20.8 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Matumizi mifuko ya plastiki mwisho Julai mosi

MWANDISHI WETU-DODOMA

SERIKALI imetangaza mwisho wa matumizi ya mifuko ya plastiki nchini kuwa Julai 1.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni jijini hapa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF), aliyetaka kujua ni lini mifuko hiyo itasitishwa matumizi yake.

Makamba alisema amepokea maagizo kutoka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu suala la upigaji marufuku mifuko ya plastiki na ameagizwa ndani ya wiki hii kukutana na idara za Serikali zinazohusika na jambo hilo.

Na hivyo ameandaa vikao na taasisi hizo ikiwemo TBS, Uhamiaji, Forodha, TRA, Polisi na Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kujadili vema ili ifikapo Julai 1 iwe ni mwisho wa matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini.

Awali akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Sima, alisema matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini yamekuwa na athari kubwa kwenye uharibifu wa mazingira na uchafuzi wa miji.

Alisema matumizi ya mifuko ya plastiki yameongezeka hasa kutokana na kutolewa bure kwenye maduka, masoko, migahawa na maeneo mbalimbali.

“Aidha, kutokana na baadhi ya nchi jirani kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki na kuruhusu uzalishaji kwa ajili ya soko la nje ya nchi, kumekuwa na wimbi kubwa la uingizaji wa mifuko ya plastiki hapa nchini.

“Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, imeanza kuchukua hatua zifuatazo katika kuelekea kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki: kuhamasisha wajasiriamali, vikundi vya kinamama na vijana, sekta binafsi na viwanda kuwekeza katika uzalishaji wa mifuko mbadala ikiwemo vikapu vya asili, mifuko ya karatasi na vitambaa. 

“Ofisi iliendesha mikutano miwili ya wadau katika mikoa ya Dar es Salaam Novemba 6, 2018 na Mwanza Desemba 18, 2018 na kuelimisha umma kuhusu changamoto na athari za mifuko ya plastiki na kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa mifuko mbadala kutokana na dhamira ya Serikali kusitisha matumizi ya mifuko ya plastiki katika siku zijazo,” alisema Sima.

Suala la matumizi ya mifuko ya plastiki limekuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kutoka kwa wadau ambao wamekuwa wakipinga.

Kutokana na hali hiyo kila wakati zimekuwa zikitolewa kauli mbalimbali ikiwamo kuondolewa kwa mazuio kadhaa kuhusu matumizi ya mifuko hiyo.

CHANGAMOTO ZA MUUNGANO

Katika hatua nyingine, Sima alisema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, imezipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali za Muungano.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Fakharia Shomar Khamis (CCM), aliyetaka kujua moja kati ya majukumu ya kuimarisha Muungano ni pamoja na kuhakikisha kuwa kero zote za Muungano zinatatuliwa.

“Licha ya vikao vingi vilivyokaa na kujadili kero hizo: Je, ni kero ngapi tayari zimetatuliwa na zipi ambazo hadi sasa zimeshindikana kupatiwa ufumbuzi?” alihoji Fakharia.

Kutokana na swali hilo, Sima alisema changamoto ambazo zimekwishapatiwa ufumbuzi ni 11 kati ya 15 zilizowasilishwa.

Alisema changamoto nne zilizobaki zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi.

Aliongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kumaliza changamoto zote zinazoukabili Muungano ili uendelee kuwa nguzo pekee ya kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa nchi yetu.

Waziri Makamba akiongeza majibu ya swali hilo, alisema ratiba na utaratibu wa vikao vya kushughulikia changamoto za Muungano vimeboreshwa.

Alisema kuna utaratibu mpya ambapo kikao kikubwa cha Makamu wa Rais ambacho ni cha Serikali zote mbili yaani Baraza la Mawaziri SMT na Baraza la Mawaziri SMZ kinakutana mara moja kwa mwaka.

“Kikao cha mawaziri kinakutana mara moja kwa mwaka, kikao cha makatibu wakuu wote kinakutana mara mbili kwa mwaka na kikao cha wataalamu wa Serikali zote kinakutana mara mbili kwa mwaka,” alisema Makamba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles