29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

Washindi tamasha la utamaduni wa Mtanzania wakabidhiwa zawadi zao

Na Clara Matimo, Mwanza

Washindi wa michezo mbalimbali iliyofanyika kwenye Tamasha la Utamaduni wa Mtanzania , Mila na Desturi zetu lililofanyika Septemba 7 na 8, mwaka huu katika uwanja wa Msalaba Mwekundu(ngomeni) Kata ya Kisesa, Wilaya ya Magu mkoani Mwanza wamekabidhiwa zawadi zao ambazo ni ngao na medali.

Mshindi wa Mchezo wa Bao, Nestory Shishi(kulia), kutoka Mkoa wa Mwanza akipokea zawadi yake ya ngao kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, aliyemwakilisha Chifu Mkuu wa Tanzania Hangaya.

Jaji Mkuu wa mashindano hayo, Jackson Kadutu, alisema michezo iliyoshindaniwa katika tamasha hilo ni ngoma za asili, kupigana fimbo, bao, kupekecha moto, kurusha mkuki, kutwanga mahindi na kusaga kwenye jiwe.

Kwa mujibu wa Kadutu Mkoa wa Shinyanga umeongoza kwa kutoa washindi watatu katika mchezo wa kusaga kwenye jiwe, kutwanga mahindi na kupigana fimbo ukifuatiwa na mkoa wa Mwanza ambao umeongoza kwa ngoma za asili  na mchezo wa bao, Arusha imetoa mshindi wa kupekecha moto na Singida kurusha mkuki.

“Kikundi cha Bacesilia Bujora kutoka Wilaya ya Magu  ndicho kimeongoza kwa ngoma za asili kimepata alama 82.2, kilishindana na vikundi 12, kupigana fimbo washiriki walikuwa wawili, Chuga Hoyanga ndiye aliyeibuka mshindi, kupekecha moto Chifu Isaka Lekisongo ndiye aliyenyakua medali.

 “Kurusha mkuki Salum Senge, bao Nestory Shishi, kusaga kwenye jiwe aliyeibuka kidedea ni Felister Kashinje na kutwanga mahindi kwenye kinu wameshinda washiriki  watatu ambao ni Felister Kashinje, Felister Raphael na Maria Jimwaga,”alisema Kadutu.

Akikabidhi zawadi hizo kwa niaba ya Chifu Mkuu wa Tanzania, Hangaya, ambaye ni Rais  Samia Suluhu Hassan, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, alisema kila mwaka mwezi wa tisa tamasha la utamaduni litafanyika mkoani hapo ili kuenzi tukio la kusimikwa uchifu kwa rais lililofanywa na Umoja wa Machifu Tanzania (UMT) Septamba nane mwaka huu.

“Nawapongeza sana UMT kwa kuandaa tamasha hili zuri ambalo linatukumbusha mila, desturi na tamaduni zetu watanzania pamoja na michezo ya jadi, tujipange kama mkoa ili tamasha la mwaka kesho liendane na maonesho, mauzo ya bidhaa  za utamaduni kutoka makabila  mbalimbali watalii wakija wapate full package ya utamaduni.

“Nataka tamasha lijalo liwe na vionjo vingi, tuanze maandalizi mapema tunataka Mwanza iwe kilele cha kuitangaza nchi yetu kwa utamaduni inawezekana, kinachotakiwa ni upendo, mshikamano na undugu tukiwa na vitu hivyo tutaenzi utamaduni wetu,”alisema Mhandisi Gabriel.

Amesema washindi wengine ambao wako mikoani kwao watakabidhiwa zawadi zao na Mratibu wa Tamasha hilo, Chifu Aron Mikomangwa Nyamilonda wa III.

Akizungumza na Mtanzania Digital baada ya kukabidhiwa zawadi zake, mshindi wa mchezo wa bao, Nestory Shishi, aliwaomba waandaaji wa mashindano hayo kuongeza muda katika mashindano yajayo kutoka dakika tano hadi kumi ili kuwapa nafasi washiriki kuonesha vipaji vyao vizuri na kutoa burudani ya kutosha kwa watazamaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles