TFF YAMPA ONYO MANARA

0
31

NA MWANDISHI WETU

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limeuandikia barua uongozi wa klabu ya Simba ya kumpa onyo Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wao, Hajji Manara, kwa kitendo chake cha kuwashutumu waamuzi wanaochezesha Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hatua hiyo imekuja baada ya siku chache Manara kuzungumza na vyombo vya habari akiwatuhumu waamuzi kutoitendea haki Simba katika baadhi ya mechi za Ligi Kuu, huku akionyesha vipande vya video akidai mwamuzi Heri Sasii, kuwanyima penalti mbili katika mchezo dhidi ya Yanga uliochezwa Jumamosi iliyopita.

Manara aliwahi kufungiwa kwa kutojihusisha na soka kwa kipindi cha mwaka mmoja na faini ya Sh milioni tisa na uongozi wa aliyekuwa Rais wa TFF, Jamali Malinzi, kabla ya kufunguliwa na Rais wa sasa, Wallace Karia.

Kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa TFF alisema ni kweli wamepeleka barua hiyo kwa uongozi wa Simba kumpa onyo msemaji wao huyo.

“Tayari Simba imewafikia barua hiyo tuna imani na uongozi wao kulifanyia kazi suala hilo kwani matukio hayo si mara moja kuyafanya kwa msemaji huyo,” alisema.

MTANZANIA halikuishia hapo, liliwatafuta viongozi Simba, ambapo kigogo anayeshika nafasi ya juu ya uongozi kwenye klabu hiyo alikiri  kwamba wamepokea barua hiyo na sasa wanaifanyia kazi na muda utakapokuwa tayari wataliweka wazi.

“Ni kweli tumepokea barua hiyo kutoka TFF, lakini kutokana na majukumu tuliyokuwa nayo ya timu yetu, tunashindwa kuwajibu na tutalifanyia kazi, baada ya mechi na Mbeya City tutakutana viongozi na kuliangalia hili suala limefikia wapi,” kilisema chanzo hicho.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here