MHESHIMIWA Mwenyekiti nashukuru kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia katika Bajeti hii ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti nimejaribu kufuatilia hotuba ya Mheshimiwa waziri sijaona sehemu ikizungumzia ni kwa namna gani walimu wataboreshewa maslahi yao, lakini pia Mheshimiwa Mwenyekiti kule kwenye jimbo langu bado watoto wanakaa chini, shule hazina vitabu, madawati wala walimu wa kutosheleza hali inayopelekea matokeo ya wanafunzi kwenye jimbo langu kuwa mabovu.
Mheshimiwa Mwenyekiti bado sijamuelewa Mheshimiwa Waziri kwa sababu katika bajeti hii haioneshi mpango wowote wa ujenzi wa nyumba za walimu na hata mabweni ya watoto wa kike pamoja na hayo Mheshimiwa Mwenyekiti naunga hoja mkono.
Hii ni aina ya uchangiaji hoja ya wanachama wengi wa Chama Cha Mapinduzi walio bungeni, hali hii ilinisababisha kutowaelewa wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi na kujiuliza ni kipi haswa huwa wanafikiria kuzungumza kabla hawajawasilisha hoja zao au michango yao kipindi cha bajeti.
Unawezaje kuunga mkono hoja wakati mchango wako zaidi ya asilimia tisini inaonesha huridhishwi na hoja iliyoko mezani? Yawezekana uchangiaji huu mara nyingi hutokana na shinikizo la vikao vya chama lakini nna imani kuwa ukiwa mwanadamu bado unahitaji kuwa na itikadi na misimamo isiyoyumbishwa na mtu yeyote na fikra mara nyingine unatakiwa utambue kuwa upo bungeni kuwakilisha wananchi wako na sio kuunga mkono hoja na hali halisi inaonesha kuwa huridhishwi na kile kinachoendelea.
Baada ya kupata shida sana na michango ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi hatimaye nikafanikiwa kusikia mchango ambao niweke wazi tu kuwa kwangu mimi ule ni moja kati ya michango bora niliyowahi kusikia kutoka kwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mchango wa Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini, Hussein Bashe.
Ndugu Bashe aliwaambia ndugu zake wa CCM kile walichopaswa kukisikia na sio walichotamani kukisikia, nchi ya Tanzania ni nchi ya wananchi na si nchi ya chama japo wananchi wana vyama ila linapokuja suala la maslahi ya Taifa basi Taifa lije kwanza na vyama baadaye, najua chama tawala huwa hakipendezwi na watu ambao hukikosoa chama hicho na kuwaona wale kama wasaliti, lakini ama kwa hakika ukosoaji unajenga zaidi kuliko sifa lakini tu pale ambapo anayeshauriwa au kukosolewa atakubali kukosolewa japo kiukweli maneno ya ukosoaji huuma kuliko sifa zisizo na tija.
Yawezekana kwa kuwa Bunge halipo live mnaweza mkawa hamjasikia wala kuona ni maneno yapi mliambiwa na MwanaCCM huyo, kwa manufaa ya chama chenu ningependa ninukuu nini alichowaambia, Bashe, alisema hivi “Mwalimu Nyerere aliwahi kuongea na wafanyakazi mwaka 1975 alisema, akiwaambia wafanyakazi Utii ukizidi unakuwa uoga na siku zote uoga huzaa unafIki na unafiki huzaa kujipendekeza na hivyo kuzaa mauti, Mwalimu aliendelea kuwaambia wafanyakazi kama nyie watumishi wa umma kwa wingi wenu mmeshindwa kupiga kura ya kuwaondoa viongozi dhalimu ni bora mfe na mimi nasema sisi kama CM kwa wingi wetu tunashindwa kuishauri Serikali hatuna sababu ya kubaki madarakani nayasema haya kwa moyo mweupe nikiwa mwanachama wa chama chetu.
Kwa nini nasema hivyo, hili ni jukumu letu Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kutafuta suluhisho la migogoro ya wakulima na wafugaji na hili sio jukumu la waziri peke yake ni jukumu letu sote kama chama na kama Serikali, Mheshimiwa Mwenyekiti hili sio jukumu la Magembe hili ni jukumu la Waziri wa TAMISEMI, hili ni jukumu la Waziri wa Kilimo, hili ni jukumu la Waziri wa Ardhi, hili ni jukumu la Waziri wa Sheria ili tuweze kutengeneza mazingira bora kwa jili ya wananchi wetu”.
Hivi umeshawahii kujiuliza siku wabunge wa chama tawala wakiamua kusimama kidete na kuibana Serikali kwenye kuwajibika kuna suala litashindikana? Kwa bahati mbaya ni kuwa hapa kwetu ni kama kuna mgawanyo wa majukumu kwa wabunge, wabunge wa vyama vya upinzani kazi yao kuu imekuwa ni kukosoa na iko hivyo sehemu nyingi ulimwenguni huku upande wa pili chama tawala chenyewe kimejikita kwenye kusifia utandaji wa Serikali bila kujali kuwa sifa zile zina tija au la.
Kwa upinzani wanapokosoa wao huwa wako sawa kwa kuwa kazi yao kubwa ni kuwaonesha watawala mahali wasipoweza kuona, ajenda ya Katiba ilikuwa ni ajenda ya upinzani, ajenda ya elimu bure ilikuwa ni ajenda ya upinzani japo hapo awali watawala walidai kuwa elimu bure haiwezekani ajenda ya ufisadi pia hapo awali ilishikiliwa na wapinzani na kwa bahati nzuri japo watawala hawakuwahi kukubali mawazo hayo lakini suala la Katiba walilichukua, suala la elimu bure watawala wakaona linafaa wakalichukua, suala la ufisadi ni kama unavyosikia hivi sasa kila kukicha yanapatikana majipu na mpaka Mheshimiwa Rais aliahidi kipindi cha kampeni kuwa ataandaa mahakama ya mafisadi huu ni baadhi ya ushauri au mawazo yaliyotolewa na wapinzani sasa tujiulize ni sifa zipi ziliwahi kuifanya Serikali ifanye kazi?
Bashe yuko sawa kabisa, haiwezekani mkae madarakani miaka yote huku kundi la wafugaji na wakulima wakiendelea kuuana huku Serikali ikishuhudia? Mnapata wapi ujasiri wa kuendelea kuongoza kwenye taifa ambalo wananchi wanatoana roho kila kukicha?
Leo anasimama mbunge anachangia bajeti akidai anasikia uchungu na anatamani kulia kwa kuwa kuna watu wanadai Bunge live nyie ndio kwanza mnakaza mikono kumgongea meza kama vile alilozungumza ni hoja itakayofanya Taifa lisonge mbele, anasimama Mbunge mwingine bila hata ya kuwa na uoga anaona achangie kuwa tumuweke msanii pale kwenye mnara wa Posta, wapo waliosikitika kutokana na kauli hizi lakini haya ni matokeo kwani vituko bungeni havikuanza leo, mtu anakaa bungeni kwa vipindi vitatu lakini kazi yake kubwa ni kulalamika juu ya bajeti lakini wakati anahitimisha lazima aunge mkono hoja hivi ni vioja.
Wabunge wa CCM iambieni Serikali mambo inayopaswa kuyasikia sio inayotaka kuyasikia, ushauri wa Bashe kwa chama chake ni ushujaa ila kwa wenye fikra finyu ni usaliti.