26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

WAGENI KUTOKA SAYARI NYINGINE WANAPOKUWA GUMZO MAREKANI

Na JOSEPH HIZA-MASHIRIKA YA HABARI


wanasayansi-wengi-wanaamini-binadamu-hatuko-pekee-katika-ulimwengu-huu
wanasayansi-wengi-wanaamini-binadamu-hatuko-pekee-katika-ulimwengu-huu

KWA wadau na mashabiki wa masuala ya anga za juu, mwezi huu wa Novemba ulikuwa gumzo kwao kwa kile kinachoelezwa kuonekana kwa vyombo kutoka sayari za mbali.

Vyombo hivi virukavyo vilivyo mfano wa nyungo au sahani maarufu kama Unidentified Flying Object (UFO), vilinaswa na kamera za ndege zisizo na rubani maarufu kama drone vikipita angani vikitokea mwezini.

Video ikivionesha ijapokuwa kwa mbali imeonekana katika mitandao ya jamii na kuzua gumzo kubwa nchini Marekani na kwingineko hasa magharibi na kuwapa nguvu watetezi wa uwapo wa vyombo hivyo na viumbe kutoka sayari za juu.

Kutokana na utata, Shirika la Sayansi la Anga za Juu la Marekani (NASA) lilichukua video kwa ajili ya uchunguzi wa kina.

Je, kuna ukweli wa uwapo wa vyombo hivi vinavyoaminika kuendeshwa na viumbe kutoka sayari nyingine?

Ni suala lililojaa ubishani mno kwa vile kuna kundi kubwa linaloamini uwapo wake na lile linalopinga iwe majumbani, ofisini, jeshini, serikalini hadi kwa wanasayansi wa anga za juu katika mataifa ya Magharibi.

Limewagawa wengi katika mataifa hayo kutokana na kukosekana kwa uthibitisho usio na shaka huku pia kukiwepo watu wa kuheshimika wanaodai kuviona.

Wakati UFO, vikiwa si maarufu katika nchi zetu pengine kutokana na uduni wa sayansi na teknolojia zetu, wengi wetu hakuna shaka tumeziona hadithi hizo kupitia filamu.

Waongozaji wa filamu walijitosa kuzitengeneza baada ya kuona kuna ushabiki mkubwa kuhusu viumbe hao, wakitumia vitabu au simulizi walizosikia.

Ubishani wa suala hili unaweza kufananishwa na suala la uwepo au kutokuwapo na kile kinachoitwa ‘popobawa’ ambacho kimejizolea umaarufu zaidi katika Visiwa vya Unguja na Pemba.

Kama vile ambavyo popobawa huzua mijadala, ubishaji na hofu ndivyo ambavyo viumbe hawa wa ajabu huvumishwa katika mataifa ya magharibi.

Miongoni mwa uvumi ni kujitosa kwa majeshi ya nchi za magharibi kutafiti suala hilo kunakotokana na hofu kwamba ujio wao duniani ni upelelezi wenye maandalizi ya kuivamia dunia.

Ni sababu zinazochangia kwa mujibu wa watetezi wa uwapo wa viumbe hawa, serikali za magharibi ikiwamo Marekani kutokuwa tayari kulizungumzia hadharani zaidi ili kutoharibu uchunguzi.

Katika tukio la mwezi huu, walioona video za vyombo hivyo na kupata nafasi ya kutoa maoni yao mitandaoni kuna wenye hofu na wale waliopuuza, ambao walisema viumbe hawa licha ya kuwa na teknolojia kubwa kuliko binadamu hawana madhara yoyote kwetu.

Nchini Marekani pamoja na ukimya wa miaka mingi ukielezwa na mashabiki wa viumbe hawa kuwa hofu ya kutovuruga uchunguzi, utawala wa Rais Barack Obama ni pekee uliowahi kugusia hadharani.

Katika hilo serikali ilijibu mashauri mawili yaliyowasilishwa kwa njia ya mtandao, ikisema haijui kuhusu ushahidi wa uwapo wa viumbe hao wala kuonana au kuwasiliana nao.

Hali kadhalika, ilisema hakuna taarifa za uhakika kuonesha kuna ushahidi wowote unaofichwa kuhusu viumbe hawa.

Kitu ambacho serikali ilikiri ni kwamba wanaunga mkono mradi wa utafiti wa upelelezi wa sayari nyingine (SETI) pamoja na programu nyingine kama hizo chini ya Shirika la Sayansi na Anga za Juu Marekani (NASA).

Serikali ilisema wanasayansi wengi na wanahisabati wamekuwa wakitafiti uwapo wa maisha ya kishushushu katika eneo lingine la ulimwengu huu.

Robo ya Wamarekani wanaamini uwapo wa viumbe hawa ambao kwa sasa tunaweza sema wa kufikirika kutoka dunia nyingine, ambayo binadamu bado hajaigundua.

Ni suala linalochunguzwa kwa miaka mingi na kwa namna nyingi kisayansi.

Si serikali ya Marekani pekee bali pia na nchi nyingine kama Canada, Uingereza , Japan, Peru, Ufaransa, Ubelgiji, Sweden, Brazil, Chile, Uruguay, Mexico, Hispania na Urusi, ambazo zinafahamika kwa kuchunguza ripoti za uwapo wa UFO.

Kaika kuonesha jinsi suala hilo linavyovuta hisia za wengi, kuna upanuzi wa michezo na vipindi vya runinga katika mada za viumbe vya ajabu na kile wanachokiita uvamizi unaohatarisha maisha ya mwanadamu ulimwenguni.

Wakati kiufundi UFO hurejea vitu visivyojulikana virukavyo, katika utamaduni wa kisasa neno UFO kwa sehemu kubwa limekuwa likihusisha dude kama ndege mara nyingi lenye umbo la mviringo lirukalo.

Wakosoaji wanasema vitu hivi vinaonekana kutengenezwa kwa siri na mwanadamu na baadaye kuvumishwa kuwa ni kutoka anga za juu.

Lakini watetezi wake wanasema kuonekana kwa ndege hizo au umbo kama hilo linaloonekana katika teknolojia isiyofahamika miongoni mwa ndege tuzijuazo ni hitimisho kuwa kamwe hazitoki Duniani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles