28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

Falsafa ya binadamu na Watanzania

NI wiki mbili mfululizo sasa kumekuwa na masuala mbalimbali yaliyokuwa yanaripotiwa kwenye vyombo vya habari na kujadiliwa katika mitandao ya kijamii. Kilichonishangaza zaidi ni baada ya watu kadhaa waliponitumia ujumbe, kunipigia simu wakiniuliza maswali kuhusu baadhi ya  mambo hayo.

Kwa mfano kuna mtu aliniuliza “mbona  mamlaka ya polisi ilitakiwa kupeleka  mkataba kwenye kamati ya Bunge na haikutimiza na inaelekea kamati imegwaya kufanya chochote? Nikamjibu wamewapa muda mwingine, yule mtu akaniambia mbona Mh. Ester Bulaya alikamatwa na kuletwa kwa ndege kutoka Mwanza aliposhindwa kuitikia wito?

Mwingine akaniuliza  kuna mtu huko Arusha anashtakiwa kwa kosa la kumwita Mh.  bwege lakini kuna mtu aliyewaita  watu wapumbavu na malofa mbona hakuchukuliwa hatua?

Mwingine akaniuliza eti yule wakili wa Takukuru katika kesi ya aliyekuwa Meneja wa Tanesco baada ya hukumu ya kuachiwa meneja huyo na wenzake, yeye amelalamika  kuwa kuna rushwa katika suala hili, Je, kama  ameona rushwa kwanini asichukue hatua kwa vile yeye  kazi yake ni kushughulikia rushwa?

Mimi nilipata maswali mengi sana maana maswali haya yameletwa na watu tofauti kutoka sehemu tofauti na haiba tofauti. Kwanini wananiuliza mimi? Wanadhani kuwa nina majibu ya kila swali? Na kama wanadhani hivyo ni kwanini? Katika kutafakari nilikumbuka  somo la falsafa na wanafalsafa mbalimbali  niliowahi kuwasoma. Somo hili lilikuwa na maswali na mengine hayakuwa na majibu na katika kujaribu kujibu huweza kuwa na maswali zaidi. Kwa mfano  jibu la swali kuwa falsafa ni nini limejibiwa kwa njia nyingi sana.

Clare Carlisle yeye anasema  falsafa ni kujaribu kuelewa mazingira yote yanayotuzunguka. Tumejikuta katika hii dunia bila kuamua au kupanga hivyo kuna haja ya kujaribu kuielewa kwa kufanya tafsiri  na maana katika  dunia hii. Kwa hiyo kwa upande wake ni kupata majibu ya uelewa wa hali tunayojikuta kwayo.  Naye John Dunn  anasema kuwa falsafa ni uchunguzi wa nini kilicho kweli na jinsi watu wanavyopaswa kuishi. Huyu yeye anaona ukweli wa maisha  na jinsi watu wanavyopaswa kuishi  imekuwa na hali ya kuwa na umbali badala au ya  kuwiana  au kukaribiana.

Wapo wengine wengi ambao wao hawakujaribu kujibu swali la falsafa ni nini bali walitoa kanuni za maisha kama vile Plato aliyesema mpaka wanafalsafa watakapotawala  kama wafalme na kuwaongoza watu kwa nia njema, yaani  mamlaka  ya kisiasa na falsafa vitakavyowiana au vitakavyoongea lugha moja   maovu hayataisha katika miji na hata kwa wanadamu.  Aristotle yeye aliweka kanuni ya kutenda  mema na si kuwa mwema. Haina maana alisema, ya kuwa mwema wakati wema wako hauhusiani na kuwatendea watu wengine mema.

Haya mawazo yalijitokeza pale niliposaidiwa na baadhi ya watu kutafakari maswali niliyoulizwa hapo juu. Hayo maswali si magumu ukiyaangalia juu juu. Ila ukiyaangalia kwa undani ni maswali mazito yanayohusu kanuni katika maisha.  Katika wale tuliojaribu kutafakari kuna aliyesema tuzingatie falsafa ya Binaadamu na Watu. Neno binaadamu linasemekana kubeba itikadi. Na inategemea tuko katika itikadi gani. Kwa sasa nchi yetu imehama kutoka katika itikadi ya ujamaa na ipo katika itikadi ya ubepari. Namkumbuka sana Mwalimu Nyerere  katika kupambanisha itikadi hizi mbili na mawazo yake yalieleweka sana kwenye mazungumzo baada ya habari wakati huo yakisomwa Redio Tanzania. Tulikuwa tunasikia  ‘Ubepari ni unyama’ na’ Ujamaa ni utu, utu , utuuuu’. Katika tafakari yetu mmoja wetu alieleza kuwa katika  mfumo wa ubepari  binadamu ni yule mwenye mtaji  yaani fedha, mali, hadhi au wadhifa.

Mwalimu Nyerere  alikuwa anasisitiza haki na utu. Na pia  kwenye Katiba yetu kila mtu ni sawa mbele ya sheria.  Katika hali ya kuwa  binaadamu kwenye itikadi ya ubepari ni wenye mitaji  au wadhifa ndio binadamu na wasio navyo wao si binadamu, pengine ndio watu. Ndio maana  katika kumjibu yule ndugu aliyetaka kujua habari za bwege na malofa au habari za Mbunge aliyekodiwa ndege na Mkuu wa Jeshi la Polisi  ni kuwa mmoja ni binadamu na mwingine haonekani hivyo kwa mujibu wa itikadi. Dola zipo kuwasaidia binaadamu na ukimkosea binadamu utachukuliwa hatua na wewe  usiye binadamu ka mujibu wa itikadi hiyo ukikosewa  kama mfumo wa sheria ukikusaidia basi una bahati.

Katika nchi hii ambayo inasemekana ni ya Kidemokrasia inayoongozwa na Katiba kuna mambo ambayo yanawashangaza watu walio na nafasi ya kufikiri na kuhoji. Kila mtu anapenda atendewe vizuri na hakuna mtu yeyote anayependa kusemewa maneno maovu au machafu. Mtu  akinenewa  vibaya yule aliyefanya hivyo  ni sawa kabisa achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria. Kama tumeweka sheria na kanuni lazima zifuatwe, ni sawa kabisa asiyefuata ashughulikiwe kwa mujibu  wa sheria au kanuni.

Inakuwa ni tatizo pale panapokuwa na hali ya kiubaguzi katika  kuchukau hatua. Watu wanashangaa pale wanapoona kuwa iwapo ipo sheria dhidi ya suala fulani iweje katika  kushughulikia hali kama hiyo akikosea huyu anashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na akikosea huyu sheria inakuwa kama haioni. Au ndio yale katika kitabu cha ‘Amimal Farm’ kuwa wanyama wote ni sawa ila wengine ni sawa zaidi?

Tumepata Serikali  ya Awamu  ya Tano ambayo nilizungumza wiki iliyopita kuwa Rais anayeiongoza  Serikali hii amejipatia sifa kubwa sana hadi sasa na si nchini tu hata nje ya nchi. Ninamsikia mara nyingi Rais akisema ana uchungu na Watanzania hasa wa hali ya chini. Iwapo hivi ndivyo basi kwa mamlaka aliyonayo Rais ya kiutendaji na ya kiushauri aweze kutoa miongozo kwanza ya kubadili sheria hizo kandamizi na kuna mmoja aliyeniambia jibu ni Katiba Mpya.

Lakini pia atoe ushauri hasa kwa mamlaka za utekelezaji kuweza kutekeleza sheria kwa haki na usawa. Isionekane kuwa  wapo walio juu ya sheria na wengine wako ndani ya sheria na wengine chini ya sheria. Pia tungependa kuona udhati wa Serikali yetu hii. Mimi hadi sasa sielewi suala la Bunge na vyombo vya habari.

Mwanzo nilisikia kuwa Serikali haina fedha ya kugharimia matangazo ya moja kwa moja kwa Bunge.  Baadaye nikasikia wenye uwezo wa kugharimia  wakijitokeza  kuwa wapo tayari kusaidia, kama ambavyo tunaona wengi wanaojitolea kugharimia madawati na majengo ya shule. Baadaye tunasikia Bunge sasa litakuwa na studio yake ambayo ndio itakuwa inarekodi na vyombo vya habari vipate kutoka kwenye studio ya  Bunge.

Sasa kuanzisha hii studio kwenyewe hakuna gharama? Na kama sio, tungependa kujua kwa kufanya hivyo tumeokoa kiasi gani cha fedha, dhidi ya  kile ambacho kilikuwa kinatumiwa na televisheni ya Taifa kurusha Bunge  moja kwa moja. Tunapenda Serikali yetu iwe na uwazi na isituogope wananchi wake kiasi cha kutupa  taarifa zinazokanganya.

Wale walioniuliza maswali nasikitika kuwa sikuweza kuyajibu ila yamenisaidia kupata maswali mengi zaidi na kuangalia hali ya nchi yetu kwa upana zaidi ya kiasi  cha mbunge kubebwa mkuku kutoka Mwanza kuja Dar, kwa kukiuka amri na kuachiwa baada ya muda mfupi na gharama kutumika kumrudisha huko Mwanza. Pia mtu aliyetamka maneno mabaya na kuchukuliwa hatua na mwingine kutochukuliwa hatua na  hata malalamiko ya mtendaji wa TAKUKURU dhidi ya mahakama.

Bado jibu la maswali yetu mengi litapatikana iwapo tutawatafakari zaidi wale wanafalasafa na hasa kwenye suala la kuangalia tunaendesha vipi maisha yetu na muongozo wetu ni Katiba tuitakayo.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles