Imechapishwa: Sat, Oct 7th, 2017

YANGA YAISHUTUMU BODI YA LIGI

NA CLARA ALPHONCE

KLABU ya Yanga imesema haijaridhishwa na uamuzi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kulikataa ombi lao la kutaka mechi yao dhidi ya Simba isichezwe katika Uwanja wa Uhuru.

Yanga waliiandika barua Bodi ya Ligi ikiomba mtanange huo upelekwe Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, kutokana na sababu za kiusalama zinazosababishwa na udogo wa Uwanja wa Uhuru.

Hata hivyo, licha ya kukiri hawajapokea barua ya ombi lao kukataliwa na Bodi ya Ligi, Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, alisema hawataridhishwa na majibu hayo.

“Tumesikia katika vyombo vya habari, ila bado hatujakubaliana nao. Hatujui tutachezaje, uwanja ni mdogo na una vitu vingi ambavyo kwetu tunaona vitaleta shida,” alisema Mkwasa.

Mkwasa aliongeza kuwa wanachosubiri sasa ni barua ya uthibitisho kutoka kwa Bodi hiyo na kama itakuwa imeamua mchezo huo uchezwe Uhuru, basi watacheza kwa shingo upande.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura, alisema wameamua kuacha mechi hiyo katika Uwanja wa Uhuru, huku akisisitiza sababu walizozitoa Yanga hazitoshi kuhamisha mechi hiyo.

“Uamuzi wa Bodi umezingatia kanuni ya sita, kuhusu uwanja ambapo mamlaka ya mwisho kuhusiana na mechi kuhama au haihami inabaki kwa Bodi ya Ligi na TFF. Kwa hiyo tumekaa na kutafakari baada ya kupitia maombi ya Yanga hatujakubaliana nayo kwa hiyo mechi itabaki kama ilivyo.

“Kumbuka kuhamisha mechi itawahusu na wapinzani ambao watalazimika kuifuata timu mwenyeji sehemu nyingine nje na uwanja wako ambao unajulikana, lakini vile vile bodi ya ligi italazimika kupeleka maofisa wa mechi kwenye kituo kingine,” alisema Wambura.

Alisema hata hivyo watakutana na Yanga kuzungumza nao juu ya suala la viingilio ikiwa tatizo waliloliona Wanajangwani hao ni katika suala la mapato kwa kuwa uwanja ni mdogo.

 

 

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

YANGA YAISHUTUMU BODI YA LIGI