28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

ZAHERA: Nimewachoka

SOSTHENES NYONI-DAR ES SALAAM

Kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa timu ya Polisi Tanzania, kimemchefua kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ambaye ameamua kutangaza vita dhidi ya wachezaji wake ‘magoigoi’.

Yanga ilikutana na kichapo cha vijana hao wa Jeshi la Polisi, katika mchezo wa kirafiki uliochezwa juzi, Uwanja Ushirika, Moshi.

Zahera aliihitaji mchezo huo, ili kutengeneza muunganiko mzuri katika kikosi chake, hasa eneo la ushambuliaji kabla ya Yanga kurudiana na timu ya Township Rollers ya Botswana, katika mchezo wa pili wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaochezwa Agosti 23 jijini Gaborone.

Mchezo wa kwanza ulichezwa wiki moja iliyopita, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo Yanga ililazimishwa sare ya bao 1-1.

Ili kusonga mbele raundi ya kwanza, Yanga itatakiwa kuhakikisha inapata ushindi au sare ya kuanzia mabao 2-2 na kuendelea, katika mchezo wa marudiano.

Zahera anaamini kikosi chake kina uwezo wa kupata matokeo mazuri ugenini, lakini kwanza lazima ahahakikishe anatengeneza muunganiko mzuri wa wachezaji wapya waliosajiliwa dirisha la msimu ujao na wale wa zamani.

Udhaifu ambayo kwa sasa unamuumiza kichwa kocha huyo mwenye uraia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) na Ufaransa, ni kikosi chake kutengeneza nafasi nyingi za mabao, lakini zikishindwa kutumiwa vema na washambuliaji kuuweka mpira wavuni.

Hili ndilo lililomfanya kuwaomba mabosi wake michezo miwili ya kujipima ubavu, ukiwemo wa juzi dhidi ya Polisi Tanzania, ili kunoa zaidi makali ya kikosi chake kabla ya kuvaana na Township.

Akizungumzia kipigo cha juzi, Zahera alisema bado kuna wachezaji wamekuwa wakimwangusha kutokana na kutoonyesha kiwango cha maana, licha ya kuwapa nafasi mara kadhaa wathibitishe ubora wao.

“Nimekuwa nikitumia wachezaji tofauti tofauti ili kumpa nafasi kila mmoja kuonyesha uwezo wake, wapo ambao wameonyesha mchezo mzuri lakini wengine hawabadiliki.

“Tulipokuwa Zanzibar  kikosi kilichocheza mchezo wa kwanza kilishinda mabao 3, mchezo mwingine nilitumia kikosi kingine ambacho tulitoka sare ya bao 1-1.

“Ukweli ni kwamba kuna wachezaji hawataki kubalidika licha ya kwamba nimewapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao.

“Niseme wazi kwamba, itakuwa vigumu mimi kuwatumia, katika hilo sitakuwa na huruma hata kidogo, wataishia kukaa benchi,”alisema Zahera na kuongeza.

“Yanga hii nataka kila anayepewa nafasi aisaidie timu kupata matokeo mazuri lakini kinyume na hapo hakutakua na mtu wa kulaumiwa.”

Baada ya mchezo wake wa kwanza dhidi ya Township, kikosi cha Yanga kilitimkia Zanzibar ambako kilicheza michezo miwili ya kujipima ubavu dhidi ya timu ya Mlandege na kushinda mabao 4-1, kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 na Malindi.

Katika hatua nyingine, kikosi cha Yanga leo kitashuka tena dimbani kuumana na timu ya AFC Leopards, katika mchezo wa mwisho wa kujipima ubavu Kanda ya Kaskazini utakaopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Leopards inashiriki Ligi Kuu ya nchini Kenya.

Zahera amesema katika mchezo huo, atatumia kikosi tofauti na kile kilichopoteza kwa mabao 2-0 kutoka kwa Polisi Tanzania. Baada ya mchezo huo, Yanga itarejea Dar es Salaam kuendelea na matayarisho  ya mchezo wake wa marudiano dhidi ya Township.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles