MTIBWA SUGAR YAKOLEZA MAUMIVU MBEYA CITY

0
419

NA MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM


TIMU ya Mtibwa Sugar imezidi kuiweka pabaya Mbeya City baada ya kuichapa mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa jana Uwanja wa Manungu,Morogoro.

Mabao ya Mtibwa Sugar yalifungwa na Stamil Mbonde, dakika ya nane na Ismaili Mhesa dakika ya 42, huku bao la kufutia machozi la Mbeya City likiwekwa wavuni dakika ya 48 na Eric Kyaruzi.

Ushindi huo unaifanya Mtibwa  kuendeleza kung’ara baada ya kutoka   kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo uliopita.

Mtibwa Sugar imefikisha pointi sita baada ya kucheza michezo mitatu, ikianza kuchapwa na Yanga mabao 2-1, kisha ikaichapa Prisons bao 1-0.

Matokeo hayo yanazidi kuiweka Mbeya City katika hali mbaya, ikisalia mkiani bila pointi, baada ya kucheza michezo mitatu na kupoteza yote.

Wagonga Nyundo hao wa jiji la Mbeya walianza msimu  kwa kucharazwa mabao 2-0 na Azam FC Uwanja wa Azam Complex, kabla ya kukubali kipigo kama hicho kutoka kwa Simba,Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ligi hiyo iliendelea pia katika viwanja vingine vinne, Stand United  iliilaza  Biashara United bao 1-0 Uwanja wa Kambarage,Shinyanga.

Bao la Stand United lilifungwa na Bigirimana Blaise, dakika ya 60.

Stand United  imefikisha pointi sita baada ya kucheza michezo mitatu, ikishinda miwili na kupoteza mmoja.

Coastal Union nayo ikiwa nyumbani ilijikuta ikilazimishwa sare ya bao 1-1 KMC Katika mchezo uliochezwa kwenye wa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Bao la Coastal Union lilipachikwa na Hamis Kanduru dakika ya 23, huku lile la KMC likitumbukizwa wavuni na Omari Issa dakika ya 79.

Kivutio kikubwa katika mchezo huo kilikuwa mwanamuziki, Ali Kiba ambaye alikuwa jukwaani akiishudia timu yake ya Coastal Union.

Tangu ajiunge na Coastal Union, Kiba alikuwa hajaonekana katika michezo  miwili ya awali dhidi ya Lipuli FC na Biashara United.

Maafande wa Jeshi la Magereza nchini,  timu aya  Tanzania Prisons  jana ilizinduka na kupata ushindi wao kwanza wa bao 1-0 dhidi ya Alliance,   mchezo uliopigwa Uwanja wa Sokoine,Mbeya.

Bao la Prisons lilifungwa na Laurian Mpalile dakika ya 20.

Prisons imefikisha pointi tatu baada ya kucheza michezo mitatu ya ligi hiyo, ikianza kwa kuchapwa na Simba bao 1-0, kisha kukubali kipigo kama hicho kutoka kwa Mtibwa Sugar.

Mchezo mwingine ulizishuhudia African Lyon na Kagera Sugar zikigawana pointi moja kila mmoja baada ya kutoka suluhu Uwanja wa Kaitaba , Bukoba.

Kagera Sugar imefikisha pointi nne baada ya michezo mitatu, huku Lyon kifikisha pointi mbili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here