Imechapishwa: Thu, Oct 5th, 2017

MEXIME: YANGA HAWATOKI KAITABA

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Mexime, amesema licha ya kutopata matokeo mazuri tangu Ligi Kuu Tanzania Bara ianze msimu huu, watafufukia kwenye mchezo wao dhidi ya Yanga unaotarajiwa kupigwa Oktoba 14 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Tangu msimu huu uanze, Kagera Sugar haikuwahi kushinda mchezo hata mmoja, ambapo kwa sasa wanaburuza mkia kwenye msimamo wa ligi, wakiwa wamejikusanyia pointi mbili kati ya michezo mitano waliyocheza baada ya kutoka sare na kupoteza mitatu.

Timu hiyo inanolewa na kocha bora, lakini imekuwa ikipata matokeo yasiyoridhisha tofauti na msimu uliopita ambapo ilifanikiwa kumaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu huku ikijikusanyia pointi 53.

Msimu uliopita timu hizo zilipokutana raundi ya kwanza kwenye Uwanja wa Kaitaba, Yanga ilifanikiwa kutoa kichapo cha mabao 6-2, huku walipokutana mara ya pili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam walipokea kichapo kingine cha mabao 2-1.

Mchezo huo wa Oktoba 14, utakuwa wa kulipiza kisasi na kwa kuwa Kagera Sugar wanahitaji matokeo mazuri ili kuweza kujinasua katika nafasi waliyopo kwa sasa, wakati huo Yanga wakitaka kufuta makosa yao ya michezo ya hivi karibuni.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mexime alisema anafahamu ubora wa wapinzani wao, hivyo ni lazima wapambane kuhakikisha wanashinda mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

“Nafahamu Yanga ni timu nzuri na ina wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu, lakini wasitegemee kama watapata matokeo mazuri kwenye mchezo huo, mipango yetu ni kuhakikisha tunang’ara kwenye mchezo dhidi yao,” alisema Mexime.

Alisema kwa sasa anatumia muda huu kuyafanyia kazi mapungufu ambayo yalijitokeza kwenye michezo ya nyuma ili yasijirudie kwenye mchezo huo.

“Mchezo huo utakuwa mgumu na wenye ushindani mkubwa lakini ninawaandaa wachezaji wangu kisaikolojia ili wakapambane na kuleta matokeo mazuri,” alisema.

Mexime amewataka mashabiki wa timu hiyo waendelee kuwapa sapoti licha ya kutopata matokeo mazuri kwenye michezo ya ligi.

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

MEXIME: YANGA HAWATOKI KAITABA