24.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

UVUMBUZI: Teknolojia zitakazovuma 2019

MWANDISHI WETU NA MTANDAO

KATIKA ulimwengu wa sayansi na teknolojia, kila siku kunaibuka mahitaji na ulazima wa uundwaji na uvumbuzi wa vitu mbalimbali vyenye teknolojia ya hali ya juu.

Lakini pia wakati teknolojia mpya zikizidi kubuniwa, uvumbuzi duniani na matumizi ya teknolojia zilizopo unabadilisha utendakazi wa kampuni nyingi na jinsi wanadamu wanavyotangamana.

Maendeleo katika uwezo wa kompyuta kufanya kazi za wanadamu, uchanganuzi wa data kubwa na upanuzi wa mtandao wa intaneti ni miongoni mwa mambo yanayochochea mapinduzi hayo.

Kwa msaada wa mtandao, zifuatazo ni orodha ya teknolojia kuu zinazoweza kubadili maisha mwaka huu wa 2019.

1.Matumizi ya mashine kufanya kazi za binadamu

Teknolojia ya roboti inatarajiwa mwaka huu kuwa na sifa kamili za mwanadamu kama kuzungumza, kusoma, kuona, kufikiria na kutambua vitu au watu wanaotembea.

Kwa kutumia teknolojia ya hesabu ya mashine (algorithms) inayowiana na mahali, zitaweza kufanya kazi ambayo inachosha au hatari kwa binadamu, kwa kasi zaidi na kwa umakini zaidi.

Teknolojia hii inatarajiwa kuvuruga kila sekta ya uchumi, huku kampuni nyingi zikiipendelea kwa uwezo wake wa kupunguza gharama na kuongeza ubora.

Mifumo inayohusisha video za 3D, sauti, uwezo wa kushika, kuonyesha maeneo na hata uwezo wa kunusia itabadilisha utendaji wa mitambo kwa uwezo wake wa kutambua mazingira kwa mbashara.

2. Teknolojia ya Blockchain

Thamani ya sarafu ya dijitali ya Bitcoin imewasisimua wengi kutokana na kutumia kwake teknolojia ya Blockchain.

Hii ni teknolojia salama ya kurekodi na kuthibitisha ununuzi na uuzaji pamoja na uhifadhi wa data muhimu.

Ina uwezo wa kuzima matukio mengi ya kihalifu kama vile wizi wa fedha kidijitali katika benki, wizi wa data, wizi wa kura na kutathimini utendaji wa wafanyakazi huku historia ya watumiaji  wote wa data ikionekana na kila mtumiaji.

Tayari kampuni nyingi duniani zinatumia teknolojia hii, lakini mwaka huu wadau wa teknolojia wanatarajia Blockchain kuanza kutumika kikamilifu hata na serikali na mashirika.

3. Magari ya kielektroniki

Kuna uwezekano mkubwa mno kuwa kufikia mwishoni mwa 2019, kila kampuni ya kuunda au kuuza magari itakuwa na magari ya kielektroniki kwenye maegesho yake ya mauzo.

Tayari kampuni ya Amerika ya Tesla inauza magari haya ambayo badala ya kutumia dizeli au petroli, yanatumia betri moja hutiwa kwa umeme wakati nguvu zake zimeisha.

Hii inawiana na ajenda ya kimataifa ya kutumia nishati safi na kukoma kutumia nishati inayotoa moshi.

Magari machache ya kielektroniki tayari yameingia Afrika Mashariki hususani Kenya lakini yanatarajia kuongezeka idadi yake mwaka huu.

Pia teknolojia ya magari yanayojiendesha yenyewe bila dereva mwanadamu yanatarajiwa kutua Afrika Mshariki mwaka huu.

4. Malipo ya kidijitali

Tayari tumeshuhudia malipo mengi yakifanywa kupitia Tigo Pesa, M-Pesa na Airtel Money, lakini huduma muhimu kama usafiri na ununuzi wa bidhaa umebakia kufanywa kwa kutumia sarafu na noti.

Huduma ya kulipia ugeshaji wa magari katika Kaunti ya Nairobi ya eJijiPay nchini Kenya na ile ya kutuma na kupokea hela kutoka benki tofauti ya Kenswitch zimeongoza katika malipo ya kidijitali.

Hata hivyo, baadhi ya kampuni nchini Uswisi zimewaweka wafanyakazi wake kidude mkononi ambacho kinatumika kulipia kila huduma na bidhaa.

Kampuni ya Google ina huduma kwa wateja inayoitwa Google Pay huku Apple Inc ikiwa na Apple Pay. Huduma hizi zinatarajiwa kuvumisha malipo ya kidijitali kupitia kwa simu.

Hivyo, Afrika Mashariki mwaka huu itashuhudia mapinduzi zaidi ya malipo ya kidijitali kutokana na fedha taslimu kuwa sumaku ya kuvuta wezi.

5. Uchapishaji wa 3D

Kwa Afrika Mashariki, teknolojia hii tayari ni maarufu katika mtaa wa Westlands, Nairobi lakini haijaenea sana kwingineko kwa kuwa Wakenya na raia wengi wa Afrika Mashariki bado hawajatambua uwezo wake.

Ni uvumbuzi unaokuwezesha kutengeneza vifaa vingi vya miundo aina tofauti kama vyombo vya jikoni, samani ya plastiki na vioo.

Lakini katika mataifa yaliyoendelea, teknolojia hii hutumika kujenga nyumba, kutengeneza viungo vya mwili katika matibabu huku pia ikiwa na uwezo wa kupika vyakula kama pizza.

Mtumiaji hutakiwa kuchora muundo wa chombo anachotaka kutengeneza kwa kutumia kompyuta kwanza. Kisha mashine ya uundaji hujazwa na viambato vya kutengeneza chombo hicho kama plastiki iliyosagwa kuwa uji kisha kubonyeza kitufe cha ‘Chapisha’.

Ikiwa teknolojia hii inatumika mijini, utaanza kuona uagizaji wa bidhaa nyingi kutoka mataifa ya nje ukipungua.

6. Uzinduzi wa mtandao wa 5G

Kizazi cha tano cha teknolojia isiyotumia waya inatazamiwa kutawala matumizi ya simu kote duniani.

Hii ndiyo teknolojia itakayochukua nafasi ya Wi-Fi, kwani itapunguza muda wa kutuma na kupokea data kwa intaneti kutoka milisekunde 30 hadi milisekunde moja.

Hii itaongezea uzito wa muunganisho baina ya mashine mbili kwenye mtandao.

Tofauti na Wi-Fi ambapo data inaweza kuzuia na kutekwa, 5G data itakuwa salama huku mtandao binafsi wa 5G ukiwezesha upakiaji na upakuaji wa data kubwa.

Kasi ya intaneti itakuwa juu zaidi na kutazama video ndefu au kuipakia kwa YouTube kutakuwa haraka zaidi, ukitumia kompyuta, tableti au simu.

Hivi karibuni kongamano la kimataifa kuhusu teknolojia lililofanyika jijini Las Vegas, Marekani wiki liyopita, kampuni mbalimbali zilionyesha namna intaneti hiyo ambayo itakuwa na kasi ajabu itainua ufanisi wa wa mitandao.

Ikianza kazi, intaneti ya 5G itawezesha watumizi wa mitandao kufanya mambo mbalimbali kwa kasi, takriban mara 10 zaidi ya ile ya 4G.

baadhi ya huduma ambazo zitanufaika na intaneti hiyo ni kama kuingia katika tovuti, kuchota’ nyimbo ama filamu ama kutazama filamu moja kwa moja mitandaoni.

Teknolojia hiyo inatarajiwa kuanza kufanya kazi Marekani kuanzia 2020, japo baadhi ya kampuni zimeeleza kuwa zinalenga kuanza kuitumia mwaka huu.

Kampuni ya Verizon ilisema kuwa intaneti hiyo ya 5G itasaidia hata katika sekta ya afya na madaktari wa upasuaji kurahisisha kazi ili kufikia habari muhimu za mazoezi hayo kwa haraka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles