MBUNGE wa Tarime Mjini, Esther Matiko (Chadema) amesema kumekuwa na mkakati au maelekezo kwa menejementi ya vyuo vikuu kuwanyanyasa wanafunzi ambao hawapendezwi kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amesema katika mkakati huo, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kinaongoza.
Matiko alikuwa akimuuliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitaka kujua kama ni kweli kuna maelezo na Serikali inazieleza nini menejimenti za vyuo.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu ni dhahiri kwamba wanafunzi hawatakiwi kufanya siasa vyuoni lakini kumekuwapo na ama mkakati au maelekezo kwa menejimenti ya vyuo kuwawanyanyasa wanafunzi ambao hawapendezwi na siasa za CCM.
“Je, ni kweli kuna hayo maelekezo na Serikali inazieleza nini menejementi hiyo ya vyuo na kuingilia uongozi wa serikali za wanafunzi,”alihoji Matiko.
Akijibu swali hilo Majaliwa alisema,”Kwanza nikanushe kwamba kuna maelekezo. Pili hakuna unyanyasaji wowote unaofanyika katika vyuo.”
Majaliwa alisema Watanzania wote wanao uhuru wa kujiunga na vyama wanavyovitaka lakini kila eneo limewekwa utaratibu wake.
“Lakini liko zuio la mtumishi kuendelesha siasa akiwa kazini na wanafunzi hivyo hivyo hawaruhusiwi kufanya siasa wakati wa masomo.
“Ninawasihi viongozi wa vyama vya siasa kwamba hili si msimamo wa serikali bali ni mapenzi ya watu wengine. Tanzania ni yetu sote kila mmoja anao uhuru wa kujiunga na chama anachokitaka,”alisema Majaliwa.