27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

15 WAKAMATWA KWA KUKAIDI KUHAMA MABONDENI

Veronica Romwald na Julieth Julius -Dar es Salaam

WATU 15 wanaoishi katika Bonde la Msimbazi, wamekamatwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, wakidaiwa kukaidi amri ya kuhama katika maeneo hayo.

Askari wa jeshi hilo walifanikiwa kuwakamata watu hao kwa kushirikiana na viongozi wa Manispaa ya Ilala, walipofanya operesheni kali ya kuwakamata watu wanaoendelea kuishi kwenye maeneo hatarishi ya mabondeni eneo la Buguruni, Kata ya Vingunguti.

Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Simon Sirro, aliwaeleza waandishi wa habari juzi ofisini kwake kwamba operesheni hiyo ilifanyika Machi 15, katika maeneo hayo.

“Operesheni hii inafanyika kufuatia kukiukwa kwa amri ya mahakama inayowataka watu hao kuhama katika maeneo hayo hatarishi, kufuatia kuwepo kwa mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha mafuriko,” alisema.

Aliwataja waliokamatwa ni Mohamed Hatibu, Mwanaidi Mwinyimvua, Kulwa Antony, Mwanahamisi Ally, Sophia Mwinjuma, Salim Juma, Mwajuma Athumani, Saada Said, Sabahi Abdallah, Mariam Abbasi, Ashura Petro, Fitina Mohamed, Faudhia Juma, Magreth John na Ayoub Abdallah.

“Watu hawa wanatoka katika familia tofauti tofauti, tumewahoji na wamekiri kuendelea kukaa katika maeneo hayo hatarishi na kwamba wanasubiri maelekezo kutoka kwa Serikali,” alisema Sirro.

Aliongeza kuwa watuhumiwa hao wameachiwa kwa dhamana na kwamba upelelezi bado unaendelea na pindi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.

Wakati huo huo, Kamishna Sirro alisisitiza wananchi kuendelea kushiriki ulinzi shirikishi katika maeneo yao kwani suala hilo lipo kwa mujibu wa Katiba.

“Jiji la Dar es Salaam limekua, sasa hivi kuna watu zaidi ya milioni sita, tupo askari zaidi ya 6,000. Kwa idadi hii inamaanisha kila askari anapaswa kulinda raia zaidi ya 1,000 wao na mali zao jambo ambalo ni changamoto.

“Awali tulilazimika kuzuia ulinzi shirikishi kwa sababu watu walianzisha tu wenyewe na badala ya kulinda maeneo yao walikuwa wanakwenda kulinda mitaa mingine, huu ni ubabaishaji ambao ulisababisha vitendo vya rushwa na uhalifu na wananchi wakaanza kulalamika.

“Lakini vikundi vinavyoanzishwa sasa, vinasimamiwa na mwenyekiti wa mtaa husika ambaye kwa mujibu wa sheria ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama katika mtaa husika,” alisema.

Kamishna Sirro alisema kwa kuwa vikundi hivyo vipo chini ya wenyeviti, ulinzi shirikishi sasa umeanza kuzaa matunda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles