23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa moto tena

Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

NA WAANDISHI WETU

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umewasha moto tena.

Moto huo, unatoka na Ukawa kumwomba Rais Jakaya Kikwete kusitisha mara moja vikao vya Bunge Maalumu la Katiba vinavyoendelea mjini Dodoma kwa nia ya kuepusha upotevu wa fedha za walipakodi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, wakati wa kutoa tamko la umoja huo, Mwenyekiti wa Maridhiano, James Mbatia, alisema baada ya majadiliano kati ya Rais Kikwete na Kituo cha Demokrasia (TCD), walibaini mchakato wa Katiba unaoendelea usingefika mbali.

Majadiliano kati ya Rais Kikwete na TCD, yalifanyika Agosti 31 na Septemba 8, mwaka huu.

“Baada ya kufanyika kwa majadiliano, tulibaini mchakato wa Katiba hautaweza kufikia hatua ya mwisho kwa wakati huu, ni vyema Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta akashauriana na Kamati ya Uongozi ili kuahirisha Bunge hadi wakati mwafaka utakapopatikana.

“Kuendelea na vikao hadi Oktoba 4, mwaka huu, ni kuhalalisha ufisadi wa fedha za walipa kodi, sisi Ukawa tunapaza sauti zetu na kusema hapana! Hapana! Haikubaliki,” alisema Mbatia.

Alisema baada ya kujadili hoja hizo, waliona upo umuhimu wa kuahirisha mchakato wa Katiba ili kupisha maandalizi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya mabadiliko ya 15 ya Katiba ya sasa na kutoa nafasi ya mazungumzo yanayoendelea kupata maridhiano ya kisiasa.

Mbatia alisema mchakato wa Katiba utaendelea baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa kutumia rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na sheria iweke bayana kipindi cha mpito na kuhakikisha mchakato huo unakamilishwa baada ya kupatikana  maridhiano ya kisiasa.

Jambo jingine ilikuwa ni kuvitaka vyama vya siasa kuandaa mapendekezo ya mambo machache na ya msingi yatakayokubalika na wadau wote ndipo yapelekwe serikalini kwa ajili ya kuandaa muswada wa mabadiliko ya 15 ya Katiba ya sasa.

Alitaja mapendekezo hayo kuwa ni kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi inayokubalika na kuaminiwa na wananchi pamoja na majukumu mengine, lakini jukumu kuu liwe kuratibu na kusimamia uchaguzi ulio huru na wa haki.

Alisema pendekezo jingine ni kuweka mgombea huru katika uchaguzi, rais achaguliwe kwa asilimia 50+1 ya kura, matokeo ya urais yahojiwe mahakamani na kuweka ibara za kipindi cha mpito cha kuhakikisha kuwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba unakamilika baada ya kupatikana kwa maridhiano ya kisiasa.

Mbatia alisema katika majadiliano yao, walibaini muda wa ratiba iliyotolewa ya mchakato huo ulionyesha wazi kwamba hautoshi kukamilisha mchakato mzima.

Ilibainika muda uliobaki kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015 na maandalizi ya kisheria, kiutendaji na kimiundombinu yanahitajika ili kuwa na uchaguzi wa haki, yatakayosimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi.

Alisema jambo jingine lililojitokeza ilikuwa ni taifa kukabiliwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ikiwamo mchakato wa kuandikisha upya daftari la kudumu la wapigakura kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015 kwa kutumia mfumo wa kielektroniki wa Biometric (BVR).

Kuhusu namna ambavyo wananchi wameupokea mchakato huo wa Katiba, Mbatia alisema kuwa kumekuwapo na misimamo mikali katika jamii ya Watanzania.

Alisema walikutana pia kutafuta mwafaka wa kisiasa kuhusu mchakato wa Katiba na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Aliongeza kuwa mambo mengine waliyotafakari kwa pamoja ilikuwa ni kuhusu msingi wa kupatikana kwa Katiba kwa njia ya maridhiano yatakayoliwezesha taifa kuwa na maelewano, maendeleo endelevu, umoja na amani.

Ajenda nyingine ni kujadili kuhusu kipindi kigumu inachopitia ambacho kama hatua madhubuti hazitachukuliwa, Tanzania na watu wake wanaweza kuingia katika machafuko na vurugu ambayo si kuchafua taswira ya nchi, bali italiacha taifa lote likiwa limegawanyika katika makundi yanayohasimiana.

Alisema walibaini kuendelea kwa mchakato wa utoaji wa vitambulisho vya taifa ambao hata hivyo unasuasua.

Mazungumzo hayo yalisainiwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Phillip Mangula, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa Maridhiano, Mbatia.

DK. Slaa

Naye Katibu Mkuu wa Chadema Willibrod Slaa alishangaa kuona Rais Kikwete anakiri hadharani kuwa Katiba mpya haitapatikana mwaka huu.

Dk. Slaa alisema anasikitishwa na Rais Kikwete kushindwa kusitisha Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea mjini Dodoma.

“Kama Bunge hilo litaendelea katika siku 19 litakuwa limepoteza Sh bilioni 3 ambazo ni sawa na kujenga vyumba vya madarasa 195,” alisema.

MBOWE

Naye Mbowe amesema chama chake kimechoka na ubatili unaoendelea ndani ya Bunge Maalumu la Katiba, na kwamba kitaandamana endapo Bunge hilo halitaahirishwa.

Akitoa msimamo wa chama hicho wakati wa ufunguzi wa uchaguzi wa Baraza la Vijana Taifa (BAVICHA) jijini Dar es Salaam jana, Mbowe alisema hawatakubali vikao vya Bunge kuendelea hadi Oktoba 4.

Alisema haiwezekani rais ashindwe kuvunja Bunge hilo kwa kuogopa sheria, huku mabilioni ya fedha za Watanzania yakiendelea kutumika.

“Eti rais hana sheria ya kuvunja Katiba hivyo waendelee na ufujaji wa fedha za umma. Huu si msimamo wa Chadema ni wa Ukawa…tumevumilia kiasi cha kutosha, wametuchezea sasa tutaonana barabarani,”alisema.

Alisema kwa wajumbe ambao wanaendelea kujitajirisha kwa mabilioni ya Watanzania ipo siku watayajibu.

“Hawa ambao wanaendelea na vikao na kujitajirisha hizi fedha haramu ipo siku watayajibu haya. Rais anashindwaje kusimamisha uamuzi batili eti kwa vile tu anaogopa kuvunja sheria sasa hatuwezi kuwa sehemu ya ubatili… tumechoka na utapeli wa kisiasa,”alisema Mbowe.

Alisema siku ya mkutano mkuu wa chama hicho pamoja na vyama vingine watatoa siku ya kufanya maandamano endapo Bunge hilo halitaahirishwa.

SITTA
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, ameutangazia umma kuwa Katiba mpya inayopendekezwa na wananchi itapatikana kabla ya Oktoba 10.

Kauli hiyo inakinzana na uamuzi uliofikiwa na Rais Kikwete na viongozi wakuu wa vyama vya siasa vinavyounda TCD, ambao kwa pamoja walikubaliana kuwa kutokana na mazingira yalivyo mchakato huo hauwezi kutoa Katiba mpya.

Rais na viongozi hao walikubaliana kuwa Bunge Maalumu la Katiba liendelee na mchakato wake hadi Oktoba 4, licha ya kwamba mchakato huo hautaweza kutoa Katiba itakayotumika katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Akizungumza jana wakati akisoma ratiba ya shughuli za Bunge, Sitta alisema: “Nafurahi kuwaambia kwamba juzi katika kikao cha Kamati ya Uongozi tumedhihirisha kwamba tunakwenda vizuri.

“Kamati ya Uandishi ambayo imekuwa ikitazama mambo yanavyokwenda na mjadala ulivyoanza jana (juzi), imejipanga kutupa rasimu ya mwisho tarehe 21, mwezi huu.

”Ni dhahiri kabisa kwamba lengo tulilopewa na taifa la kutoa Katiba inayopendekezwa tutalimudu ndani ya wakati.”

Alisema ratiba ya Bunge hilo inaendelea kama ilivyopangwa, siku 60 za Bunge hilo ambazo ni nyongeza ya siku zilizotolewa na rais.

“Kwa mujibu wa sheria, usipohesabu siku za Jumamosi na Jumapili na sikukuu, siku 60 zinaishia Oktoba 4, mwaka huu, tunaangalia upigaji kura wa wenzetu ambao wako nje ya Bunge kwa sababu mbalimbali,” alisema.

Sitta alieleza kuwa mpango huo wa kupigia kura rasimu hautawahusu waliosusia Bunge.

“Wapo wengine wana sababu za kutokuwapo, kama vile hospitalini na kadhalika, kanuni zitatuongoza kwenye hilo, kwahiyo itakapofika wakati wa kupiga kura tutatoa maelezo ya utaratibu upi utatumika kuweza kuwapata kwa sababu akidi inatuhusu sisi sote ambao tuliteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa wajumbe wa Bunge hili,” alisema.

Aliwahakikishia wajumbe wa Bunge hilo ambao wapo nje kwa sababu yoyote na wanaokwenda kuhiji, kuwa wataipigia kura rasimu hiyo zoezi linalotarajiwa kuanza Septemba 26.

Aliwataka wajumbe wanaokwenda hijja kupeleka taarifa zao kwa Katibu wa Bunge ambazo zitaeleza wanakwenda kuhiji wapi pamoja na kuwataja mawakala wanaowashughulikia kwa safari hiyo.

Taarifa hii imeandaliwa na Rachel Mrisho (Dodoma), Elizabeth Hombo na Shabani Matutu (Dar)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles