28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

MUGABE: NITAFIA ZIMBABWE

HARARE, ZIMBABWE


ALIYEKUA Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, amekataa kuishi uhamishoni akisema atafia nchini mwake, jambo lililofanya jeshi kumpa kinga ya kutoshtakiwa yeye na mkewe na pia amepewa stahili zote anazopaswa kupata kama mstaafu.

Awali ilielezwa kuwa Mugabe alikuwa anaombwa akaishi uhamishoni Zambia, jambo ambalo mkongwe huyo wa siasa za Afrika alilikataa.

Shirika la Habari la Reuter, jana liliripoti kuwa Mugabe alisisitiza kutoondoka nchini humo, badala yake apewe ulinzi wa kutosha yeye na familia yake na kinga ya kutoshtakiwa.

Chanzo cha habari cha Serikali kilichokuwa katika meza ya majadiliano, kilisema Mugabe alisema kwamba alitaka kufia Zimbabwe na hana mpango wa kuishi ugenini.

Kikizungumza hilo kwa hisia na kusisitiza, chanzo hicho ambacho hakikuwa tayari kutajwa kwa vile hakina mamlaka ya kufanya hivyo kilisema kuwa kwake ni muhimu sana kupatiwa usalama wa kuishi nchini, ijapokuwa hilo halitamzuia kusafiri ng’ambo akitaka au ikibidi.

“Mugabe anafahamu kuwa umma unamchukia mkewe na wengi wana hasira namna anavyoendesha maisha ya anasa pamoja na kuingilia siasa za ZANU-PF.

Katika hali hiyo, ilikuwa lazima kumhakikishia yeye na mkewe pia usalama,” chanzo kingine kilisema.

 

JESHI LATHIBITISHA KINGA

Jana jioni, Jeshi la Zimbabwe (ZDF), lilithibitisha kuwa Mugabe na mkewe wamepewa kinga ya kutoshtakiwa, na wameruhusiwa kuishi chini humo.

Msemaji wa ZDF, Kanali Overson Mugwisi, aliliambia Shirika la Habari la Marekani (CNN), kuwa makubaliano yamefikiwa na Mugabe, ikiwamo kinga ya kutoshtakiwa na kuhakikishiwa usalama wake na mkewe Grace.

Mugabe alitumia wiki nzima kujadili kuondoka kwake kwa amani baada ya shinikizo la chama chake na jeshi lililotwaa madaraka na kumweka kizuzini.

Katika majadiliano marefu ambayo awali maofisa wa jeshi walikuwa tayari kumsamehe Mugabe lakini si mkewe, majenerali walilazimika kwa shingo upande kumkubalia masharti yake, ikiwamo kutogusa mali zake zinazodaiwa kupatikana isivyo halali.

Baada ya kutangazwa kwa kinga hiyo, Mugabe atapatiwa marupurupu ya kustaafu, ikiwamo pensheni, makazi, posho ya likizo na usafiri, bima ya afya, usafiri wa ndege na usalama.

Chanzo kingine cha habari kilicho karibu na familia yake, kimesema kutokana na kuathirika kisaikolojia kulikotokana na mlolongo wa mambo uliomtokea kipindi cha wiki moja hadi kufikia kujiuzulu, Mugabe anatarajia kusafiri kwenda Singapore kwa uchunguzi wa afya yake wiki chache zijazo.

“Alikuwa asafiri Singapore katikati ya Novemba mwaka huu kabla ya jeshi kumweka katika kizuizi cha nyumbani,” kilisema chanzo hicho.

Mugabe amekuwa akisisitiza kuwa yeye na familia yake wanaishi maisha ya kawaida na hamiliki utajiri wowote nje ya Zimbabwe.

Lakini mgogoro baina ya Grace na mfanyabiashara mmoja wa Ubelgiji kuhusu pete ya dhahabu yenye thamani ya dola milioni 1.3, ulianika staili ya maisha ya anasa ya Mugabe na mkewe aliyepachikwa jina la “Gucci Grace” kwa sifa yake ya kufanya manunuzi ya bei mbaya.

 

UPINZANI KUMFUATILIA KWA KARIBU MNANGAGWA

Katika taarifa yake ya kwanza tangu kujiuzulu kwa Mugabe, chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change, kimesema kitamfuatilia kwa karibu rais mpya, Emmerson Mnangagwa.

Kimesema wakati kikiuchukulia kwa tahadhari urais wa Mnangagwa, anapaswa kutoiga uovu, rushwa na udhaifu mwingine wa utawala wa Mugabe.

Chama hicho kikuu cha upinzani kimemtaka Mnangagwa kuvunja misingi yote ya ukandamizaji iliyosaidia kumdumisha Mugabe miaka 37 madarakani.

 

IMF YANENA KUHUSU UCHUMI

Zimbabwe ambayo awali ilikuwa moja ya mataifa yaliyostawi kiuchumi, iliathirika na miongo kadhaa ya angukola uchumi kutokana na kile kinachoelezwa sera zilizotumiwa na Mugabe za unyang’anyaji wazungu mashamba na uchapishaji fedha uliosababisha mfumuko mkubwa wa bei.

Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF), lilisema ukuaji wa uchumi wa Zimbabwe unatishiwa na matumizi makubwa ya Serikali, viwango visivyokubalika vya kubadilisha fedha za kigeni na upungufu wa mageuzi.

“Hali ya uchumi wa Zimbabwe imebakia ngumu,” Gene Leon, Mkuu wa IMF nchini Zimbabwe alisema katika taarifa yake kwa Reuters juzi jioni.

“Hatua za haraka ni muhimu kupunguza nakisi ili kufikia kiwango endelevu, kuharakisha mageuzi ya kimiundo na kushirikiana na jumuiya ya kimataifa ili kupata msada unaohitajika wa kifedha.”

 

MNANGAGWA: TUMEFUNGUA UKURASA MPYA

Kwa upande wake, Mnangagwa, anayetarajia kuapishwa leo, amehutubia wafuasi wake akisema Zimbabwe imefungua ukurasa mpya wa demokrasia kamili.

Akiwahutubia mamia ya wafuasi wake katika makao makuu ya chama cha ZANU-PF, usiku wa jana, alisema: “Leo tunashuhudia mwanzo mpya wa demokrasia kamili nchini mwetu.”

Mnangagwa (75) aliyevuliwa nafasi ya umakamu wa rais na Mugabe Novemba 6, katika hotuba yake ya jana alisisitiza umoja na haja ya kuufufua uchumi.

“Watu wamezungumza. Sauti ya watu ni sauti ya Mungu,” Mnangagwa aliwaambia maelfu ya wafuasi wake.

”Hakuna aliye muhimu kuliko mwingine, wote ni Wazimbabwe. Ninaahidi kuwa mtumishi wenu. Ninawasihi Wazimbabwe wazalendo kuungana pamoja tushirikiane. Hakuna aliye muhimu kumzidi mwingine, wote ni Wazimbabwe.

“Tunataka demokrasia, kuukuza uchumi wetu, tunataka amani katika nchi yetu, na fursa za ajira kwa idadi kubwa ya watu wasio na ajira, nchini mwetu.”

Katika hotuba yake hiyo, iliyokolezwa na maneno yaliyokuwa yakitumika wakati wa vita vya uhuru wa nchi hiyo, Mnangagwa alilishukuru jeshi la nchi hiyo, ambalo liliingilia kati baada ya yeye kufukuzwa na Mugabe na kuweza kufanikisha hali iliyopo sasa kwa amani.

Aidha alifahamisha kuwa aliikimbia nchi hiyo baada ya kutishiwa maisha yake alipofukuzwa katika nafasi yake ya umakamu wa rais.

Hata hivyo, kwa wakosoaji, ushirika wa muda mrefu kati ya Mnangagwa na Mugabe unazusha shaka juu ya uhalisia wa mabadiliko yanayotarajiwa nchini Zimbabwe.

Mnangagwa alivuliwa madaraka yake kutokana na kile kinachodaiwa ni kuwa na mvutano wa kuwania nafasi ya kurithi madaraka ya urais, kati yake na mke wa rais, Grace.

Mgogoro ulivyoongezeka zaidi, ulilifanya jeshi kuingilia kati, na kuanzisha mchakato uliomlazimisha Mugabe kusalimu amri na kuachia madaraka.

 

WAZIMBABWE WAGAWANYIKA

Hotuba hiyo ya Mnangagwa ambaye si mgeni katika siasa za Zimbabwe, ilipokewa kwa hisia tofauti.

Ijapokuwa Mnangagwa alizungumzia kufanya kazi kwa ushirikiano, pia alinukuu baadhi ya kaulimbiu za chama chake, jambo ambalo halikuwapendeza wapinzani.

Ni kwa vile kaulimbiu hizo zimekuwa zikichukuliwa kwa kuwahesabu wapinzani kuwa si wazalendo kamili wa taifa lao na kuwahusisha na wageni na mabeberu.

Aidha baadhi ya wafuasi wa upinzani wanaamini Mnangagwa alihusika kwa kiasi kikubwa wakati wa mauaji ya maelfu ya watu, pale Mugabe alipokabiliwa na wapinzani wake katika miaka ya 1980.

Hata hivyo, Wazimbabwe wengi wanayo matumaini kuwa ataleta mabadiliko.

Gift Bvunzawabaya, muuza maua katika mitaa ya mji mkuu, Harare alisema: “Ninafikiri anaenda kufanya yale ambayo hayajafanywa na Mugabe. Tunamtaka rais huyo kutuunganisha na watu wengine na mabara mengine ili tuijenge nchi yetu.”

 

ISEMAVYO UJERUMANI

Mjumbe maalumu wa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani barani Afrika, Guenther Nooke, amesema ingawa Mnangagwa anatarajiwa kushinda katika uchaguzi ujao bila tabu, huo utakuwa ushindi wa kundi lilelile lililokuwa na ushawishi chini ya Mugabe, kwa kusaidiwa na China.

“Atapata ushindi kwa kutumia hila na vitisho na kisha, tutashuhudia madaraka yakihama kutoka kiongozi mmoja wa kiimla, na kuangukia mikononi mwa mwingine wa aina hiyo,” alisema mjumbe huyo wa Kansela Merkel.

Mnangagwa ambaye amekuwa mshirika wa karibu wa Mugabe tangu enzi za kupigania uhuru, anaandamwa na tuhuma za kuhusika katika visa vingi vya ukiukaji wa haki za binadamu vilivyofanywa na Serikali ya Mugabe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles