NA GRACE SHITUNDU, DAR ES SALAAM
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema tangu kuanza kwa mchakato wa kuandika Katiba mpya, uongozi wa visiwa hivyo ulishirikishwa kila hatua.
Akizungumza mjini Dodoma jana, Dk. Shein alisema pia kupatikana kwa Katiba hiyo inayopendekezwa kumesaidia kumaliza kero zote za Muungano zilizokuwapo.
“Matukio yote ambayo yalikuwa yakifanyika tangu kuanza kwa mchakato huu, kila hatua mpaka tulipofikia leo, Zanzibar imeshirikishwa kikamilifu.
“Pia mchakato huu umesaidia kumaliza kero za Muungano, sasa koti lililobana halitakuwapo tena na hizo zinazoitwa kero za Muungano hazitakuwapo,” alisema Dk. Shein.
Alisema Katiba hiyo itakuwa msingi wa kuimarisha umoja na mshikamano wa Tanzania.
“Waliosema haitowezekana, imewezekana, leo nimefurahi sana kwa hilo, nitaendelea kushirikiana na Rais Jakaya Kiketwe katika kuendeleza mshikamano wetu.
“Sisi wananchi wa Zanzibar, tumefurahishwa sana na upatikanaji wa Katiba hii, hasa siku Bunge lilipolipuka kwa furaha mara baada ya kupigwa kura na kupatikana kwa theluthi mbili, tulitamani kufika Dodoma lakini hakukuwa na njia kutokana na sisi wengine si wajumbe wa Bunge,” alisema.