33.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kipato cha Mtanzania kwa mwaka dola 900

dola-900

Na LEONARD MANG’OHA

DAR ES SALAAM

LICHA ya taarifa za Benki ya Dunia (WB) kuonyesha kuwa pato la chini zaidi kwa mtu mmoja kwa mwaka linapaswa kuwa dola za Marekani 3,000, kwa hapa nchini pato hilo ni kati ya dola 900 na 1,000, hali inayotajwa kusababisha Watanzania wengi kulalamikia ugumu wa maisha.

Kauli hiyo ilitolewa na Meneja Takwimu za Pato la Taifa Ofisi ya Takwimu ya Taifa, Daniel Masolwa, katika maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.

Masolwa alisema ikiwa Taifa litafanikiwa kuimarisha sekta muhimu kama vile kilimo na viwanda, ambavyo vitasaidia kutoa ajira kwa Watanzania walio wengi, itawezesha kufikia malengo hayo ya WB na kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi.

“Tunatakiwa kutoka katika kilimo cha jembe la mkono na kwenda katika kilimo kinachozalisha kwa kiwango kikubwa kinatakachotosheleza mahitaji ya chakula na kuhakikisha mazao yanayozalishwa yasiuzwe yakiwa ghafi, badala yake yaongezwe thamani kwa kuyasindika na kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Suala la viwanda ni la lazima kwa sababu usipokuwa na viwanda unageuka kuwa soko la bidhaa za wengine, hivyo ni lazima kuanzisha viwanda na kutafuta masoko ya ndani na nje kwa ajili ya mazao ya wakulima,” alisema Masolwa.

Aliongeza kuwa, takwimu zinaonyesha kuwa kilimo kimechangia asilimia 29 ya pato la taifa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, hivyo kutokana na ukosefu wa mvua za kutosha katika robo ya mwisho ya mwaka huu, ni wazi kuwa pato la Taifa litatetereka kutokana na uzalishaji wa mazao ya kilimo kutegemewa kushuka.

“Tunapopambana kukuza uchumi tunapaswa pia kuzingatia umuhimu wa kutunza mazingira ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira, unaochangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya tabianchi ili kuendelea kuwa na mazingira yanayoruhusu kufanya shughuli za kilimo,” alisema Masolwa.

Mmoja wa wakufunzi waandamizi kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dk. Camillus Kassala, alisema mfumo wa ugawaji wa pato la taifa ndio unaosababisha kuwapo kwa tofauti kubwa ya pato kati ya mtu mmoja na mwingine.

“Ili kupata mgawanyo mzuri, ni lazima kujua unakusanya kiasi gani na idadi ya watu ulionao ambao ndio wahitaji”.

Kassala alisema takwimu nyingi zinakusanywa bila kuzingatia kanuni 10 muhimu za kukusanya takwimu.

“Ndiyo maana sasa tunataka kila mtu anayekusanya takwimu awe amesoma walau ngazi ya awali ya ukusanyaji takwimu,” alisema Kassala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles