LUKUVI AUNDA KAMATI MGOGORO WA KAZIMZUMBWI

0
458

NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM


WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ameunda kamati maalumu ya kushughulikia mgogoro wa ardhi unaohusisha wananchi wanaoishi karibu na Hifadhi ya Msitu wa Kazimzumbwi wenye hekta 4,860 uliopo Chanika na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na mwafaka wake utapatikana ndani ya siku 30 kuanzia leo.

Pia aliwataka wakazi wa eneo hilo kuacha kutoa fedha kwa baadhi ya watu aliowaita wajanja wajanja wanaozikusanya kwa wananchi wa maeneo yanayoguswa na mgogoro huo kwa madai kuwa wanaenda kuzitumia kwa ajili ya kuushughulikia.

Akizungumza mjini hapa jana na wananchi wa Mtaa wa Zingiziwa akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Japhet Hasunga, Mtendaji Mkuu wa TFS,  Profesa Dos Santos Silayo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, alisema wizara zinazohusika na eneo hilo zimeamua kuchukua uamuzi huo baada ya kupatiwa maagizo na viongozi wa juu kwa lengo la kuwasaidia wananchi hao licha ya mgogoro huo kuusababisha wenyewe baada ya kuipeleka Serikali mahakamani.

“Lengo la kuchukua uamuzi huu ni  kuhakikisha wananchi waliopo katika eneo hili wanaweza kuendelea na shughuli zao bila kusumbuliwa na msitu huo unahifadhiwa vizuri, sisi kama mawaziri hatutengui uamuzi wa mahakama isipokuwa tumeagizwa na wakubwa wetu tuangalie utaratibu mwingine wa kuwasaidia bila kugusa uamuzi wa mahakama. Tutafanya kazi hii ndani ya mwezi mmoja na tutakuja na jibu hapa,” alisema Lukuvi.

Kwa upande wake, Hasunga, alisema wameamua kuiachia Wizara ya Ardhi kutatua mgogoro huo kwa kuwa wananchi wameingia eneo la hifadhi na kufanya shughuli za kilimo.

“Eneo hili ni misitu na kitaalamu tunasema ni mapafu, msitu huu unaisaidia Dar es Salaam kuzalisha oksijeni na kufyonza hewa chafu ya mkoa huu na kitendo cha watu kulima ndani ya hifadhi hii ni kuudhoofisha,” alisema.

Hasunga alisema wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakifanya shughuli za kibinadamu na kusababisha wanyama wadogo wadogo na wadudu waliokuwamo katika hifadhi hiyo kutoweka.

Naye mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Abdala Salum, alisema wananchi 1,000 hawajahi kuishitaki Serikali na kwamba wahusika ambao ni 276 waliotajwa kufungua kesi na kushindwa ni miongoni mwa wapiga dili wanaotumia mgogoro huo kujinufaisha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here