32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yawapoza wanafunzi kuhusu mikopo

dkjoyce

Na GABRIEL MUSHI-

DODOMA

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, amesema Serikali haijafuta mkopo kwa mwanafunzi yeyote ambaye anaendelea na masomo ya elimu ya juu.

Pia ameviagiza vyuo vikuu vyote nchini ambavyo vimekwishatumiwa fedha kwa ajili ya wanafunzi wao na havijawawekea kwenye akaunti zao kuweka fedha hizo mara moja ili kuondoa adha wanayoipata kutokana na kucheleweshwa kwa malipo yao.

Profesa Ndalichako alitoa kauli hiyo jana mjini Dodoma wakati akitoa kauli ya Serikali kuhusu utoaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka 2016/17, baada ya Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM), kutaka kupatiwa mwongozo wa Serikali kuhusu malalamiko ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambao wamepanga kugoma.

Akifafanua kuhusu suala hilo, Profesa Ndalichako, alisema kwa mwaka huu 2016/17 Serikali imetenga Sh bilioni 483 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi 119,012 ambapo wanafunzi 93,295 ni wale wanaoendelea na masomo na wanafunzi 25,717 ni wale wa mwaka wa kwanza.

“Wanafunzi wote wanufaika wanaoendelea na masomo wataendelea kupatiwa mikopo kama ilivyokuwa katika mwaka uliopita wa masomo. Hivyo Serikali haijafuta mkopo kwa mwanafunzi yeyote ambaye anaendelea na masomo yake. Kwa wanafunzi ambao vyuo vyao vimewasilisha bodi ya mikopo taarifa za matokeo, bodi imekwishawatumia fedha zao.

“Hata hivyo, taratibu za kuwabaini wanafunzi wenye sifa stahiki zitaendelea na uchujaji utafanyika kwa kuwaondoa wale ambao watakuwa hawana sifa za kuendelea kupata mikopo,” alisema.

Alisema ucheleweshaji na ukamilishaji wa taarifa za matokeo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo, umeathiri kasi ya kutuma fedha kwenye vyuo mbalimbali.

Alisema baadhi ya vyuo vikuu ikiwamo UDSM tayari vimeshapatiwa fedha hizo tangu Oktoba 15 mwaka huu hivyo jambo la msingi wanafunzi wote kutakiwa kujaza fomu za usajili ili kuwekewa fedha hizo kwenye akaunti zao kwa sababu baadhi wamekuwa wakigoma kujaza fomu hizo kwa sababu zisizoeleweka.

“Aidha, naiagiza bodi ya mikopo kuhakikisha kuwa fedha zote za wanafunzi wanaoendelea na masomo zinatumwa vyuoni ifikapo Novemba 5, (leo) kwa sababu hadi kufikia Novemba 3, mwaka huu jumla ya Sh bilioni 71 zilikuwa zimekwishatumwa vyuoni kwa ajili ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wanafunzi wanaoendelea na masomo.

“Pia naagiza vyuo vikuu vyote ambavyo tayari vimekwishatumiwa fedha kwa ajili ya wanafunzi hao lakini mpaka sasa vyuo havijaweka fedha hizo kwenye akaunti za wanafunzi, waziweke mara moja ili kuondoa adha wanayoipata kutokana na kuchelewa kwa malipo yao.

Aidha, aliwataka wanafunzi wanaodanganya kugoma kusaini fomu za kupatiwa mikopo hiyo kutoendelea na mgomo huo kwani katu Serikali haitawawekea fedha hizo iwapo hawatasaini fomu hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles