24 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

Vyuo 31 vyatafuna fedha za wanafunzi hewa

Profesa Joyce Ndalichako
Profesa Joyce Ndalichako

Na WAANDISHI WETU, DAR NA ARUSHA

SERIKALI imetoa siku saba kwa vyuo 31 nchini, kuhakikisha vinarejesha zaidi ya Sh bilioni 3.8 zilizotolewa kwa wanafunzi hewa 2,192.

Agizo hilo limetolewa jana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam .

Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, fedha hizo zilizotafunwa zilitolewa na Serikali katika mwaka wa fedha wa 2015/2016.

“Serikali iliamua kufanya uhakiki wa wanafunzi wanufaika wa mikopo katika vyuo 81 nchini. Katika uhakiki wa awali uliofanywa katika vyuo 31, ilibainika wanafunzi 2,763 walikuwa hewa.

“Tulichukua jukumu la kutangaza majina ya wanafunzi hao hewa katika vyombo vya habari ambapo wanafunzi wengine 571 walijitokeza katika uhakiki wa awamu ya pili na tatu.

“Baada ya kukamilisha uhakiki, wanafunzi wote 84, 256, wanafunzi 2,192 hawakujitokeza na sasa tumeamua kusitisha malipo yao fedha zilizokuwa zimetafunwa, zirejeshwe ndani ya siku saba wakati taratibu za kinidhamu zikiandaliwa kwa waliohusika katika upotevu wa fedha hizo,”aliagiza Profesa Ndalichako.

Ili kukabiliana na udanganyifu wowote, vyuo vyote vya elimu ya juu vimeagizwa kuweka mifumo mizuri ya uhifadhi wa kumbukumbu za wanafunzi kuanzia usajili, matokeo ya majaribio, mitihani na akaunti zao.

Pia, vyuo vyote vimetakiwa kuwasilisha Bodi ya Mikopo kwa wakati taarifa zote za kitaaluma na za kibenki za wanafunzi ili kuiwezesha bodi kufanya marekebisho yanapotakiwa katika kumbukumbu zao.

Pamoja na hayo, Profesa Ndalichako aliagiza uchunguzi zaidi ufanyike ili kubaini fedha za mikopo zilizolipwa kwa watu wasiostahili na kuahidi kuwaandikia barua wakuu wa vyuo vyote vilivyokumbwa na kashfa hiyo.

“Hatua hii itatusaidia kudhibiti ulipaji hewa kwani tumebaini baadhi ya waliofukuzwa vyuo mwaka 2013/ 2014, waliendelea kupokea fedha hadi mwaka 2015/ 2016,”alisema.

Akizungumzia changamoto walizokutana nazo wakati wa uhakiki, Profesa Ndalichako alisema baadhi ya maofisa wa benki walikuwa wakikataa kutoa ushirikiano kila walipotakiwa kufanya hivyo.

“Baadhi ya benki zilithubutu kutoa taarifa za malipo ya wanafunzi ambazo hazilingani na kiasi cha fedha kilicholipwa, kwa kweli hali ilikuwa ngumu.

Profesa Ndalichako alivitaja vyuo vilivyokuwa na wanafunzi hewa kuwa ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph- Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana Dodoma (SJUT) na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU).

Vingine ni Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Chuo Kikuu cha Theophil Kisanji, tawi la Mbeya, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (RUCU), Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUTI – Mwanza) na Chuo Kikuu cha Arusha (UOA).

Vingine ni Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE- Dar es Salaam ), Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UOB), Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa (SEKOMU ), Chuo Kikuu cha Iringa (UOI), Chuo Kikuu cha Mzumbe (MU), Chuo Kikuu cha Kiislam (MUM- Morogoro), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana- DSM (SJUT- DSM), na Chuo Kikuu cha Jordan (JUCO- Morogoro).

Vyuo vikuu vingine ni Chuo Kikuu cha Tiba Bugando (CUHAS), Chuo Kikuu cha Mkwawa Iringa (MUCE), Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Chuo Kikuu cha Mount Meru (MMU, Arusha), Chuo Kikuu cha Makumila Arusha (TUMA), Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MOCU), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT- Arusha), Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT- Mbeya) na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE- Dodoma).

Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, vyuo vyote hivyo vilikuwa na wanafunzi hewa 84, 256.

Naye Mchunguzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Abubakar Msangi, alisema katika uhakiki huo walibaini akaunti nyingi zinazoingiziwa fedha za mikopo ni za wanafunzi waliomaliza vyuo.

Kwa upande wake, Mchunguzi wa Ndani wa Bodi ya Mikopo, Godfrey Sigala, alisema wakati wa uhakiki, walisaidiwa zaidi na marais wa vyuo baada ya baadhi ya watumishi wa vyuo kugoma kutoa ushirikiano.

KINONDONI

Wakati hali ikiwa hivyo katika vyuo vikuu, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam nayo ina wanafunzi hewa 5,996.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles