29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi waacha alama 2018

Mwandishi Wetu -Dar es Salaam

WAKATI ikiwa imebaki siku moja kabla ya kuingia mwaka mpya wa 2019, mengi yametokea katika mwaka huu wa 2018 na kwa upande wa wanasiasa, wapo walioacha alama kutokana na hatua walizochukua ama mambo waliyosimamia.

Pia wapo walioishia kutoa matamko yasiyotekelezeka na wengine wakitumbuliwa na waliowateua kutokana na uamuzi usiokubalika.

Kuweka kumbukumbu sawa, hii ni orodha ya baadhi ya wanasiasa waliofanya vyema na kuacha alama katika maeneo wanayosimamia.

SELEMANI JAFO

Selemani Jafo ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ni kati ya mawaziri wachache walioanza na Rais Dk. John Magufuli alipotangaza baraza lake la mawaziri la kwanza.

Alianza akiwa naibu waziri wa wizara hiyo huku bosi wake akiwa ni George Simbachawene, ambaye baadaye uteuzi wake ulitenguliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Angela Kairuki ambaye sasa amehamishiwa Wizara ya Madini.

Katika kipindi cha miaka mitatu, Jafo amekuwa akisimamia vyema sekta yake jambo lililofanya mara kadhaa hata kusifiwa hadharani na Magufuli.

Pia katika kuonesha ukomavu wa kisiasa, mara kadhaa Jafo amekuwa akikemea tabia ya baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa waliozoea kutoa amri ya watu kukamatwa na kuwekwa ndani kwa saa 48 jambo ambalo mwanzo lilikemewa na baadhi ya wanaharakati na viongozi wa upinzani.

Katika moja ya matamko yake, Jafo alisema: “Unakuta leo hii mkuu wa wilaya anamweka ndani mtu au mtumishi wake kwa sababu ambazo hata hazina tija, eti tu kwa sababu walishagombana huko nyuma na yeye anatumia mamlaka yake kulipa kisasi.

 “Msiende (wakuu wa wilaya) kutafuta ‘kiki’ kwa kuwaweka ndani wananchi na watumishi bali ‘kiki’ zenu mkazitafute kwa kuletea maendeleo wananchi.”

Tamko hilo lilipongezwa na watu kutoka ndani na nje ya chama chake, wakiwamo wanaharakati wa haki za binadamu.

Katika ziara zake pia ameonekana zaidi kusimamia miradi ya Serikali akitaka thamani ya fedha inayotumika ionekane.

Hatua hiyo ilisababisha aikatae baadhi ya miradi iliyoonekana kuwa fedha zilizotumika haziendani na thamani yake.

DOTTO BITEKO

Alianza kujulikana zaidi baada ya kuongoza Kamati Maalumu ya Bunge ya kuchunguza biashara ya madini ya Tanzanite iliyowang’oa baadhi ya mawaziri akiwamo Simbachawene, aliyewajibika kutokana na nafasi aliyokuwa nayo wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne.

Kamati hiyo ilibaini upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali kutokana na madini hayo yanayopatikana Tanzania pekee kutoroshwa kwa wingi.

Hatua hiyo ilisababisha Magufuli kutoa agizo la kujenga ukuta wa kuzunguka machimbo ya madini hayo yanayopatikana Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, jambo ambalo Serikali inasema limefanya mapato yake kuongezeka.

Baada ya ripoti hiyo, Januari, mwaka huu Biteko aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Madini.

Akiwa katika nafasi hiyo, amesimamia kwa kiasi kikubwa kurudisha maeneo ya wachimbaji wadogo waliyodhulumiwa na wafanyabiashara wakubwa.

Huko mkoani Geita alimkuta bibi ambaye ameishi katika eneo lake kwa zaidi ya miaka 50, lakini baada ya kubainika kuwa katika ardhi hiyo kuna madini, aliporwa na kuambiwa ni mali ya kijiji, amri ambayo Biteko aliibatilisha.

Pia katika baadhi ya migodi, alikuta mazingira magumu wakati wa ziara zake ikiwamo wafanyakazi kufungiwa chooni. Tunduru alikuta wageni wanatumia leseni za wazawa kununua madini, wakati Tanga alikuta mchimbaji mwenye leseni ya kuchimba madini, aliitelekeza na kuamua kuchenjua mchanga ambao wenyewe wachimbaji wadogo waliurundika.

Katika Mgodi wa Epanko alikuta tangu miaka ya 1980 ulivyoanza kuchimbwa kodi iliyolipwa ni Sh milioni 20 tu.

Baada ya kugundua hilo, Biteko aliufunga na kuunda kamati iliyobaini kuwa mgodi huo ulikuwa umekwepa kodi ya zaidi ya Sh milioni 500.

Pia katika Mgodi wa Buzwagi alikataa mpango wa kurudisha mazingira yake baada ya kufunga shughuli za uchimbaji kwa sababu wamiliki wake walisema shimo walilochimba wangeliacha lijae maji kwa kipindi cha miaka 100 ijayo.

ANTHONY MTAKA

Mkuu huyu wa Mkoa wa Simiyu amekuwa mfano kwa wakuu wa mikoa wote nchini kuanzia katika kusimamia miradi ya maendeleo vikiwamo viwanda, mazingira bora ya uwekezaji katika mkoa wake na kauli zake awapo majukwaani.

Hatua hiyo ilifanya Magufuli, kumsifia adharani na kusema wakati akitaka kumteua kuna vyombo vilimkataa, lakini kwa sasa amethibitisha ubora wake.

 “Nilipotaka kumteua niliuliza vyombo vyangu nikaambiwa hafai kabisa, lakini nimeuliza ripoti ya wakuu wa mikoa wanaofanya kazi vizuri, wakaniletea Mtaka ndiye namba moja na namba mbili ni yeye, kwa kifupi hana mfano,” alisema Magufuli.

Simiyu chini ya Mtaka imetajwa kujenga viwanda vingi, kusimamia haki kwa watu mbalimbali, kukemea tabia ya baadhi ya walio chini yake waliotaka kutumia sheria vibaya ikiwamo kuweka watu ndani kwa saa 48 na mengine mengi.

ESTER BULAYA

Wakati mwaka ukielekea ukingoni, Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema) ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye ulemavu, Ester Bulaya, alijizolea umaarufu baada ya kutoka hadharani na kupinga kanuni za wizara zilizokuja na vikokotoo vipya vya mafao ya wastaafu.

Bulaya alichochea moto katika mjadala wa Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Kwa Watumishi wa Umma ya Mwaka 2017 na kanuni zake za mwaka 2018.

Kabla ya Bulaya, mjadala huo uliendeshwa zaidi katika mitandao ya kijamii na baadaye Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), ikatoka hadharani na kusema utekelezaji wa kanuni za sheria hiyo umeanza tangu Agosti mwaka huu.

Sehemu kubwa ya mjadala ilikuwa ni kuwapo kwa taharuki miongoni mwa wadau wengi kuhusu kikokotoo cha 1/580 kilichoko katika kanuni, kinachoelekeza kuwa kila mstaafu atakuwa analipwa asilimia 25 ya mafao yake kwa mkupuo na asilimia 75 inayobakia katika mfuko atakuwa analipwa kidogo kidogo kila mwisho wa mwezi kama mshahara.

Mjadala huo uliendelea na baadaye kuwaibua Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) ambao awali baadhi ya watu walihoji ukimya wao.

Mjadala huo ulifungwa kwa Tucta kuomba Serikali warudi mezani kujadili suala hilo na juzi Magufuli akiwa Ikulu, Dar es Salaam alitangaza kikokotoo kilichotumika kwa kila mfuko kabla ya mifuko ya hifadhi ya jamii haijaunganishwa na kuwa miwili kiendelee katika kipindi cha mpito hadi mwaka 2023.

Pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Dk. Irene Kisaka.

ZITTO KABWE

Mbunge huyu wa Kigoma Mjini kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, aliibua sakata la Sh trilioni 1.5 alizosema katika bajeti ya mwaka jana hazionekani zilipo.

Hoja hiyo ilipamba moto wakati wa Bunge la Bajeti, lakini baadaye Serikali ilitoa ufafanuzi wa suala hilo.

Pia mwaka huu unaoisha umeweka historia mpya katika maisha yake ya siasa za upinzani baada ya kukamatwa na polisi na kulala ndani kwa siku kadhaa kabla ya kupelekwa mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles