WAOGELEAJI wawili watakaoiwakilisha Tanzania katika michezo ya Olimpiki inayotarajiwa kuanza Agosti 5-21 jijini Rio de Jeneiro, Brazil wanaendelea kujifua kwa ajili ya michezo hiyo.
Wawili hao wako kambi ya nje ya nchi ambapo Magdalena Ruth Alex amejichimbia Adelaide, Australia wakati Hilal Hemed Hilal yuko Dubai na wanatarajia kurudi nchini Julai 28.
Katibu wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Ramadhan Namkoveka, aliliambia MTANZANIA jana kuwa kutokana na maandalizi wanayoyafanya wana matumaini ya kupata medali.
“Tumewataka kurejea nchini kabla ya Julai 28 ili tuwaangalie tena, pia watakuja ili waweze kujiunga na wenzao kwa ajili ya safari kwa ujumla mazoezi yao yanaendelea vizuri na ni matumaini yetu kuwa safari hii tutaenda kuipeperusha vema bendera ya Tanzania,” alisema Namkoveka.
Olimpiki Rio mwaka huu itawakilishwa na wanamichezo 12 katika mchezo wa kuogelea, judo na riadha na timu inatarajiwa kusindikizwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, akiongozana na Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na Katibu wake, Filbery Bayi.