Na Brighiter Masaki
-Dar es Salaam.
Kufuatia uwepo wa ubovu wa baadhi ya Barabara Jijini Dar es salaam, Mkuu wa Mkoa huo, Abubakar Kunenge ameelekeza TARURA kuhakikisha inaanza Mara moja Ujenzi na ukarabati wa Barabara Muhimu zenye mashimo ili kuondoa kero na usumbufu kwa wananchi.
Kunenge ametoa agizo hilo wakati alipotembelea baadhi ya Barabara Jijini humo ambapo ameshuhudia uwepo wa mashimo yanayofanya vyombo vya usafiri kupita kwa tabu na kusababisha malalamiko kwa Wananchi Jambo lililopelekea kutoa agizo hilo.
Miongoni mwa Barabara alizotembelea Kunenge ni Vingunguti Darajani kuelekea Barakuda yenye urefu wa Km 1.24 ambayo kwa mujibu wa Mratibu wa TARURA Mkoa wa Dar es salaam Mhandisi Geofrey Mkinga amesema Mkandarasi amekabidhiwa Kazi leo na anatakiwa kukamilisha kazi kwa muda wa miezi miwili kuanzia leo ambapo Mkuu wa Mkoa ametaka Ujenzi kufanyika usiku na Mchana.
Aidha Kunenge ametembelea Barabara ya Gerezani – Machinga Complex yenye changamoto ya Mashimo ambapo amemuelekeza Meneja wa TARURA Jiji la Ilala Samwel Ndoven kuhakikisha ifikapo Jumatano ya Mei 19 Barabara ikamilike kwa ubora na kuanza kutumika.