Waziri ashangaa wanaohoji alipo mwandishi Azory Gwanda

0
423

MAREGESI PAUL-DODOMA

WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amewashangaa watu wanaohoji mahali alipo mwandishi wa habari wa Mwananchi, Azory Gwanda.


Amesema pamoja na kwamba watu hao wanataka kujua alipo mwandishi huyo, wanachotakiwa kujua ni kwamba, maeneo alikopotelea mwandishi huyo, walipotea watu wengi wakiwamo viongozi wa Serikali.


Dk. Mwakyembe aliyasema hayo bungeni jana alipokuwa akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2019/20.
“Mheshimiwa Spika, waheshimiwa wabunge wanahoji alipo Azori Gwanda. Hiyo ni kesi dhaifu sana kwani maeneo alikopotelea walipotea watu wengi wakiwamo viongozi wa Serikali, sasa iweje wawe wanahoiji alipo yeye badala ya wengine?


“Tunajua mnawalisha wazungu matango pori, ngoja wale na endeeleni kuwalisha, nawaambia hatutakosa chochote hata kama wakitushusha madaraja,” alisema Dk. Mwakyembe.


Kuhusu watu wanaokashifiwa na vyombo vya habari, Dk. Mwakyembe aliwataka waende mahakamani kwa kuwa huko ndiko haki inakopatikana.
“Kuna wabunge hapa wamelalamikia vyombo vya habari, kwamba vinakashifu watu, lakini Serikali haichukui hatua.


“Hivi kama gazeti limekuchafua unataka tuchukue hatua zipi, unataka dola ifanye nini, kama heshima yako imeshushwa nenda mahakamani.
“Pamoja na hayo, kwa mujibu wa sheria, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), ana mamlaka ya kusimamisha chombo kinachokiuka masharti ya uandishi wa habari, lakini wengi wanaofungiwa wanakimbilia kwa mabalozi kulalamika.


“Vile vile, ieleweke kwamba, kwa mujibu wa kifungu cha 59 cha sheria ya huduma za habari, waziri ana mamlaka ya kuzuia uchapishaji wa maudhui yanayohatarisha amani.
“Kwa hiyo, ikitokea tumekifungia chombo fulani cha habari, tusionekane kwamba tumekionea, bali tunafanya hivyo baada ya kuwaandikia barua nyingi za kuwaonya,” alisema Dk. Mwakyembe.


Kuhusu uhuru wa habari na kujieleza, aliwataka wananchi wafuate sheria kwani Serikali itaendelea kuvichukulia hatua vyombo vya habari pamoja na watu wanaokiuka sheria ya kutoa habari.


Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza, alisema Serikali itaendelea kuonyesha ‘Live’ ziara za Rais Dk. John Magufuli, licha ya baadhi ya watu kutaka zisionyeshwe.


“Kuna waheshimiwa wabunge wamehoji ziara za rais kuonyeshwa live. Naomba niwahakikishie kwamba, ziara hizo zitandelea kuonyeshwa ‘Live’ kwa sababu ni ziara za maendeleo,” alisema Shonza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here