WAFUGAJI WALALAMIKIA BEI YA MIHTASARI

0
5

Na RAMADHAN LIBENANGA-MOROGOROWAFUGAJI wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro, wamesema wamekuwa wakitumia fedha nyingi kununua mihtasari ya vikao vya vijiji ili kuzionyesha mamlaka mbalimbali jinsi walivyoruhusiwa kumiliki ardhi waliyonayo.
Hayo yalielezwa jana na mchungaji Joseph Sepuke, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Kibaoni wilayani Mvomero.

“Wamasai wanapata mihtasari ya kijiji kwa gharama kubwa na viongozi hawa hawa wa vijiji ndio wanaowauzia hii mihtasari ili waweze kumilikishwa maeneo.

“Kwa hiyo, tunaomba gharama za mihtasari hiyo zipunguzwe ili tuweze kuzipata kwa urahisi zaidi,” alisema Sepuke.
Awali, akizungumza katika mkutano huo, mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Kibaoni, Fabian Beatus, alisema kijiji chao kimegundua kuna baadhi ya wananchi walioghushi mihtasari ya vijiji na kufanikiwa kupata ardhi.

“Kuna watu wameghushi mihtasari kwa sababu sharti kuu linalomwezesha mwananchi kumiliki ardhi ni kuwa na muhtasari unaoonyesha vikao halali vya kijiji vilikaa kumjadilli na kuridhia kumpa eneo,” alisema.

Akizungumza katika mkutano huo, mfugaji mwingine wa jamii ya kimasai, Songambili Mfaume, aliwatupia lawama baadhi ya viongozi wa kijiji hicho kwa kusema wamekuwa wakimfuata awape milioni mbili ili wampe muhtasari aweze kumilikishwa eneo lake.

Hata hivyo, tuhuma hizo zilikanushwa na Kaimu Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Stephano Udoba ambaye alisema wamekuwa wakifuata taratibu wakati wa kuwamilikisha wananchi ardhi.

Akizungumza katika mkutano huo ulioandaliwa na Mradi wa Kuendeleza Kilimo katika Safu za Milima ya Uluguru (UMADEP) unaotekelezwa chini ya usimamizi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Ofisa Miradi wa UMADEP, Pesa Kusaga, alisema SUA inashirikiana na Serikali kuhakikisha migogoro ya ardhi inamalizika mkoani Morogoro.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here