22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mwaka 1 wa JPM muziki, filamu safi, sanaa nyingine hoi

RAIS Dk. John Magufuli
RAIS Dk. John Magufuli

NA CHRISTOPHER MSEKENA

WAKATI Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli leo akitimiza mwaka mmoja toka aapishwe kuwa kiongozi wa Taifa hili, sekta ya sanaa ipo njema, ipo vizuri na inaendelea kuwa na mvuto wa aina yake kila siku.

Haikuwahi kutokea kabla yake sanaa kuwekwa rasmi kwenye wizara. Awamu iliyopita, licha ya kuwa na rais anayependa masuala ya sanaa na burudani, hakufanikiwa kuifanya iwe rasmi kama ilivyo sasa.

Mara baada ya JPM kuingia madarakani, ndipo wasanii na kazi za sanaa zilipoanza kupata nafasi ya kutambulika kama sekta rasmi.

Kwa mara ya kwanza kukawa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, hivyo kuonyesha wazi kuwa sanaa ni ajira.

Ndani ya mwaka mmoja wa uongozi wa JPM, tunaiona sanaa ikizidi kustawi, hasa muziki na filamu vikipewa mashiko zaidi kuliko sanaa nyingine, hiyo imetokana na ukweli kwamba, nguvu kubwa imewekwa kwenye Bongo Fleva na Bongo Movie.

Sanaa ina wigo mpana, tunakosea tunapoishia kuitazama sanaa kupitia muziki na filamu pekee. Kuna sanaa nyingine zilizoajiri watu wengi hazipewi nafasi, jambo ambalo siyo haki kwa ustawi wa sanaa yetu.

Kuna sanaa ya uchoraji. Tunajua nchi yetu ina vijana wenye vipaji vya kuchora, wanaendesha maisha yao kupitia kazi hiyo, lakini hawana soko la uhakika la bidhaa zao.

Hii ni changamoto ambayo ndani ya mwaka mmoja wa uongozi wa JPM haijatazamwa.

Sanaa ya ufundi na zile za maonyesho. Hali ni tete, hali ni mbaya kwa wasanii wanaofanya kazi hizo, hakuna miundombinu rafiki itakayowafanya wasanii wanufaike na kile wanachokifanya.

Sanaa hizo zina idadi kubwa ya wasanii, hivyo Serikali ikizitazama kwa kiasi chake inaweza kupunguza uhaba wa ajira.

Tuache dhana ya kuyapima maendeleo ya sanaa kwa kuitazama Bongo Fleva na filamu. Huko kuko vizuri, wasanii wananufaika na kile wanachokifanya, ndiyo maana wanalipa kodi.

Najua misingi ya muziki huo haikujengwa mara moja, hivyo tunaweza kuanza kujenga misingi ya sanaa nyingine leo ili baada ya miaka kumi ijayo sanaa za ufundi, uchoraji na maonyesho zichangie kwa wingi kodi.

Muda bado tunao. Huku kwenye filamu na muziki tuachane nako na nguvu zote zielekezwe kwenye sanaa nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles