Na BENJAMIN MASESE,
SERIKALI imewaagiza Watalaamu wa Jiolojia Tanzania (GST) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufanya utafiti wa kina juu ya tetemeko la ardhi lilitokea mkoani Kagera Septemba 10 mwaka huu   na kuainisha maeneo mengine yenye viashiria katika mikoa mitano.
Pia imewazuia watalaamu wa jiolojia  waliopo Kagera kutokuwa wasemaji tukio hilo  isipokuwa tu Mtendaji Mkuu wa GST, Profesa Abdulkarim Mruma ambaye ni kiongozi wa timu ya wataalamu wote.
Agizo hilo lilitolewa juzi na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo  ambaye yupo mkoani Kagera kutembelea  eneo lilipotokea tetemeko   kujionea uharibifu na kukagua shughuli za utafiti unaoendelea sehemu mbalimbali mkoani humo.
Akizungumza na wataalamu wa GST na wale wa UDSM, Profesa Muhongo aliwaagiza kufanya utafiti wa kina wa miamba yenye viashiria vya tetemeko na kuanisha maeneo hayo kwa mfumo wa ramani mpya  kila mmoja aweze kuyafahamu.
Alisema ikiwa maeneo hayo yatafahamika, yatasaidia Serikali   na watalaamu wa GST kuchukua tahadhari na kutoa taarifa kwa wananchi jambo ambalo litaepisha vifo vya watu na uharibifu wa miundombinu.
Profesa Muhongo alibainisha mikoa ambayo itafanyiwa utafiti  utakaochukua muda mrefu kuwa ni Geita, Mwanza, Shinyanga, Tabora, Dodoma na   baadaye utafanyika  nchi nzima.
“Kwanza naomba mfanye utafiti wa kina wenye taarifa sahihi, mnapaswa kuanisha maeneo yenye miamba iliyo na viashiria vya milipuko ili iandaliwe ramani mpya ambayo itasadia serikali katika kuchukua hatua za awali.
“Pia hakikisheni mnatoa mafunzo ya awali kwa umma hususan kwenye maeneo yaliyoathiriwa zaidi na tetemeko   waelewe nini wanapaswa kufanya endapo tetemeko jingine litatokea jingine. Elimu hiyo ianze kutolewa Septemba 24, 2016  kuanzia saa 4 Asubuhi.
“Si kwamba elimu hiyo iishie Kagera hapana, ratiba ya mafunzo hayo kwa maeneo mengine iwafikie    na kuandaa vipeperushi vyenye maelezo ya kutosha kuhusu tetemeko la ardhi kwa ajili ya kuwasambazia wananchi.
“Jambo jingine naagiza ujengwe mnara maalum mrefu   palipotokea mlipuko yaani kwenye kitovu katika Kijiji cha Kigazi, Kata ya Minziro, kilomita 88 kutoka Bukoba mjini ili iwe kumbukumbu ya baadaye. Eneo hilo mliwekee alama, muandike siku na muda ambao tetemeko lilitokea,” alisema.
Profesa Muhongo alisema wananchi wa Kagera wameendelea kuwa na hofu kutokana na kuwapo   taarifa za wasomi na watalamu mbalimbali kutoa kauli zinazokinzana jambo ambalo linawazidishia wasiwasi wakazi wa mkoa huo na maeneo mengine ya nchi.