Rais kuwa amri yake haina maana kuwa machinga waendeshe shughuli zao kwa kuvunja sheria.
Tunasema lazima wazingatie sheria, wasipange bidhaa zao ovyo mitaani na kuchafua mazingira.
Tunapendekeza pia wamachinga watengewe baadhi ya mitaa huku wakiweka meza kwa mpangilio pembezoni mwa barabara na kuacha nafasi za watu kuingia madukani na kuweka mapipa ya taka.
Tunaamini mpango huu utawezesha kutolewa kwa mashine za kukusanya ushuru na kukagua risiti za wafanyabiashara ili Serikali ipate mapato yake pia.