MLIPUKO MPYA WA EBOLA DRC WADHIBITIWA

0
605

KINSHASA, DRC


WIZARA ya Afya nchini Kongo, imetangaza kwamba imefanikiwa kudhibiti virusi vya ugonjwa wa Ebola uliolipuka kwa wiki kadhaa na kusababisha vifo vya watu 89 Magharibi mwa nchi hii.

Taarifa hiyo imekuja, baada ya Agosti mosi mwaka huu wizara hiyo kutangaza kuwapo kwa ugonjwa huo katika eneo la Kaskazini mwa Jimbo la Kivu na mwishoni mwa wiki iliyopita ikatangaza tena ugonjwa huo kusambaa hadi katika mji wa Butembo ambao unakaliwa na mamilioni ya watu.

Hata hivyo, jana Waziri wa Afya, Dk.  Oly Ilunga Kalenga, alisema kwamba tangu Agosti 13, mwaka huu hakuna taarifa mpya kuhusu wagonjwa wapya na hivyo anaweza kusema kwamba hali imedhibitiwa katika kituo cha Mabalako.

“Tangu Agosti 13 mwaka huu hakuna kesi mpya iliyoripotiwa hivyo tunaweza kusema hali imetengemaa katika kituo chetu cha Mabalako,” alisema waziri huyo.

“Mpaka leo hii  taarifa tulizonazo ni za wagonjwa  129 na kati yao 31  wana dalili zake, 98  wametibiwa, 89  wamekufa  na  33 bado wamelazwa,” aliongeza Dk. Ilunga.

Taarifa mlipuko huo mpya ni mara ya 10 tangu ugonjwa huo uliripotiwe kuikumba nchi hii tangu mwaka 1976 na ulipewa jina hilo la mto mmoja uliopo Kaskazini mwa nchi hii.

Wasiwasi wa kusambaa ugonjwa huo uliibuka tena mwishoni mwa wiki iliyopita, baada ya kuripotiwa kutokea vifo vya watu wawili katika mji wa  Butembo, ambao ni mashuhuri kibiashara na ambao pia ni kiungo cha usafiri kwenda nchi jirani ya Uganda.

Katika tukio hilo mwanamke mmoja na mhudumu wa afya walifariki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here