25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Marufuku ya mifuko ya plastiki yaibua wafanyabiashara

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

WAFANYABIASHARA wa mifuko ya plastiki wameiomba Serikali kuangalia upya hatua yake ya kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo, kwa kuwa itaathiri soko la ajira itokanayo na mifuko hiyo.

Marufuku hiyo ilitangazwa rasmi Aprili 9, mwaka huu na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ambaye alisema Serikali imetangaza marufuku ya kutengeneza, kuuza, kuingiza na kutumia mifuko yote ya plastiki baada ya Mei 31 mwaka huu.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Mifuko ya Plastiki, Ramadhani Mussa alisema wamepokea marufuku hiyo kwa mshtuko mkubwa kwa kuwa imefanyika kwa haraka bila maaandalizi.

Alisema hatua hiyo imechukuliwa bila kuwashirikisha wadau hasa wauzaji na wasambazaji wa mifuko hiyo, ambao tayari walishanunua mzigo mkubwa, ambao hauwezi kumalizika ndani ya muda uliowekwa na Serikali.

“Tunaiomba Serikali yetu sikivu iangalie upya suala hili. Suala hili limekuja ghafla sana na hakukuwa na taarifa wala maandalizi.

“Kuna wafanyabiashara wana hifadhi kubwa sana ambayo tayari walishainunua kutoka kwa watengenezaji, ambayo itahitaji muda zaidi ya huo uliowekwa ili kumalizika,” alisema.

Alisema ni vyema Serikali ikaangalia upya uamuzi huo kwa kuwa kuna watu wengi wamejiajiri  kupitia uuzaji na usambazaji wa mifuko katika maeneo yote ya nchi.

Mussa alisema uamuzi huo umechukuliwa bila wafanyabiashara na wasambazaji kufahamishwa hivyo ni vyema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba kuangalia suala la kupitisha kanuni za kukazia marufuku hiyo.

Mfanyabiashara katika soko dogo la Kariakoo maarufu kama soko la mifuko, Abdulkarim Malik alisema ni vyema Serikali ikaangalia upya kwa kuwa tayari ilishapitisha agizo la kutengeneza mifuko inayoweza kuzalishwa tena kupitia viwanda vya ndani, ambalo ndilo lililokuwa likifuatwa.

Alisema katika suala hilo la marufuku ya mifuko hiyo ya plastiki, Serikali ilitakiwa kuangalia namna ya kuwasaidia wafanyabiashara waliojiajiri kupitia mifuko hiyo ambao wengine wana mikopo mikubwa benki ambayo waliichukua kwa ajili ya kununua bidhaa hizo.

“Kuna watu wamechukua hadi mikopo mikubwa benki na wamenunua hifadhi ya mifuko kutoka viwanda vya ndani, ambayo bado wanamzigo mkubwa. Agizo hili limekuja ghafla sana na limewavuruga sana wafanyabiashara,” alisema.

Alisema ni vyema Serikali iangalie upya uwezekano wa kutoa muda zaidi kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara, ikae na wenye viwanda pia ambao nao tayari walikuwa na malighafi nyingi kwa ajili ya uzalishaji wa mifuko hiyo na kutoa muda mrefu wa wastani ili wasiingie hasara.

Mfanyabishara mwingine, Nzogora Mbaruku alisema kabla ya agizo hilo la Serikali kupitia kwa Waziri wa Mazingira na Waziri Mkuu hawakuwahi kupata taarifa yoyote ambayo ingewapa tahadhari kuhusu namna ya kujiandaa katika hilo.

“Hatushindani na Serikali. Tunaamini Serikali yetu ni sikivu na inayojali raia wake. Hapa tulipo tuna hifadhi ya mifuko ambayo katika uuzaji wa kawaida inaweza kwisha hata baada ya miezi sita ijayo. Tunaomba ituangalie katika hili,” alisema.

Akitangaza marufuku hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema ifikapo Mei 31 mwaka huu, itakuwa mwisho wa matumizi ya mifuko ya plastiki kubebea bidhaa mbalimbali.

Akijibu hoja za wabunge walizozitoa katika mjadala wa bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2019/2020, alisema katika kipindi hiki hadi Mei 31, Serikali inatoa fursa ya viwanda kubadili teknolojia yao na wauzaji kuondoa mizigo yao au kumaliza kuuza yote.

Alisema ofisi Ofisi ya Waziri wa Nchi Makamu wa Rais itajiandaa kutumia kanuni chini ya Sheria ya Mazingira ili kulifanya katazo hilo kuwa na nguvu ya kisheria.

Majaliwa alisisitiza kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo ili kulinda afya ya jamii, wanyama, mazingira na miundombinu dhidi ya athari kubwa zinazotokana na taka za plastiki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles