30.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mjadala Mahakama ya Kadhi wazidi kutikisa Bunge

Bunge
Bunge

NA WAANDISHI WETU, DODOMA

MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Abdallah Mtutura (CCM), amewataka wajumbe wa Bunge hilo ambao ni Waislamu, washirikiane kuipinga Rasimu ya Katiba kama Mahakama ya Kadhi haitaruhusiwa katika Katiba mpya.

Akichangia sura za nne na 10 za Rasimu ya Katiba bungeni mjini hapa juzi, Mtutura alisema kitendo cha baadhi ya wajumbe kuonyesha dalili za kuipinga mahakama hiyo, hakiwezi kukubalika kwa kuwa ni muhimu kwa Waislamu wanaoiamini.

“Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti, katika nchi yetu tunayo matabaka matatu ambayo ni ya Waislamu, Wakristo na kuna tabaka jingine ambalo wao hawaamini chochote.

“Ukiangalia mgawanyo wa idadi ya watu, utakuta matabaka haya mawili, karibu yanawiana, lakini katika ujenzi wa Katiba hii tumepitisha vifungu mbalimbali tena vya matabaka madogo.

“Lakini, leo tabaka hili la Waislamu ambalo linachukua karibu nusu ya ‘population’ ya nchi hii, tunalipuuza ingawa katika imani yetu kuna baadhi ya mambo ambayo lazima tuyafanye ndipo tuuone ufalme wa Mwenyezi Mungu,” alisema Mtutura.

Kwa mujibu wa Mtutura ambaye pia ni Mbunge wa Tunduru Kusini, Waislamu wana baadhi ya mambo ambayo lazima wayafanye kwa kuwa yanakwenda sawa na ibada zinazoendeshwa katika baadhi ya madhehebu.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni ndoa, mirathi na talaka ambayo alisema lazima yatambuliwe kikatiba.

“Haya mambo ni ibada kwetu ndiyo maana tunasema mama wewe Katiba tunaomba utambue mambo haya, lakini anatokea kaka ambaye hata jambo hili halimhusu, anasema usimpe, tunawashangaa.

“Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti, hapa nchini tunayo Mahakama ya Biashara ambayo haiwezi kupingwa na mkulima kwa sababu haimuhusu na tunayo kada ya wavuvi ambayo haiwezi kupingwa na wakulima kwa sababu haiwahusu.

“Hivi tunataka kujenga ‘society’ ya namna gani, narudia kusema Uganda inayo Mahakama ya Kadhi, Kenya wanayo Mahakama ya Kadhi, Zanzibar wanayo Mahakama ya Kadhi na kote huko hatujawahi kusikia zimetokea vurugu kwa sababu ya Mahakama ya Kadhi.

“Mlisema hatuwezi kuwapa Mahakama ya Kadhi kwa sababu hatuna fedha, Waislamu tukasema tupeni tutaiendesha wenyewe, lakini bado mnatusumbua, hivi mnachotaka Waislamu wafanye nini?

“Ninachoweza kuwaambia ni kwamba Waislamu tuko tayari kwa umoja wetu na itafikia mahala tutasema kama Mahakama ya Kadhi haitapatikana, Waislam hatutaipitisha Katiba.

“Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti, katika hili Waislamu tutakuwa na sauti moja na hatutabadilika,” alisema.

MAKAMU MWENYEKITI AONYA

Maneno hayo yalionekana kutomfurahisha Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu Hassan na kuwataka wajumbe wanapojadili, wasitumie maneno yanayoamsha hisia za wananchi.

CHEYO AINGILIA KATI

Mjumbe wa Bunge hilo ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), alipingana na kauli zilizotolewa na Mtutura kwa kile alichosema kuwa zinalenga kuwagawa wananchi.

Kutokana na hali hiyo, alipendekeza Kamati ya Uongozi ikutane ili kuangalia namna ya kutatua suala hilo.

SITTA ATAHADHARISHA

Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, alisema suala la Mahakama ya Kadhi lipo kwa Waziri Mkuu ambaye analifanyia kazi.

Pamoja na hayo, alikanusha kauli za baadhi ya wajumbe wanaosema suala la mahakama hiyo lipo katika Katiba za Uganda na Zanzibar.

Kwa mujibu wa Sitta, Mahakama ya Kadhi nchini Uganda na Zanzibar inatambuliwa kisheria na haipo katika Katiba.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wajumbe wasijadili mambo ambayo hayakupitishwa wakati wa vikao vya kamati kwa kuwa kuyajadili ni kutaka kuvuruga mjadala wa Bunge.

Katika hatua nyingine, jana Mtutura aliomba radhi bungeni kwa kutumia maneno makali wakati akiwasilisha hoja yake hiyo juzi.

CCM YAWEKA MKAKATI

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimekutana mwanzoni mwa wiki mjini Dodoma, kwa kile kinachoaminika kuwa pamoja na mambo mengine kikao hicho kililenga kuwanyamazisha wajumbe wao wasijadili masuala yanayohusu Mahakama ya Kadhi.

“Kikao hicho kiliitishwa baada ya kuonekana kuwa baadhi ya wajumbe hususani Waislamu wanajadili zaidi udini kwa kupigia debe Mahakama ya Kadhi iingizwe kwenye rasimu ili kesi zinazowahusu Waislamu zikiwamo za ndoa, mirathi, talaka na wakfu zisikilizwe na watu wanaotambua sheria za Kiislamu,” kilisema chanzo chetu.

Kikao hicho kilifanyika chini ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.

“Yaani tumekatazwa kuzungumzia suala la Mahakama ya Kadhi ili kuepuka chuki za kidini, hili jambo limeonekana litaleta mpasuko mkubwa na kutugawa kwa itikadi zetu za kidini, tumeambiwa tuache kamati inayolishughulikia ifanye kazi yake, ila inavyoonekana halitaingizwa kwenye rasimu kama wajumbe wanavyotaka,” kilisema chanzo hicho.

Taarifa hii imeandaliwa na Maregesi Paul na Rachel Mrisho, Dodoma.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles