23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MECHI KUBWA KWA LIVERPOOL KULIKO MANCHESTER UNITED

ADAM MKWEPU NA MITANDAO

TIMU ya Liverpool na Manchester United zitakutana tena leo wakati ‘Mashetani Wekundu’ wa Jose Mourinho, watakapozuru Uwanja wa Anfield.

Pointi saba tayari zinazitenganisha timu hizo mbili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, lakini mechi hii itakuwa mtihani wa uwezo wa Manchester United na Liverpool katika harakati zao kwenye mbio za ubingwa msimu huu.

Manchester United hawajashinda mechi nne za mwisho dhidi ya Liverpool katika michuano yote, ingawa mechi tatu za mwisho baina ya timu hizi maarufu ziliishia sare.

Mechi kama hii msimu uliopita ilikuwa sare tasa katika Uwanja wa Anfield.

Liverpool wameshindwa kuifunga United katika mechi sita za mwisho Ligi Kuu, mara ya mwisho walishinda Septemba 2013 katika Uwanja wa Anfield, Daniel Sturridge, alipofunga bao pekee la mechi hiyo.

Danny Murphy anaamini mechi hii ya leo  itakuwa ni kubwa kwa Liverpool kuliko kwa Manchester United kwani United tayari wameshavuna pointi nyingi na mwenendo wao wa sasa ni mzuri ukilinganisha na wapinzani wao hao.

Liverpool ni timu ambayo imekuwa ikipewa nafasi kubwa katika mbio za ubingwa baada ya kushinda wa mabao 4-0 dhidi ya Arsenal, lakini imekuwa tofauti kwa sasa.

Wameshinda mechi moja tu kati ya saba, baada ya mapumziko ya kimataifa, Reds sasa wanashika nafasi ya saba kwenye jedwali la Ligi Kuu, bila ya ushindi kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa na wameshatolewa kwenye michuano ya Kombe la EFL kufuatia mwenendo mbaya Septemba.

Pengo baina yake na klabu za Manchester zinazoshikilia usukani tayari ni pointi saba, ikiwa itakubali kichapo leo pengo litaongezeka hadi 10. Ikiwa bado ni mapema kusema chochote kuhusu jedwali la ligi, deni la pointi 10 litakuwa mzigo mkubwa kwa Liverpool kuzifukuzia City na United ambazo zitakuwa mbali sana.

Kusema mechi hii ni lazima ushindi haitakuwa haki kwa Liverpool, wamepoteza mechi moja Ligi Kuu msimu huu na wanapungukiwa pointi moja tu kutoka timu inayoshika nafasi ya nne.

Mfumo wa Jurgen Klopp hauruhusu timu kufungwa kirahisi, ingawa kushinda pia si rahisi, Mjerumani huyo huenda asibadili falsafa yake dhidi ya United wikiendi hii.

Safu ya ulinzi imekuwa tatizo la muda mrefu, Klopp amekiri kuwa anachoshwa na tatizo hilo, lakini tatizo jingine kwa Liverpool ni kupoteza nafasi nyingi mbele ya goli. Pointi nyingi walizopoteza ni katika mechi walizomiliki mchezo kwa kiasi kikubwa lakini hawakufanikiwa kuziona nyavu.

Sare dhidi ya Burnley na Leicester City na ile ya mapema msimu huu waliyopata dhidi ya Watford, Liverpool hawana jipya lakini watapambana kuweka rekodi dhidi ya mahasimu wao.

United imekuwa tofauti msimu huu na Liverpool hawajashinda tangu Agosti, Iwapo Mashetani Wekundu watacheza kwa kushambulia zaidi hali itakuwa mbaya kwa Vijogoo wa Anfield.

Kufuatia mwenendo mbaya msimu uliopita kwenye Ligi Kuu Uingereza, Manchester United ya Mourinho sasa inafidia muda waliopoteza na wanawapa presha mahasimu wao Man City.

Wakiwa wamepoteza pointi 23 msimu uliopita, United wameanza kampeni hizi kwa rekodi nzuri mbele ya mashabiki wao na mechi zao za ugenini wamekuwa wakifanya vizuri wakiwa wamepata sare ya 2-2 dhidi ya Stoke City, mechi pekee waliyotetereka.

Maswali bado yapo juu ya uwezo wao kuwania taji, City wameshajitwalia pointi nyingi katika mechi dhidi ya Chelsea na Liverpool, mechi ya wikiendi hii itakuwa jaribio kubwa kwa United kwani watakutana na moja ya mahasimu wao sita wakuu.

Ni kweli kwamba, timu ya Mourinho husambaratisha kila wanayekutana naye na mwendo wa mechi 10 bila kufungwa ni pamoja na mechi tisa walizoshinda, haijalishi walikutana na mpinzani gani, lakini mechi hii ya Anfield ndio mtihani wao wa leo.

United ina wastani wa magoli matatu kwa mechi katika Ligi Kuu Uingereza msimu huu na wapo nyuma ya Man City kwenye chati ya magoli, wamefunga mabao manne katika mechi sita.

United wana kikosi bora zaidi kuikabili Liverpool zaidi ya ilivyokuwa msimu uliopita, lakini Mourinho atalazimika kuwa mkali zaidi ili kuhakikisha wanashinda na kuwaongezea presha Man City.

Liverpool imepata pigo baada ya winga wao, Sadio Mane, kupata majera mara baada ya kumaliza adhabu yake na kuna uwezekano mkubwa akakaa nje wiki sita kuuguza majeraha aliyopata kwenye jukumu la kimataifa akiwa na Senegal.

Hapakuwa na matatizo makubwa ya majeruhi kipindi cha mapumziko ya kimataifa, ingawa Philippe Coutinho na Georgenio Wjnaldum walifanya mazoezi tofauti na kikosi cha Liverpool Alhamisi.

Dejan Lovren alitolewa kwenye mechi ya Croatia kufuzu dhidi ya Finland, lakini alicheza wakishinda dhidi ya Ukraine na anatarajiwa kuwa fiti wikiendi hii licha ya kukiri kuwa anaishi kwa dawa za kupunguza maumivu kabla ya mechi zote.

Nathaniel Clyne na Adam Lallana, bado wataendelea kukosekana kwenye kikosi cha Reds, Alex Oxlade-Chamberlain, anaweza kuanza mechi ya kwanza Ligi Kuu akiwa na klabu hiyo.

Manchester United wamepata pigo katika mapumziko ya kimataifa baada ya Marouane Fellaini kupata majeraha ya ligamenti akiwa Ubelgiji, jambo litakalompa Mourinho maumivu ya kichwa kwani Paul Pogba na Michael Carrick hawapo pia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles