BAADHI ya wananchi wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma, wamegoma kujiandikisha wapate msaada wa fedha zinazotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAFIII) kusaidia kaya masikini,wakidai fedha hizo zinatolewa na Freemason.
Taarifa hiyo ilitolewa juzi na Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Kujenga Uwezo ya Tasaf, Fariji Michael, alipozungumza mbele ya makatibu tawala wa wilaya na mikoa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), waliotembelea shughuli za Tasaf zinazotekelezwa wilayani Chamwino. “Baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa kikwazo kwa watu wanaowaongoza kwa sababu wanawaambia fedha zinazotolewa na Tasaf zina uhusiano na Freemason.
“Baadhi ya waumini wanakubaliana na kauli hizo na wanaacha kujiandikisha ingawa ni masikini wanaohitaji msaada. “Kwa hiyo, naomba wananchi waelewe kwambafedha hizo siyo za Freemason bali zinatolewa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi masikini,”alisema Michael.
Awali, viongozi hao kutoka Zanzibar walitembelea miradi ya Tasaf katika Vijiji vya Chinangali II na Buigiri. Wakiwa katika vijiji hivyo, waliona jinsi shughuli zinazotekelezwa ikiwamo uhamishaji wa fedha, mpango wa ajira kwa walengwa na miradi yamiundombinu. Pia walikagua ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi ya Wasioona ya Buigiri, mradi ambao pia unatekelezwa na Tasaf.
Akizungumza kwa niaba ya makatibu hao, Mohammed Omary Hamad kutoka Wilaya ya Kaskazini A Unguja, alisema wamejifunza jinsi Tasaf inavyozisaidia kaya maskini na kuahidi yale waliojionea kuyapeleka Zanzibar. “Tasaf ni mfano wa kuigwa, tumeona jinsi wanavijiji vya Buigiri na Chinangali II wanavyoweza kujikwamua na umaskini na haya sasatutayapeleka kwetu Zanzibar,” alisema Hamad.
Awali, akisoma taarifa ya utekelezaji wa mpango huo, Kaimu Mratibu wa Tasaf, Mkoa wa Dodoma, Paul Ngussa, alisema tangu mpango huo uanze wilayani humo miaka kadhaa iliyopita, zimepokelewa zaidi ya Sh bilioni saba kwa ajili ya kusaidia kaya masikini. “Pamoja na hayo, tunakabiliwa na wingi wa kaya zinazohitaji msaada na pia hatuna ulinzi wa kutosha wakati wa kugawa fedha kwa walengwa,” alisema Ngussa.