Imechapishwa: Sat, Jan 7th, 2017

SINACH JOSEPH HADI ROSE MHANDO: HUU NDIYO MUZIKI WA INJILI WENYE UPAKO WA WELEDI

sinach2

KAMA hii ni mikong’osio mahsusi inayomtukuza Mungu basi lazima ijitofautishe ili isiwe bora liende kwa kulipua kwa kuwa tu ndani ya nyimbo kumehanikizwa vibwagizo: “Haleluyah!” na “Amen!” weledi ndiyo unaohitajika kujinasibisha na upako.

Ikiwa toka mwanzo wanamuziki kama Rose Mhando hawakueleweka basi sasa katika nyakati hizi ni lazima wataeleweka tu kwani kuinjilisha kimuziki si kwa mikong’osio dhaifu kwa kuwa cha ‘Bwana’ kinapaswa kujiakisi kwa nguvu ya chema kinachojiuza, tofauti na kibaya kinachojitembeza kwa nguvu ya giza.

Utanielewa zaidi ukiamua kutafuta na kusikiliza nyimbo kadhaa za mwimbaji nguli wa Gospo kutoka Afrika Magharibi, mwanamama anayeitwa Osinachi Kalu a.k.a Sinach, mke wa Mchungaji Joe Egbu wa Kanisa la Christ Embassy, aliyeimba wimbo ‘I Know Who I am’.

Wimbo huo unasumbua kwenye wigo wa muziki hapa nchini kwa jinsi ulivyotengenezwa kwa mikito kama ya kijukwaani ndani ya studio, pia kichupa chake kikiwa kimejaa ubunifu usiopitiliza na kukengeusha upako unaotolewa na wimbo huo ambao ukiusikiliza hakika utakubariki sana.

Lakini suala hapa siyo uzuri wa nyimbo zake au huu unaotesa kwa sasa unaopendwa sana na watoto na akina dada, kama ilivyo kwa nyimbo nyingi zinazopendwa na kada hiyo kugubika mashabiki wengine wenye nasaba na makundi hayo.

Awali wakati Rose Mhando anaibuka na mihanikizo yake mbadala madongo yaliruka kutoka kwa wenye mtazamo mgando, wanaodhani kuwa ‘Gospo’ ni upako wa utakatifu dumavu lakini ni kama walisahau kuwa Mfalme Daudi aliwahi kupagawa na muziki, akacheza hadi viwalo vikamchojoka katika kuhanikizwa sifa na utukufu kwa Bwana.

Achana na mambo ya Mfalme Daudi, muasisi wa mfumo wa kwaya aliyefanya mambo makubwa kutokana na kutumia talanta ya karama yake ya kipaji cha muziki kilichompelekea kuwa Mfalme, kwa kutumia vyema fursa ndogo aliyopewa ya kutuliza mapepo ya Sauli kwa kinubi lakini sasa Sinach amekuja kumsemea Rose Mhando, kama kile alichokuwa anakifanya kilipitiliza basi cha Sinach mke wa Pastor sijui kitasemwa kuwa nini!?

Ni rahisi, Mungu ndiye aliyeumba muziki tena kabla hajamuumba binadamu ambaye hakumuimbia hadi alipokombolewa kwenye taabu, lakini shetani akauteka muziki baada ya kuasi kwa kuwa alipokuwa malaika wa utukufu anayeng’aa akiimbisha kwaya ya malaika Mbinguni alikuwa ‘Kwaya Masta’ aliyeimbisha wenzake.

Kama wewe unayesoma hapa ni muumini na unashangaa nilipoyatoa haya basi punguza uvivu wa kusoma maandiko na usigubikwe fikra mgando!

Kuna mengi yanayohusu kuimba kwenye Agano la Kale kuliko jipya lakini inafurahisha Sinach anapokuja sasa kumsemea Rose Mhando, hata kama hawajuani binafsi lakini hii ndiyo ‘Front’ tunayoitaka kwenye muziki wa Injili.

Weledi ukitamalaki kwa nyanja mtambuka ya mikong’osio inayojitofautisha na mgando wa zamani (Back). Kwani si imenenwa kuwa kuimba humpendeza Mungu naye hufurahishwa na kuachilia baraka zake sawa na sadaka na dhabihu impendezayo kama manukato mazuri!?

Mbarikiwe sana Sinach, Rose na waumini wote. Amen!

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

FACEBOOK

YOUTUBE

Translate »

SINACH JOSEPH HADI ROSE MHANDO: HUU NDIYO MUZIKI WA INJILI WENYE UPAKO WA WELEDI