27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

TFRA YAAGIZA MBOLEA KWA MAZAO MBALIMBALI

Na MWANDISHI WETU

TANI 55,000 za aina kuu mbili za mbolea zimeingizwa nchini awamu ya kwanza katika mpango mpya wa uingizaji mbolea nchini kwa mtindo wa zabuni na kwa pamoja, ili kufaidi athari chanya za ukubwa wa shughuli na faida zake, kwani inategemewa bei ya bidhaa hiyo itapungua vilivyo.

Kuthibitisha ahadi yake kwa wakulima ya kuwapatia mbolea ya bei nafuu na katika muda mwafaka, Serikali imeingiza nchini jumla ya tani 23,000 za mbolea ya kupandia na tani 32,000 za mbolea ya kukuzia kupitia mfumo mpya wa uagizaji wa mbolea kwa pamoja, lengo likiwa ni kudhibiti kupanda bei kwa  bidhaa hiyo kunakofanywa na walanguzi wa pembejeo na hivyo kuwezesha kuzingatia bei elekezi inayopangwa na serikali yenyewe  kuwanufaisha wakulima.

Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea Tanzania (TFRA), Lazaro Kitandu, akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam wakati zoezi la upakuaji wa mbolea hiyo likiendelea, amesema mpaka sasa jumla ya tani 55,000 za mbolea zimewasili nchini na nyingine ziko njiani.

Hii ni awamu ya kwanza ya kuingiza mbolea nchini kupitia mfumo mpya ya uagizaji mbolea kwa pamoja ambapo kampuni ya OCP S.A ya nchini Morocco imeingiza jumla ya tani 23,000 za mbolea ya kupandia na Kampuni ya Premium Agro Chem imeingiza tani elfu 32 za mbolea ya kukuzia.

“Mpaka sasa zoezi la kupakua mbolea ya kupandia (DAP) tani elfu 23 linaendelea vizuri na mara baada ya kumaliza kupakua mbolea hii tutaanza zoezi la kupakua mbolea ya kukuzia (UREA), ambayo ni tani elfu 32,” alisema Kitandu.

Aliongeza kuwa, Waziri wa Kilimo alipokuwa anaongea na waandishi wa habari mjini Dodoma na alisisitiza bei ambazo zimetolewa zisimamiwe na kila ngazi, kwasababu taasisi peke yake haiwezi kuwa na watu kila mahali, hivyo Tawala za mikoa, Serikali za mitaa mpaka Kijiji zitasaidia kusimamia bei ambazo zimetolewa.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa, serikali imewekeza   katika uagizaji wa pembejeo hizo na matumaini yake ni kuwanufaisha wakulima wake na si wachuuzi ambao wao hujali faida ya kipesa na si malengo mapana ya nchi ya kuzalisha mazao ya chakula na biashara ili iweze kuwa na uwezo wa kuuza mazao hayo nje  na kufanya maendeleo yake.

Kitandu vilevile alifafanua kuwa, kuhusiana na suala la bei ya mbolea hiyo ambayo itatangazwa kupitia vyombo vya habari kama vile magazeti, redio na televisheni na hivyo ili ziwafikie wananchi kwa marefu na mapana ya nchi, alitoa onyo kwa mawakala kuacha kujipangia bei kwa kuuza mbolea nje ya bei elekezi ya Serikali kwamba watachukuliwa hatua za kisheria kama kunyang’anywa leseni, kufungwa, faini au vyote kwa pamoja, kwani itakuwa ni kuihujumu serikali ambayo inataka wakulima wake wafaidike kwa maslahi mapana zaidi ya Taifa.

Serikali imeweka wazi kuwa, suala la pembejeo limefanyiwa mabadiliko ambayo kila mdau inabidi ayazingatie, vinginevyo  atajikuta katika matatizo yasiyotakikana.

“Mbolea hizi siyo mbolea za ruzuku, kwani wakulima wengi wamekuwa wakichanganya mbolea hizi na mbolea za ruzuku, kwani zinatakiwa kulipiwa zilivyo,” alifafanua na kuongeza kuwa mbolea hii imefanyiwa utaratibu wa kudhibiti toka kule inapotoka na hivyo serikali itahakikisha inauzwa kwa kulingana na bei ya soko la dunia na hivyo kusitokee ubabaishaji na udanganyifu kwa wakulima.

Awali wakulima walikuwa wanauziwa mbolea kwa kiasi cha Sh 70,000 hadi 100,000, lakini kwa mfumo huu mpya mbolea inatarajiwa kuuzwa kwa bei elekezi na ya chini ya kiasi cha kuanzia Sh 53,000 hadi 60,000 kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea na inategemewa wengi watamudu bei hiyo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles