22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali, wadau waweka mikakati vita dhidi ya lishe duni

Na Clara matimo, Mwanza

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau wa lishe wamekutana jijini Mwanza na kuzindua mradi wa urutubishaji unga wa mahindi.

Wadau hao waliokutana jana ni mashirika yanayojishughulisha na urutubishaji wa vyakula ambayo ni Sanku na Gain ambapo mradi huo utatekelezwa  katika mikoa sita ya kanda ya ziwa  ambayo ni Mwanza, Kagera, Simiyu, Geita, Shinyanga na Mara lengo lakiwa ni kuongeza upatikanaji wa unga salama uliorutubishwa ambao utaendana na vipaumbele vya serika vya afua ya lishe.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk.Thomas Rutachunzibwa, wa kwanza kutoka kulia akisikiliza maelezo namna virutubisho vinavyochangwanywa kwenye unga wa mahindi wakati wa kusaga  kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi wa kampuni ya kipipa Millers LTD inayozalisha unga ulioongezwa virutubisho kwa ufadhili wa Shirika la Sanku akiwa na Kaimu Katibu Tawala wa  mkoa huo , Emil Kasagala pamoja na Afisa Lishe Mwandamizi Wizara ya Afya, Peter Kaja.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Lishe Mwandamizi kutoka Wizara ya Afya, Peter Kaja, almesema pamoja na jitihada ambazo Serikali imekuwa ikizifanya kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo lakini bado tatizo la utapiamlo nchini ni kubwa huku likiaathiri zaidi watoto wenye umri chini ya miaka mitano, akina mama wajawazito na wanaonyonyesha.

“Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa Afya na Demografia ya Mwaka 2015/16 udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ulifikia asilimia 34 kitaifa, huku mkoa wa Mwanza ukiwa na asiliamia 39, matokeo hayo pia yalionesha asilimia 4.3 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wana ukondefu wakati asilimia 14.1 ya watoto walikuwa na uzito pungufu ukilinganisha na umri wao.

“Katika kupambana na hali hiyo, serikali iliweka sheria, viwanda vyote vikubwa vinavyozalisha unga wa mahindi, ngano, chumvi na mafuta ya kula viwe vinaweka virutubishi sasa tumetoka kwenye viwanda vikubwa tumehamia kwenye viwanda vidogo tunahitaji navyo viweke virutubishi kwenye bidhaa hizo ili tupambane na changamoto hii  lengo letu ifikapo mwaka 2025 tuwe na asilimia 50 tutoke kwenye 34,” alisema Kaja.

Kwa upande wake Afisa Lishe mkoa wa Mwanza, Sophia Lugumi, alisema mwaka 2020/2021 mkoa huo ulikuwa na asilimia 0.6 wenye udumavu, waliozaliwa hai wakiwa na uzito chini ya kilogramu 2.5 asilimia sita wenye uzito pungufu asilimia tisa.

“Katika vituo vya kutolea huduma za afya asilimia 76 ya akina mama wajawazito walipewa vidonge vya kuongeza damu ili kupambana na tatizo la upungufu wa damu wakati wa ujauzito na wakati wa  kujifungua.

 “Tatizo ni kubwa hivyo wito wangu kwa jamii waupokee mradi huu, wakianza kula vyakula ambavyo vimeongezwa virutubishi tutapunguza tatizo la upungufu wa damu kwa mama wajawazito, watoto na vifo vitokanavyo na uzazi pia uelewa kwa watoto utaongezeka na watafundishika wakiwa shuleni,  ufaulu utaongezeka,“ alisema na kuongeza

“Virutubishi  hivi  ni vya kisayansi vimekubalika na mashirika yetu ambayo yanahusika na masuala ya viwango TBS na TMDA wamefanya uhakiki wameona vina faida kwenye jamii, tumeanza na unga wa mahindi kwa sababu ni chakula ambacho kinaliwa kwa wingi na watu wa lika zote virutubishi  vinavyowekwa ni  madini chuma, zinc na vitamin B 12,” alisema.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk.Thomas Rutachunzibwa, alisema tatizo la utapiamlo na ukosefu wa vitamini linasababisha watoto kuzaliwa wakiwa na vichwa vikubwa na mgongo wazi hivyo inapaswa jamii ishirikiane katika kulitatua.

“Nawashukuru sana wadau wetu Sanku, Gain na Kipipa Millers Ltd ambao ni wazalishaji wa unga wenye virutubishi naamini kupitia mradi huu watoto watazaliwa wakiwa salama maana mama anapata virutubishi kila siku kabla ya ujauzito hata akipata ujauzito anakuwa na virutubishi tayari mwilini,” alisema.

Meneja  Mwandamizi kwa ajili ya mashirikiano wa kampuni ya Sanku, Gwao Omari alisema ili kutekeleza mradi huo kwa ufanisi wamegawana majukumu na Gain ambapo wao wanajishughulisha na masuala ya urutubishaji kwa kutumia teknolojia walioigundua inayoongeza virutubishi katika unga, wanatoa virutubishi ambavyo vinaendana pamoja na mashine na mafunzo jinsi mashine hiyo inavyofanya kazi,

 “Tunaingia mikataba na wazalishaji wadogo wamiliki wa mashine zinazozalisha unga wa mahindi tunawapa bure teknolojia yetu tunawatengenezea mifuko ya kuhifadhia unga ambayo tumeitengeneza kwa  kuzingatia vigezo vya TBS pia tunawapa bure virutubishi ambavyo wanaviongeza katika unga wa mahindi lengo ni kuisaida serikali kupambana na tatizo la utapiamlo na udumavu,”alisema Omari.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Kipipa Millers LTD, inayozalisha unga wenye virutubishi kwa kutumia teknolojia ya Sanku,  Jofrey Peter, alisema jamii imetambua umuhimu wa kula vyakula vyenye  virutubishi kwani kwa siku anazalisha zaidi ya tani tatu za unga ambapo anafunga katika ujazo tofauti tofauti kuanzia kilo tano hadi 50 ili kila mteja anunue kulingana kadri ya uwezo na mahitaji yake.

Meneja Mradi wa urutubishaji vyakula kutoka Shirika la Gain, Archard Ngemela, alisema majukumu yao ni kushirikiana na taasisi za  serikali kutoa mafunzo kwa kamati za lishe kwenye masuala ya urutubishaji wa vyakula  ili waweze kuyasimamia katika maeneo yao ya kazi, kuwajengea uwezo  wazalishaji  katika masuala ya urutubishaji wa vyakula vyenye viwango kwa kuzingatia sheria zilizopo ili waendane na matakwa ya sheria za nchi yanayotakiwa katika masuala ya viwango vya usalama wa vyakula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles