23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mke wa Magufuli amwaga chozi akiaga walimu

MTZ Alhamisi new july.inddJonas Mushi na Bethsheba Wambura (RCT), Dar

MKE wa Rais, Janeth Magufuli,  amejikuta akimwaga machozi wakati akiwaaga walimu wenzake katika Shule ya Msingi Mbuyuni, jijini Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo, walimu walimweleza Janeth changamoto zinazowakabili ikiwamo suala kupunguza makato ya kodi ya mishahara (PAYE), posho ya kufundisha na kumtaka afikishe kilio chao kwa shemeji yao (Dk Magufuli).

Mama Magufuli, alijikuta akitokwa machozi  katika hafla ya kuagana na walimu wenzake, ambapo alisema kazi ya ualimu ni ngumu na kuahidi kufikisha kilio chao kwa shemeji yao.

“Naomba mfanye kazi kwa bidii naahidi kuwa haya matatizo ya walimu nitayachukua na kuyafikisha kwa shemeji yenu ili yafanyiwe kazi,” alisema Janeth.

Alisema amefanya kazi ya ualimu kwa miaka 17 na anaona kuna changamoto kadhaa kwa walimu, kwani kazi ya kukaa na watoto ni ngumu ambayo inahitaji moyo wa kujitoa na huruma ya hali ya juu.

“Kukaa na watoto hawa ni kazi ngumu sana, wanahitaji malezi mazuri na huduma nyingine mbali na kuwafundisha kama vile kuwapa chakula, mavazi na kuwatibia, ” alisema Janeth.

Aliwataka wazazi na walezi kutobweteka na elimu bure, bali wajue kuwa bado kuna majukumu ambayo wanapaswa kuyatekeleza kama vile kununua sare, vifaa vya kujifunzia na kuhakikisha wanapata chakula na mahitaji mengine muhimu.

Akielezea kuhusu maisha yake shuleni hapo, alisema yeye ni mwanafamilia wa shule hiyo tangu kuwa mwanafunzi hadi mwalimu aliyeitumikia kwa miaka 17.

“Mimi nitaendelea kuwa mwalimu na mwanafamilia wa shule ya Mbuyuni kwa sababu nina historia ndefu na nusu ya maisha yangu nimeishi hapa kwani nimesoma, nimefundisha na watoto wangu wote wamesoma na kumaliza shuleni hapa,” alisema

Akisoma risala ya walimu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Dorothy Malecela,  alisema hivi sasa walimu wanakabiliwa na matatizo kadhaa ikiwemo ya kutopandishwa madaraja kwa wakati, kucheleweshewa nauli wakati wa likizo, kucheleweshewa  mafao baada ya kustaafu na upungufu wa walimu hususani wa vitengo.

Alisema nyingine ni upungufu wa nyumba za walimu, vyumba vya madarasa, ofisi, matundu ya vyoo na madawati.

Pamoja na hali hiyo Mwalimu Dorothy, alimwomba Rais Magufuli, kurejesha posho za kufundishia, kupunguza kodi ya mapato ya mshahara, kupandishwa madaraja baada ya kujiendeleza tofauti na ilivyo sasa ambapo mwalimu hulazimika kufanya kazi kwa miaka mitatu.

“Walimu tunatambua jitihada za Rais Magufuli, ikiwemo ya kutoa elimu bure lakini tunaomba ayashughulikie matatizo ya walimu,” alisema Dorothy.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles