30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Gazeti la Mseto lafungiwa

NapeNa Grace Shitundu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, ametangaza uamuzi wa kulifungia Gazeti la Mseto  kwa kipindi cha miaka mitatu, kutokana na kuchapisha habari zinazodaiwa kuwa ni za uongo na kutumia nyaraka mbalimbali za kugushi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Nape alisema uamuzi huo ulitolewa kwa Tangazo la Serikali Na. 242 lilitolewa Agosti 10, mwaka huu kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 Sura ya 229, kifungu 25 (1).

Alisema kifungu hicho kinampa mamlaka yeye kama waziri kuchukua uamuzi wa kufungia gazeti lolote ambalo mwenendo ni mbaya na linaandika na kuchapisha habari za uongo.

“Serikali kwa masikitiko makubwa imelazimika kilifungia Gazeti la Mseto kutokana na mwenendo wa uandishi wa kuandika na kuchapisha habari za uongo kwa nia ya kumchafua Rais wetu wa awamu ya tano, Dk. John Magufuli na viongozi wa Serikali,” alisema Nape.

Alisema hatua ya kulifungia gazeti hilo linalochapishwa kila wiki, imechukuliwa baada ya Msajili wa Magazeti kufanya jitihada za muda  mrefu tangu Septemba, 2012 hadi Agosti mwaka huu za kumtaka mhariri wa gazeti hilo kuacha kuandika  habari za upotoshaji, uchochezi na za uongo na zisizozingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari bila mafanikio.

Licha ya hali hiyo alisema Serikali imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayoainisha uhuru wa habari na mipaka ya habari kama vile tamko la Haki za Binaadamu la mwaka 1948, ambapo nchi yetu imeruhusu kwa kiwango kikubwa kwa kuweka ukomo wa uhuru huo kwa kukataza habari za uzushi uongo na uchochezi.

Gazeti la Mseto pia limezuiwa kuchapishwa katika njia nyingine yoyote ikiwemo mitandao (Online Publication) kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya  Kieletroniki na Posta Sura ya 306.

Kauli ya Kubenea

Akizungumza na MTANZANIA kuhusu uamuzi wa Serikali kulifungua gazeti hilo, Mmoja wa Wakurugenzi wa Kampuni ya Hali Halisi, Saed Kubenea, alisema kuwa kulikuwa na mkakati maalumu wa kulifungia gazeti hilo.

Alisema anashangazwa na hatua ya Waziri aliyodai kuwa tangu mwaka 2012 gazeti hili lilikuwa likionywa.

“Mseto lilisajiliwa mwaka 2006 na tangu wakati huo lilikuwa likichapisha habari za michezo hadi Aprili mwaka huu, lakini  barua tumeletea Jumatatu ambayo ilikuwa ni sikukuu ili tujieleza na majibu tuwasilishe Jumanne saa tatu asubuhi kwa Msajili wa Magazeti.

“Hakusikilizwa kutokana na hoja tuliyotakiwa kujibu ikiwemo ya kumchafua Rais Magufuli, huu ni mkakati kwa vyombo na waandishi wa habari nchini. Jumapili Bosi ya Wakurugenzi ya Hali Halisi itakutana na kuamua hatua za kuchukua na baada ya hapo tutaueleza umma,” alisema Kubenea ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo kupitia Chadema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles