30.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

Makala: Wananchi walia na utamaduni wa watoto wa kike kusindikiza bibi harusi

Na Damian Masyenene, Shinyanga

Asiliami 53 ya watu katika mkoa wa Shinyanga ni watoto, ambapo mkoa huo unatajwa kuwa kinara nchini kwa idadi kubwa ya ndoa za utotoni (59%), huku ukiorodheshwa katika namba tano kwa mimba za utotoni ukiwa na asilimia 34, kwa mujibu wa utafiti wa afya na idadi ya watu (DHS) Tanzania, 2014.

Pamoja na takwimu hizo, ripoti ya mpango mkakati wa mkoa huo wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2020/21 hadi 2024/25, inaeleza kuwa katika kipindi cha Julai, 2018 hadi Juni, 2019 kesi 32 za ndoa za utotoni ziliripotiwa kwenye mamlaka mbalimbali, huku sababu za ndoa hizo zikitajwa kuwa ni imani potofu na kandamizi, kuporomoka kwa maadili, umaskini na kipato duni cha familia pamoja na malezi yasiyofaa ya wazazi.

Picha: Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ambaye pia ni Mratibu wa Kamati ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika halmashauri hiyo, Aisha Omary.

Kutokana na kuendelea kuwepo kwa matukio ya ndoa na mimba za utotoni katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, baadhi ya wananchi katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wamesema baadhi ya wazazi na walezi wanaendeleza mila na desturi zinazowapa uhuru watoto wa kike kujiingiza katika mapenzi wakiwa kwenye umri mdogo.

Baadhi ya wananchi hao waliozungumza na www.mtanzania.co.tz katika Kata ya Mwamala halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani hapa, ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa ‘nafasi ya vyombo vya habari katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto’ unaofadhiliwa na Women Fund Tanzania (WFT), wamebainisha kuwa utamaduni wa watoto wa kike kusindikiza harusi za kimila, umekuwa chanzo cha mabinti kupata ujauzito na kuolewa katika umri mdogo.

Mmoja wa wananchi hao, Ramadhan Dotto, alieleza kuwa panapotokea harusi katika kijiji, huteuliwa watoto wa kike wenye umri mdogo kwenda kusindikiza kule anakoolewa msichana mwenzao wanaeishi nae, ambapo watoto hao (wasindikizaji) huishi kule ugenini (ukweni) kwa siku tano hadi saba.

“Watoto hao wa kike wanaoenda kwa ajili ya kumsindikiza mwenzao wanakutana na watoto wa kiume ambao wanakuwa wameandaliwa kabisa kwa ajili ya kubadilishana mawazo na usiku hulala nao kama mke na mume, hali ambayo imekuwa ikihatarisha maisha ya watoto wa kike ikiwemo mimba na kupata maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU),” alieleza.

Naye Ester Maige amesema kuwa baadhi ya wazazi huwaruhusu watoto wao kwa kigezo kuwa wanafanya ushirikiano na kwamba kumsindikiza mwenzao nao watapata wanaume wa kuwaoa kama alivyoolewa waliyemsindikiza, hivyo huwaruhusu kwa kujua kuwa nao watakuja kuchumbiwa  baada ya kuonekana huko ugenini.

Kwa upande wake, Lucy Amos akizungumzia utamaduni huo alisema kuwa wazazi ndiyo wamekuwa wakiwajengea watoto wa kike mazingira ya kusindikiza  na wakifika huko wanakuwa huru bila uangalizi wowote, hivyo hujikuta wakishiriki vitendo vya ngono na vijana wa huko ugenini bila tahadhari zozote.

“Hizi mila na desturi zimekuwa hatari kwa watoto wetu hususan wa kike kwa sababu huwapelekea kushiriki vitendo vya ngono bila tahadhari na kupata mimba, magonjwa ya zinaa ikiwemo Ukimwi na wengine kuachishwa masomo kwa kuolewa,” alibainisha.

Inaelezwa kuwa utamaduni wa mabinti kumsindikiza ukweni mwenzao anayeolewa ni wa kawaida kwa maeneo mbalimbali katika mkoa wa Shinyanga, ambapo hufanya hivyo ili kumfanya binti anayeolewa asiende ukweni peke yake kwani kabla hajaolewa alikuwa akiishi na wenzake na kucheza nao.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Kata ya Mwamala, Suzan Kayange, aliwataka wajumbe wa kamati ya kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na wanawake kuwaelimisha wanajamii katika maeneo hayo waweze kubadilika kifikra.

“Mila na desturi ambazo mnaendelea kuzitumia zimeshapitwa na wakati tunatakiwa kuwalinda watoto wetu na kuwalea katika maadili mema ili baadae tuje tufurahie matundu yao kuliko kuwapoteza na kupotezea ndoto zao,” alisistiza.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Mwamala, Sophia Philbert alitoa wito kwa wazazi kubadilika kimtazamo na kutokuwa chanzo cha mimba na ndoa za utotoni kwa mabinti zao, kwani dhana ya kuwaruhusu watoto kumsindikiza mwenzao kwa nia ya kupata wenza, huwaletea pia magonjwa watoto hao na kuyaweka maisha yao hatarini.

Akizungumzia jitihada za halmashauri ya wilaya ya Shinyanga katika kutokomeza vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto, Afisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo, Aisha Omary amesema kuwa wamefanya jitihada kubwa za kutoa elimu na kusaidia kubadilisha fikra, ambapo baadhi ya wazazi wameacha vitendo hivyo.

“Tunaendelea kuelimisha jamii ili iweze kuwanusuru watoto wa kike waweze kutimiza ndoto zao, serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali ukiwemo mradi wa nafasi ya vyombo vya habari yamepewa fedha na Women Fund Tanzania (WFT) kwa ajili ya kuelimisha jamii ya wilaya ya Shinyanga kwa ajili ya kutokomeza ukatili wakijinsia dhidi ya wanawake na watoto,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles