30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

CCM KURUKA BAADA YA KUJINYONYOA MANYOYA?

Na Dennis Luambano, aliyekuwa Dodoma

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, wamehalalisha mabadaliko ya katiba yao.

Mabadiliko hayo yameibua kishindo kinachowapiga panga wajumbe na kuanzia sasa wanakosa sifa za kuhudhuria vikao vya uamuzi vya chama hicho, baada ya idadi kubwa kupunguzwa.

Awali, uhalali wa mabadiliko hayo ulikuwa ni fumbo gumu kwa siku nne mfululizo mjini Dodoma, kuanzia Alhamisi hadi Jumapili ya wiki iliyopita, wanachama wengi hawakuweza kuling’amua.

Kila mmoja alikuwa akisema lake, inawezekana mabadiliko hayo yatamfanya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. John Magufuli, aogopwe ndani ya chama hicho kama anavyoogopwa serikalini.

Kwamba baada ya mageuzi au mabadiliko hayo, huenda sasa hakuna mjumbe au mwanachama wa CCM atakayethubutu kumpinga au kumhoji Magufuli kikaoni kama ilivyokuwa zamani. Bila shaka atakayethubutu ataitwa msaliti, kwa maana ataonekana ni bata ndani ya kundi la kuku.

Pia mageuzi hayo pengine yataliendeleza lile fumbo la wanachama wengi kushindwa kuijua kesho yao itakuwaje.

Mbali na hayo, pia mageuzi hayo yamekwenda tofauti na ule msemo kwamba yaliyopita si ndwele tugange yajayo, kwa sababu kuna baadhi ya wanachama wamepewa adhabu kutokana na makosa waliyoyafanya kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi, ikiwamo kumuunga mkono aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Pamoja na mambo mengine, hakuna ubishi kwamba, utendaji wa baadhi ya wajumbe na viongozi wa CCM ulikuwa wa mazoea.

Kwa sababu miaka ya nyuma walikuwa wanafanya mambo kadha wa kadha, hivyo walitaka waendelee kufanya kama ilivyo kawaida yao, licha ya mazingira na wakati kubadilika.

Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana baadhi yao ni waoga wa mabadiliko, hali hiyo ilionekana mkoani Dodoma, kutokana na ‘kiwewe’ walichokuwa nacho kabla ya mkutano huo kuanza. Kwamba walitaka mabadiliko hayo yachelewe, licha ya kupendekezwa lakini kwa bahati mbaya yamewakuta kabla hawajajiandaa, wamelazimika kuyakubali kwa shingo upande.

Ndiyo! Hawakuwa na namna zaidi ya kuyaunga mkono, ingawa kabla hayajapitishwa na mkutano huo maalumu uliofanyika Jumapili ya Machi 12, mwaka huu katika ukumbi wa CCM Convention Centre ambao kwa sasa unaitwa Kikwete Hall, kulikuwa na tetesi zilizozagaa kuwa baadhi ya wajumbe watayapinga.

Tetesi hizo ziliambatana na hofu kwa baadhi yao kukosa nafasi za kuwa wajumbe wa vikao vya juu vya kutoa uamuzi na ndiyo maana hata zile shamra shamra za Dodoma pindi mikutano ya chama hicho inapofanyika hazikuwa kubwa kama miaka ya nyuma, sababu kubwa baadhi ya wajumbe hawakujua kesho yao kama nilivyosema hapo mwanzo.

KWANINI MABADILIKO

Kwa kawaida kila kiongozi au mtawala ana mtindo wa kuongoza taasisi aliyopewa.

Mtindo wa mtawala fulani hauwezi kufanana na wa mwingine, kwa mantiki hiyo, mabadiliko hayaepukiki na si jambo la mchezo na si kila mtu anayapenda, ndiyo maana yaliibua hekaheka na maswali mengi kwa wajumbe.   

Je, kwanini baadhi ya wajumbe walikuwa na hofu? Je, mabadiliko madogo ya katiba ya chama hicho ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2012, kanuni zake na jumuiya zake yamefanywa kwa bahati mbaya? Jibu la swali hilo ni hapana, kwa sababu yalifuata taratibu zote za vikao vya chama hicho, ndiyo maana baadhi yao waliamini pengine sehemu ya kwenda kupingwa ni katika mkutano huo maalumu kutokana na idadi ya wajumbe wake kuwa wengi.

Siku moja kabla ya mkutano huo kufanyika, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. John Magufuli, aliendesha Mkutano wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa (NEC) wa White House, aliwalainisha kwa kuwaambia wajumbe kuwa wanakutana kwa kazi maalumu waliyoianza jijini Dar es Salaam Desemba 13, mwaka jana na aliwashawishi kuwa hatarajii kuchukua muda mrefu kujadiliana.

“Tumeshawahi kufanya mabadiliko mengi siku za nyuma, sitarajii kama tutajadili sana, sitarajii kama mkutano huu utakuwa mrefu,” anasema na kuongeza:

“Naamini yote tuliyojadili yatapitishwa kwa sababu mabadiliko ndani ya CCM ni jambo la kawaida. Nimeambiwa kwamba, Chama tawala cha China kina wajumbe wa NEC yao 205, licha ya kwamba nchi nzima idadi ya watu ni bilioni moja, ANC cha Afrika Kusini kina wajumbe 110, lakini sisi tupo 163, mabadiliko ni kitu kizuri.”

Hakuishia hapo, bali aliwatoa hofu wajumbe wa mkutano huo.

“Ni lazima tujipange katika kufanya mabadiliko, makatibu wa mikoa wa chama ambao idadi yao inafikia 30 hawana ulazima wa kuwa wajumbe wa NEC,” anasema na kuongeza:

“Wajumbe wa NEC vyeo ni vingi, nililizungumza na wala msiwe na wasiwasi, sisi ndio watawala, sisi ndio Serikali na ushahidi unajulikana kwa sababu wengine nimeshaanza kuwachukua chukua, tukubali mabadiliko kwa ajili ya chama chetu na kwa faida ya chama chetu.”

Akitoa ufafanuzi wa uamuzi wa kufanya mabadiliko madogo ya katiba hiyo katika mkutano maalumu, Magufuli, ambaye pia ni Rais wa nchi, anasema madhumuni ya kufanya hivyo ni kuboresha muundo na mfumo wa chama hicho.

“Wajumbe wa mkutano mkuu, naomba sasa nizungumzie suala lililotuleta hapa, kama mnavyofahamu chama chetu kimekuwa na utamaduni wa kujitathmini kila wakati na kufanya mageuzi ambayo yamekuwa chachu ya kukifanya kiendelee kudumu na kuzidi kuimarika na kwenda na wakati,” anasema na kuongeza:

“Kutokana na utamaduni huo, ambao umejengeka ndani ya chama chetu, NEC yetu ilikutana Desemba, mwaka jana na kupokea tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi, baada ya kupitia taarifa hiyo iliyobainisha changamoto na mapendekezo. NEC ilipitisha maazimio yenye lengo la kukiwezesha chama chetu kutekeleza majukumu yake ili kuendana na mazingira ya sasa ya ushindani.”

Anasema baadhi ya maazimio yalianza kutekelezwa mara moja, lakini mengine yalihitaji kufanyika kwanza kwa marekebisho ya Katiba ndipo yatekelezwe.

“Hii ndiyo sababu kubwa ya kuitisha mkutano huu maalumu, tumeuitisha ili kuwapa fursa nyinyi wajumbe kupitia marekebisho ya Katiba yanayopendekezwa, muyatafakari na ikiwezekana muyapitishe,” anasema.

Pia anasema licha ya mfumo na muundo wa chama hicho kuwapatia mafanikio, lakini kuna upungufu na kasoro.

Anasema mathalani, kuna mwingiliano mkubwa wa kimajukumu baina ya taasisi za chama na jumuiya zake.

Mwingiliano huo ndio umechangia chama hicho kuwa na watendaji wengi wanaotekeleza majukumu yanayofanana na kusababisha migongano.

Mbali na hayo, anasema anataka chama hicho kiwe na muundo mdogo wenye kuonyesha mgawanyo wa majukumu na uwajibikaji kuanzia ngazi ya juu hadi ya chini na ionyeshe uhusiano kati ya chama hicho na jumuiya zake.

Anaongeza, vyeo vyote ambavyo haviko katika katiba ya chama hicho wanaviondoa, ndiyo maana NEC ilipeleka mapendekezo yenye lengo la kuongeza ufanisi na kuboresha utendaji.

“Naamini mtakubaliana na mimi kuwa utendaji kazi ndani ya chama chetu ulikuwa umeshuka sana, hasa uchaguzi ukimalizika na saa nyingine hata ndani ya uchaguzi kumekuwa na watu wanaokosa heshima mbele ya viongozi wa chama na mbele ya chama chenyewe,” anasema.

WARAKA WA KINANA

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, aliwasilisha waraka unaoelezea mabadiliko ya katiba ya chama hicho yaliyopitishwa na wajumbe wa mkutano huo baada ya kuhojiwa na Magufuli kama wanayakubali au hawayakubali.

Akiwasilisha waraka wa sababu tano za mabadiliko hayo, anasema chama hicho kimeshawahi kufanya mabadiliko 15 ya katiba na kanuni zake na yale ya wiki iliyopita yalikuwa ni ya 16.

“Si mara ya kwanza kwa CCM kufanya mabadiliko ya katiba na sera zake na kila baada ya miaka mitano huwa tunafanya tathmini kuanzia matawi hadi Taifa,” anasema na kuongeza:

“Na ya sasa hivi ni kabambe, kwa sababu tulifanya kwa miezi 12 na yalitolewa mapendekezo mbalimbali, kwa hiyo mabadiliko haya yanatokana na wana CCM wenyewe, hayatokani na mtu, kuna watu wanajaribu kupotosha kwamba mabadiliko haya ni ya mtu au kikundi, si kweli, hayatokani na mtu au kikundi cha watu, ni uamuzi wetu wana CCM pia, hayamlengi mtu au kikundi cha watu, bali yanalenga uhai na ubora na ushindi wa CCM.

“Tunafanya mabadiliko yenye malengo ya kuongeza ufanisi, uwajibikaji katika nafasi zote kuanzia utendaji na kutoa fursa zaidi na kuweka mkazo zaidi ndani ya chama.”

Kupitia mabadiliko hayo, anasema idadi ya wajumbe katika vikao vya uamuzi vya chama hicho imepunguzwa, huku Kamati Kuu iliyokuwa na wajumbe 34 sasa itakuwa 24, NEC watakuwa wajumbe 162 kutoka 388 na wajumbe wa Mkutano Mkuu watakuwa 1,000 badala ya 2,380 ya awali.

TSUNAMI YA MABADILIKO ILIVYOMSOMBA SOPHIA SIMBA

Kama nilivyosema mwanzo, yaliyopita hayakuwa ndwele kwa sababu kuna wanachama wamesombwa na tsunami ya mabadiliko hayo. Kimsingi wamefukuzwa. Je, tafsiri ya kufukuzwa kwao ni nini?

Kwanini wengine wamefukuzwa na wengine wamepewa onyo kali, licha ya makosa yao kufanana na hakuna ufafanuzi uliojitosheleza kuhusiana na adhabu hizo, huku wengine wakiwa hawajui makosa yao? Je, ni kweli wanachama hao walipatikana na makosa ya maadili kinyume cha katiba na kanuni za uongozi za chama hicho kama ilivyosemwa?    

Kimsingi, wajumbe wa NEC waliridhia kuwafukuza wanachama 12, akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Taifa na Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Simba na wenyeviti wa CCM mikoa ambao ni Jesca Msambatavangu (Iringa), Erasto Kwilasa (Shinyanga), Ramadhan Madabida (Dar es Salaam) na Christopher Sanya (Mara), huku Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akipewa onyo kali na wengine walipewa adhabu ya kuachishwa uongozi kutokana na kile kilichotajwa kuwa ni usaliti.

Akitangaza adhabu hizo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, anasema Sophia na wenzake walipatikana na hatia ya makosa ya kiuadilifu na kiuongozi ya chama hicho.

“Kwa sauti moja wajumbe wa NEC wameridhia kuwafukuza uanachama wanachama hao,” anasema na kuongeza:

“CCM imeanza safari ya mageuzi na kuna watu walikuwa wanasema hatuchukui hatua, sasa tumeanza kuchukua hatua kwa watu waliokihujumu chama na waliokisaliti na kukifanya kinuke mbele ya wananchi.

“Tumechukua uamuzi kwa baadhi ya wanachama na huu ni mwanzo tu wa kuelekea katika mageuzi, vikao vya chama havitakuwa na ajizi ya kuchukua hatua kwa mwanachama au kiongozi yeyote anayekwenda kinyume. Masuala ya kimaadili ndani ya chama chetu siyo ya kuyafanyia mchezo na vikao vilivyotoa uamuzi ni vya mwisho na hakuna rufaa.”

KAMATI YA MANGULA

Pia anasema NEC imeridhia kuundwa kwa kamati ndogo chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, kwa ajili ya kwenda Zanzibar kuangalia hali ya siasa na kufanya tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.

Aliwataja wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni Pandu Amiri Kificho, Daud Ismail, Suleiman Zaharani, Shamsi Vuai Nahodha, Dk. Maua Daftari, Steven Wasira, Hadija Ngozi na Zakhia Meghji.

Licha ya CCM kufanya mabadiliko au mageuzi ya katiba yake, je, yataleta tija kama ilivyokusudiwa, ikiwamo kupunguza gharama ya fedha za uendeshaji wa vikao baada ya kupunguza idadi ya wajumbe?

Pamoja na mambo mengine, je, baada ya kufanya mabadiliko hayo, huko mbele ya safari watatafuta nafasi siku moja ya kujitathmini na kujitazama upya ili wabaini kama wataweza kuruka baada ya kujinyonyoa mno manyoya yao? Wakibaini kama walijinyonyoa mno, je, wanaweza kufanya mabadiliko mengine ya katiba yao? Ni suala la muda, ngoja tusubiri tuone.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles