MWIJAGE: ELIMU YA HAKIMILIKI, HAKISHIRIKISHI ITAWAKOMBOA WENGI

0
3

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM


SHERIA ya Hakimiliki na Hakishiriki imekuwa ikiwasumbua wengi hasa katika kujisimamia katika masuala mbalimbali ya ubunifu na yenye kuleta tija kwao.

Hili linawasumbua pia wasanii na wabunifu sanaa, ambapo baada ya sheria ya Hakimiliki ya mwaka 1966 kuthibitika kwamba ina mapungufu mwaka 1999 ilifanyiwa marekebisho.

Ambapo Bunge lilitunga sheria hiyo mwaka 1999 yenye sura 218 ya sheria Tanzania kama zilizvyorekebishwa mwaka 2002.

Hii ni kwa ajili ya kuleta manufaa zaidi na ulinzi wa kazi za wasanii zinazolindwa na hakimiliki na hakishirikishi na zingine zinazoendana na hizo.

Chini ya kifungu cha 2 © cha sheria hiyo ambacho kinazungumzia madhumuni ya kutungwa kwa sheria ni umuhimu kwa maendeleo ya wasanii na watunzi na wabunifu wote katika nyanja za nyimbo, maigizo na tasnia nyingine.

Pia kwa mujibu wa sheria hizo, kuna makundi makubwa mawili ya haki za wasanii zinazolindwa na sheria ambazo ni haki za kiuchumi na haki za kitamaduni ambazo mtunzi wa kazi hizo ana haki nazo.

Haki hizo zina msingi wa mkataba wa kimataifa wa Benne wa mwaka 1883 ulioridhiwa na Tanzania Julai 25 mwaka 1994, na kwa mujibu wa kanuni za kisheria za kimataifa hivyo Tanzania ina wajibu wa kutimiza yaliyomo katika sheria hiyo kama ilivyoridhia.

Hivi karibuni Shirika la kusimamia Mali za Ubunifu la Kanda ya Afrika (ARIPO) , Shirika la Hakimiliki bunifu Duniani (WIPO) wakishirikiana na wadau mbalimbali kutoka kwenye mashirika na vyuo taasisi za serikali na zisizo za serikali, waliandaa mkutano kuzungumzia suala zima la hakimiliki la bidhaa, kilimo na kazi za wasanii.

Katika mkutano huo ambao mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage,  alisema ili kufanikisha mpango wa uchumi wa viwanda ni vyema Watanzania wakaongeza ubunifu na kuutunza.

“Ni vyema ubunifu ulindwe kwani usipolindwa unaweza ukabuni na kutengeneza kitu saa sita mchana wengine wakawa wameshakinakili wakati wewe umetumia muda mwingi na gharama za kubuni bidhaa husika,” anasema Mwijage.

Anasema ni vyema Watanzania kuwa wabunifu na kuutunza ubunifu wao ili kutengeneza ajira nyingi kupitia sekta hiyo na kuzalisha  faida.

Anasema sekta ya ubunifu ina fursa ya kuzalisha ajira nyingi kwa kutumia nguvu kidogo ikilinganishwa na sekta zingine na kwamba Tanzania kwa sasa inafanya vizuri ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika.

Hata hivyo anawataka watendaji wa Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) pamoja na Ofisi ya Msajili wa Hakimiliki za Wagunduzi wa aina Mpya za Mbegu za Mimea (PBRO) kufanya vizuri zaidi ili nchi ipate faida na kutengeneza ajira nyingi kupitia sekta ya ubunifu.

Kwa upande wake Kaimu Msajili wa Hakimiliki za Wagunduzi wa aina mpya za mbegu za mimea (PBRO), kutoka Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Joyce Mosile, anasema ni vyema wagunduzi wa mbegu wakaendelea kugundua mbegu bora ambazo zitaendana na mabadiliko ya tabia nchi yaliyopo kwa sasa.

Anasema ni vyema kuhakikisha kwanza kunawekwa nguvu milki bunifu hasa kwa wabunifu wa aina mpya za mbegu ili kupata mbegu bora za mimea na kupata chakula na kuviwezesha viwanda kupata malighafi za kutosha.

Anasema kwa sasa wana maombi ya mbegu 76 kati ya hizo 73 tayari zilishapatiwa hakimiliki huku akiwataka watafiti na wagunduzi wengine kuendelea kutafiti.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Doreen Sinare, ana ni vyema wabunifu wote wakaingia katika mpango wa hakimiliki ili uweze kuwasaidia kazi zao zisiibiwe na mtu mwingine kwa kuwa teknolojia ya sasa imekuwa zaidi.

Mmoja wa washiriki, Inocent Nganyagwa, anasema wasanii wamekuwa ni watu wa kulalama kwamba wanaibiwa kazi zao lakini suluhisho ni kujisajili COSOTA na kuwa na hakimiliki ya kazi zao.

Anasema hiyo itasaidia si kwa wasanii pekee bali na wabunifu wengine kutunza na kulinda kazi zao ndani na nje ya nchi.

Anasema wasanii wengi wameshindwa kufahamu haki zao kutokana na kudurufiwa kazi na kusambazwa ikiwa wao ndio wabunifu wa kwanza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here