Imechapishwa: Thu, Oct 5th, 2017

WENGER: BARCELONA IKIJIUNGA EPL TUMEKWISHA

LONDON, ENGLAND

BAADA ya kikosi cha Arsenal kupata ushindi wa 2-0 dhidi ya Brighton mwishoni mwa wiki iliyopita, kocha wa timu hiyo, Arsene Wenger, ametoa maoni yake kuhusu uwezekano wa Barcelona kujiunga na Ligi Kuu England, akikiri kwamba mambo yatakuwa magumu zaidi.

Kutokana na hali ya kisiasa huko Catalonia, kwamba jimbo hilo linataka kuwa huru kutoka nchini Hispania, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa baadhi ya klabu za jimbo hilo zikatafuta sehemu ya kwenda kucheza ligi yao kati ya England, Ufaransa, Hispania na Italia.

Taarifa ambazo zilisambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii nchini Hispania na England ni kwamba, klabu ya Barcelona inaweza kujiunga na Ligi Kuu nchini England, hivyo kocha huyo wa Arsenal amedai wababe hao wakipata nafasi hiyo wataifanya ligi hiyo kuzidi kuwa ngumu.

“Ninaamini Barcelona ikifanikiwa kutaka kujiunga na Ligi ya Uingereza, itafanya mambo kuwa magumu zaidi kwa kila mtu hapa, hakuna asiyejua uwezo wa klabu hiyo bora duniani.

“Lakini hadi sasa sidhani kama wamefikia uamuzi huo, ni suala la kuvutia na kuwa na visa kama hivyo kwa upande wa michezo kwa kuwa Barcelona ni klabu ya kisiasa zaidi,” alisema Wenger.

Hata hivyo, kocha huyo aliongeza kwa kusema kwamba, ingekuwa uamuzi wa kuwakaribisha Barcelona kwenye ligi hiyo ungekuwa wa kwake, basi wala hasingeweza kuwapa nafasi na angeamua kuzipa nafasi timu zile zinazoizunguka Uingereza.

“Hadi sasa kuna klabu 20 kwenye Ligi ya England, iwapo unataka kuongeza klabu nyingine na kufikia 24 ni vizuri ukaanza kuangalia klabu ambazo zipo karibu sana na nchini Uingereza kabla ya kukimbilia nchini Hispania, hivyo kama ningekuwa na nafasi hiyo nisingeweza kuwapa nafasi,” aliongeza.

Mapema wiki hii Rais wa klabu ya Barcelona, Josep Bartomeu, aliweka wazi kuwa endapo Catalonia watafanikiwa kuwa huru, basi klabu hiyo kuna uwezekano mkubwa wa kujiondoa kwenye Ligi ya Hispania.

Tangu maandamano ya Catalonia kufanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, baadhi ya klabu hazijafanya mazoezi hadi sasa ikiwa ni pamoja na klabu ya Barcelona, hivyo matokeo ya kura za maoni zilizopigwa yanatarajiwa kutoka hivi karibuni.

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

WENGER: BARCELONA IKIJIUNGA EPL TUMEKWISHA