25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

SOKO KUBWA SAMAKI AFRIKA MASHARIKI LIKO HATARINI

sHERMARX nGAHEMERA


Mwanza inafahamika sana nje ya Afrika na haswa Ulaya kwa uzalishaji wa samaki  ambapo minofu mingi ya bidhaa hiyo hupelekwa kuuzwa kwenye masoko ya huko.

Wakatri fulani hata filamu ilitengenezwa kuelezea umaarufu huo na kuhusishwa na usafirishaji silaha  katika Eneo la Maziwa Makuu.

Wakati huo huo nchi za Afrika zinaifahamu Mwanza kama ni chanzo kikubwa cha kitoweo cha dagaa ambao nchi kama tano hutegemea kupata kitoweo hicho toka Mwanza na minofu ya samaki wakavu.

Isitoshe wenye viwanda vya chakula cha kuku wanaifahamau Mwanza kuwa ni chanzo cha malighafi ya chakula cha kuku cha samaki (fishmeal) kutoka jiji hilo.

Kwa hiyo ni shida sana kwa siku za karibuni kuzungumzia maendeleo ya jiji la Mwanza bila kuhusisha mchango wa biashara ya samaki kwa eneo hilo la Afrika.

Hayo yote yanawezekana tu kutokana na kuweko kwa Ziwa Viktoria  ambalo lina sifa nyingi muhimu za kipekee na kuwa hazina kubwa ya chumi za nchi za Afrika Mashariki.

Ziwa Victoria

Kimaumbo na kijiolojia Ziwa Viktoria ni mbinyiko (depression)  mdogo  ambapo kwenye kina kirefu zaidi ni mita 84 au futi 276  na kina cha kwaida cha wastani wa mita 40  (futi 140) na ni ziwa linalomilikiwa na nchi tatu za Afrika ambapo Tanzania inamiliki asilimia kubwa ya 49 ya eneo la ziwa wakati Uganda ni asilimia 45na Kenya ni kidogo zaidi kwa kumiliki silimia 6 au kimaeneo ni kuwa Tanzania ni kilomita mraba 33,7000, Uganda 31,000 na Kenya 1,600.

Urefu wa ufukwe (shoreline ) ni wa  kilomita 7,144 na kuna visiwa ndani yake  vyenye urefu  wa asilimia 3.7 ya urefu huo.

Ikiwa na eneo la sura ya nchi kilomita mraba 68,000 ni ziwa  kubwa kupita yote la Afrika kwa eneo na ni ziwa kubwa la Kitropiki duniani na ni la pili kwa ukubwa kwa ziwa la majibaridi  baada ya lile la Superior la Amerika Kaskazini. Katika mabara ni ziwa la tisa la ndani (continental) kwa ukubwa duniani  kwa kuwa na kilomita za ujazo 2,750 wa maji.

Ziwa hilo hupata maji yake kimsingi kutokana na mvua na vijito zaidi ya 1000 katika eneo hilo la Ikweta na Mto Kagera , kwa upande wake wa Magharibi  kutokea Rwanda ndio mto mkubwa kupita yote inayoingiza maji.  Mto Nile ndio pekee unaotoa maji ya ziwa hilo kaskazini ya Ziwa hilo kwenye sehemu ya karibu na Jinja nchini Uganda.

Kuna dhana mpya kuwa huenda mto Kongo wa chini (underwater river) huwezesha ujazo wa ziwa hilo  kutokana na uwingi wa maji yake, ni dhana ambayo haijapatiwa ushahidi thabiti.

Kuna watu zaidi ya milioni 35  hutegemea maji ya Ziwa Victoria eneo la Afrika Mashariki ambao sasa wanatishiwa uhai wao na kupungua tija kwa ziwa hilo na kuharibika kwa mazingira yake kunakotokana na shughuli za kibiniadamu.

 Ziwa hatarini

Takwimu za ziwa hilo zinatisha  kwani kila anayefanya utafiti humo ziwani  huchanganyikiwa jinsi mambo yanavyokwenda kombo na hivyo mrama katika masuala mengi.

Miaka ya sabini ilikisiwa kuweko wavuvi 50,000 na wavuvi 12,000 kwenye ziwa lakini siku hizi kwa ripoti ya Taasisi ya Uvuvi wa Ziwa Viktoria au Lake Victoria Fisheries Organizatio n (LVFO) taasisi ya Jumuia Afrika Mashariki (EAC) ye nye jukumu ya kulinda hali ya ziwa kwa matumizi ya baadaye kuna wavuvi 200,000 na mitumbwi 60,000 na kila mwaka vyombo 2,000 vipya vinaingia kila mwaka.

Ni shughuli juu ya shughuli kuweza kuongoza utitiri huo wa watu na vyombo vyao kazi ambayo nchi za Jumuia hazijafanikiwa sana na hivyo kutishia uhai wa siku za usoni za  ziwa hilo.

Kwani sasa  sio mitumbwi ya kienyeji bali ni ile yenye injini za nje na makokoro ya uvuvi ambayo yameongeza kiasi cha tani za samaki wanaovuliwa kwa kiasi cha mara 10 na uharibifu kuongezeka kwa uchafuzi mazingira na uchafu wa viwanda vinavyojengwa kando ya ziwa (polution) pamoja na uchafu wa vinyesi vya wakazi wa Mwanza na miji mingine mingi  ilioko kando ya ziwa.

Maeneo mengi ya ziwa sasa samaki hawawezi kuishi kutokana na uchafuzi na sumu mabalimbali za viwanda na shughuli za kilimo zikiwamo mbolea na madawa ya pamba na kuhitaji usimamizi makini.

 Shirika la chakula Duniani (FAO)  linakisia kuwa zaidi ya watu 280,000 wanaajiriwa na shughuli za uvuvi zikiwamo wavuvi, waanika samaki, wakaanga samaki, wanunuzi na wachuuzi wa samaki, watengeneza nyavu , wajenzi wa mitumbwi, wafanya matengenezo ya mitumbwi  na wachuuzi wa samaki.

Viwanda  zaidi ya kumi vimejengwa kuchakata samaki kwenye ziwa lote kwa kuwasafisha, kuwakata kwenye minofu na kuwaweka kwenye maboksi  na kuwasafurisha samaki nje ya nchikwenye ndege za mizigo, kwenda soko kuu la Ulaya.

Taasisi ya LVFO inatoa taarifa kuwa zaidi ya Dola milioni 650 ikiwa ni mauzo ya samaki  na mazao yake kila mwaka hupatikana.

Changamoto

Uvuvi haramu usiozingatia maslahi ya muda mrefu na matumizi ya nyavu na mbinu za uvuvi usio endelevu wa makokoro  ndio changamoto  kubwa  kwani hupunguza sehemu bora za mazalio ya samaki.

Hivi basi mchanganyiko wa uvuvi usio endelevu na uchafuzi mazingira kwa pamoja umetishia uweko uvuvi  sadifu  na kufanya kiasi cha samaki na kipato chake kupungua sana.

Samaki wakubwa wamepotea ziwani  kwani  awali sangara wakubwa walikuwa na uzito wa kilo hadi 200  na kilo 50 miaka ya 80 lakini sasa ni chini ya kilo 10 na wale wa aina ndogo zaidi  aina  kama 100 uzao wao umefutika.

Wanunuzi  Ulaya wanataka minofu mikubwa na sio ya samaki wadogo na hivyo soko la samaki limeanguka vibaya huko na sasa kutegemea zaidi soko la Afrika ambao kila aina ya samaki na ukubwa wake huliwa. Baadhi ya viwanda vimefungwa na au wafanyakazi kupunguzwa kwa kukosa samaki wenye tija.

Kwa Wachuuzi dagaa ndio kipenzi chao kwani ujuzi wa kushugulika nao katika mazingira magumu unafahamika nahivyo biashara hiyo iko katika nchi tano ambao wafanyabiashara wake huja na kuchukua dagaa kwenda kuuza kwao.

Pamoja na hayo Wito umetolewa mwaka huu kwa wafanyabiashara kutoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zambia, Malawi na Uganda kujitokeza kununua dagaa waliofurika katika Soko la Samaki Kirumba Mwaloni, jijini Mwanza.

“Wateja wetu wengine wakuu ni kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini ikiwamo Dar es Salaam, Mtwara na Pwani, hao wote tunawakaribisha, dagaa wapo wa kutosha,” alisema Mwenyekiti wa soko hilo.

Dagaa na samaki wengine wakiwamo aina ya sangara wanaovuliwa katika Ziwa Victoria wameongezeka sokoni hapo tangu Novemba mwaka huu kutokana na ongezeko la maji ziwani kipindi cha mvua.

Hata hivyo, alielezea kuridhishwa na mahudhurio ya wafanyabiashara kutoka DRC akisema wamejitokeza saba katika kipindi cha wiki mbili na kwamba kila mmoja ameweza kununua magunia kati ya 100 na 1,000 yenye dagaa ya uzito wa kilo 100 kila gunia.

Naye muuzaji  mmoja wa dagaa katika soko hilo,  John Masunga alitoa wito kwa serikali   kulitangaza soko hilo la Kirumba kuwa ni la kimataifa na kupunguza ushuru wa bidhaa hizo ili kuvutia zaidi wanunuzi kutoka nje ya nchi.

Uchunguzi umeonesha kuwa Soko la Samaki Kirumba Mwaloni jijini Mwanza lina uwezo wa kuhudumia jumuiya ya wafanyabiashara wa samaki  zaidi ya 2,000 kwa wakati mmoja. Ni soko kubwa la samaki Afrika Mashariki.

Soko lina uwezo wa kuhifadhi magunia 80,000 yenye dagaa kilo 100 kila moja  na huhifadhi  aina nyingine ya samaki kama sato, kamongo na matunda na nafaka aina mbalimbali.

Ni kawaida kukuta foleni ya magari ya usafirishaji (malori) kutoka DR Kongo, Burundi na Rwanda yakibeba mzigo wa samaki.

Juhudi za pamoja

Takwimu  zinaonesha kwamba uzalishaji wa sangara kwa ajili ya soko la nje katika miaka ya 1990 ambapo hali ulifikia tani 500,000 kwa mwaka, lakini kiwango kimekuwa kikizidi kupungua kila mwaka kwa asilimia zaidi ya 10.

Isitoshe hata kiwango cha samaki wengine kwa  matumizi ya wananchi wa kawaida wanaolizunguka ziwa kimekuwa pia kikipungua na kutishia  uchumi na maisha yao.

Ziwa hilo linaweza kuendelea kuwa tegemeo muhimu la kiuchumi na kijamii kwa raia wake ikiwa  serikali zitaweka mikakati ya pamoja; ingawa hali hiyo ni muhali kutokana na nchi hizo kujali sana migogoro yao na kuendeleza ushirikiano wa kinafiki.

Matumizi ya  sera bora na  sheria moja ya uvuvi wa samaki na matumizi ya maji yake ni jambo bora la kufanikisha purukushani iliyojitokeza kwa muda mrefu sasa ya kutokujali  hali na matokeo kwa mazingira.

Ni ukweli usiopingika kuwa rasilimali za samaki na maji ya ziwa hilo haitambui mipaka iliyowekwa ya nchi za Tanzania, Kenya na Uganda na ukorofi wa wanasiasa wake.

Kwa kuwa na sheria moja ya matumizi ya rasilimali za ziwa na kuisimamia ipasavyo  sheria  itaepusha migogoro isiyo ya lazima baina ya jumuia za wavuvi katika nchi hizo.

Hivi karibuni viongozi wa kisiasa kutoka nchi za Uganda na Kenya walipendekeza kuanzisha mikakati ya kurekebisha sheria za usimamizi wa rasilimali za ziwa hilo kuepusha mgogoro baina ya nchi hizo.

Waziri Msaidizi wa Masuala ya Jumuiya (EAC) kutoka Uganda, John Maganda, alikiri kuwepo kwa mgogoro kuhusu uvuvi na matumizi ya maji ya ziwa hilo.

“Ziwa Victoria ni mali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, tunapata samaki, tunalitumia kwa usafiri kutoka Jinja, Uganda hadi Kisumu, Kenya na mpaka Mwanza, Tanzania hivyo lazima tuepushe migogoro iliyopo au inayoweza kujitokeza,” Maganda alinukuliwa akisema katika mkutano huo.

Lakini Tanzania inayo sheria mahsusi kuanzia mwezi Julai  mwaka jana inayoelekeza rasilimali zake zisichezewe  na watu wa nje  na hivyo kufanya  masuala kuwa magumu kidogo.

Wakati huo huo Mbunge wa Funyula, nchini Kenya, Paul Otwoma, aliunga mkono suala la nchi  wanachama kuwa na sheria moja ya matumizi ya rasilimali za ziwa hilo.

“Samaki hawajui mipaka… Wanazaliwa huku, wanaenda kule, sheria lazima ziwe na usawa kwetu sote  na kuwezesha leseni moja kutumika kwa wavuvi wote bila kuzingatia nchi wanakotoka,” anasema Otwoma.

Wadau pia wanaona haja kwa serikali za nchi za EAC kuwa na mikakati ya pamoja ya kukabili vitendo vya uvuvi haramu ukiwamo ule wa baruti na kutumia sumu katika Ziwa Victoria ili kuepusha uharibifu wa mazalia ya samaki, uchafuzi wa maji yake na athari za kiuchumi na afya kwa watu.

Wadau wanashauri nchi za Jumuia kuangalia uwezekano wa  kuwa na ndege ndogo au helikopta kwa ajili ya kufanya doria dhidi ya vitendo vya uvuvi haramu katika ziwa hilo badala  ya maboti.

“Kutokana na kasi yake, matumizi ya ndege yatawezesha kudhibiti uvuvi haramu tofauti na boti zinazotumika sasa ambazo haziwezi kwenda hadi katikati ya ziwa,” anasema.

Serikali ya Tanzania inashauriwa kufikiria mpango wa kuhamisha watu katika baadhi ya visiwa ili kurudisha  uoto wa asili unaochochea mazalia ya samaki ndani ya ziwa.

Taarifa  zinaonesha  visiwa ambavyo watu wanaishi na kuendelea kuharibu mazingira rafiki kwa mazalia ya samaki ni pamoja na Chitandele, Lyakanyasi, Nyazune, Bihira, Ikulu, Mfulubizi, Zilagula, Yuzu, Gembale, Nyamango, Chemagati, Chembaya na Lubalagazi katika mkoa wa Mwanza.

Mazingira yake yameharibiwa na watu waliojenga makazi kwa ajili ya shughuli za uvuvi wanadai wadau kwani samaki sasa hawawezi kuzaana kwenye kingo za visiwa hivyo kwa  kuosekana  miti iliyokuwa inasaidia kupatikana kwa vivuli na vipepeo ambao ni chakula  pendwa cha samaki vimetoweka.

Omary Myanza, Mratibu wa Mradi wa Hifadhi ya Mazingira katika Bonde la Ziwa Victoria (LVEMP), anahamasisha uanzishaji wa mabwawa ya samaki kando ya ziwa hilo kwa wingi kuliko ilivyo sasa ili kupata kitoweo .

Shirika la Muungano wa Wavuvi (FUO) mkoani Mwanza, linaamini kutumia sheria moja kutawezesha nchi hizo kunufaika zaidi na rasilimali za ziwa hilo na kwa usawa.

Juvenal Matagili, anasema hatua ya Tanzania kuweka kiwango (standard) cha nyavu zenye matundu yenye ukubwa wa inchi saba kuvua samaki huku na Uganda na Kenya zikitumia kiwango chao cha chini kikiwa nchi tano hakitoi uwiano wa mavuno sawa ya samaki katika ziwa hilo.

“Wanaotumia nyavu zenye matundu ya inchi tano wanavua samaki wadogo na wengi ikilinganishwa na wanaotumia nyavu zenye matundu ya inchi saba,” anasema Matagili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles