Na Ramadhan Hassan,Dodoma
MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imesema itaendelea kuwajengea uwezo Wahandisi ambao wametoka vyuoni lengo likiwa ni kuhakikisha wanakuwa na ubora ili kuitekeleza vizuri miradi mbalimbali nchini.
Pia imesema taendelea kusimamia sheria ya ununuzi wa umma kwa kufanya ukaguzi wa thamani ya fedha katika mikataba mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana.
Sheria ya ununuzi wa umma inaitaka kila Taasisi ya Serikali kuandaa mpango wake wa ununuzi wa mwaka  sambamba na maandalizi ya bajeti hivyo sheria hiyo imeweka misingi ya uwazi,ushindani na haki inayopaswa kuzingatiwa na Taasisi za Serikali ili kupata huduma bora.
Akizungumza jana Jijini hapa katiba banda la PPRA wakati wa maadhimisho ya 18 ya siku ya Wahandisi kwa mwaka 2021 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Mhandisi Mary Swai amesema wanaendelea kutoa elimu kwa Taasisi mbalimbali kuhusiana na sheria ya manunuzi ya umma ambapo amedai pia watawajengea uwezo wakandarasi ambao wanatoka katika vyuo lengo likiwa ni kuhakikisha miradi mbalimbali inatekelezwa vizuri na kwa ufanisi.
PPRA imeweka banda katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini hapa kwa lengo la kutoa elimu kuhusiana na kazi mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka hiyo.
Mhandisi Swai amesema sheria ya ununuzi wa umma inazitaka Taasisi za Serikali kutoa upendeleo kwa makundi maalum yaani wanawake,vijana,wazee na watu wenye mahitaji maalum kwa kutenga asilimia 30 ya bajeti yake ya ununuzi kwa makundi hayo.
Amesema ili kuhakiki kama Taasisi za Serikali zinazingatia takwa hili la kisheria PPRA ilifanya ukaguzi maalum katika eneo hilo.
Hata hivyo, Kaimu Mtendaji huyo amewataka wanawake nchini kuchangamkia fursa ya fedha hizo kwani wengi wamekuwa hawajitokezi. Â Â